Kwa mfano, TFF ingeweza kuangalia uwezekano wa kupata timu moja pinzani toka Ligi ya Afrika kusini na moja kutoka ukanda wa Afrika Mashariki Kisha kuwa na jumla ya timu 8….
RATIBA ya shindano jipya la Ngao ya Jamii inahusisha timu nne; Yanga,Simba,Azam na Singida Fountain Gate Fc. Ni michuano mipya ambayo itachezwa kwenye uwanja wa mkwakwani jijini Tanga. Michuano hii imebadilika kutoka mechi ya kufungua pazi la Ligi Kuu kwa kucheza Ngao ya Jamii. Sijui sababu za msingi kubadilishwa muundo wa mchezo wa Ngao ya Jamii lakini inawezekana Shirikisho la Soka Tanzania , TFF lingekwenda mbali zaidi ili kuchangamsha soka la Tañzania.
Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa mashindano hayo yanayoshirikisha timu nne za juu inawezekana kubadilishwa na kutanua zaidi kwa kuanzisha Super League yao ndani ya Tanzania.
Ni kwa vipi? Ikiwa timu nne zinazomaliza Ligi Kuu katika nafasi za juu maana yake zinahitaji washindani wengine ambao wana ubora au wamemaliza nafasi ya juu katika Ligi Kuu Yao.
Kwa mfano, miaka ya nyuma kulikuwa na mashindano ya Hedex, Mtani Jembe, Muungano na CECAFA ambayo yanaonekana kupoteza maana na mvuto. Kwa maana hiyo soka ni burudani ambayo inahitaji ubunifu zaidi kwa kuanzisha mashindano mfano ya Super League ya Tanzania.
Kwenye Super League ya Tanzania timu nne za Ligi Kuu zinaweza kuungana na nyingine mbili kutoka visiwani Zanzibar. Kikubwa hapa ni kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika sehemu moja ili kuepusha kuwachosha wachezaji kwa kusafiri kwenda sehemu ya kucheza.
NJE YA MIPAKA
Ikiwa timu 4 za Ligi Kuu zinaungana na mbili kutoka Zanzibar jumla zinakuwa sita. TFF wangeweza kutengeneza njia ya kualika timu nyingine mbili kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati au kusini mwa Afrika.
Kwa mfano, TFF ingeweza kuangalia uwezekano wa kupata timu moja pinzani toka Ligi ya Afrika kusini na moja kutoka ukanda wa Afrika Mashariki Kisha kuwa na jumla ya timu 8.
Timu hizo zinagawanywa katika Makundi mawili A na B kuwa nne kwa kila kundi. Mfano kualika timu kama TP Mazembe, Vipers, Kaizer Chiefs, Orlando Pirates, Nkana Red Devil, Al Hilal, na nyingine ambazo zinaweza kukubali kushiriki.
Mashindano hayo yanaweza kutumika kuziandaa timu zetu za Tanzania kwa kuzipatia maandalizi mazuri kuelekea mashindano ya kimataifa.
Vilevile mashindano hayo ni biashara ambayo kampuni zinaweza kudhamini na kuyapa thamani zaidi. Hii Tanzania Super League ni mashindano ya burudani ya soka huku wadhamini wakitakiwa kutoa marupurupu kwa timu zinazoshiriki kama njia ya kuhamasisha zaidi maombi ya kushiriki.
Mashindano hayo huenda yakatumika kuimarisha vikosi,kuvutia vipya vipya, kutangaza zaidi soka la Tanzania,kuvutia wataalamu,kuvutia wawekezaji na wadhamini pamoja na faida lukuki.
Ifahamike Tanzania imekuwa kisima cha mafanikio ya soka Afrika Mashariki, huku mashindano ya Jumuiya hiyo yakiwa hayaeleweki ni muhimu Tanzania kujiundia mashindano yake na kukaribisha timu za kigeni kushiriki kama ambavyo Simba na Yanga wanavyoalika kwenye matamasha yao.
Tanzania Super League itasaidia timu zinazoalikwa kutumia kama Sehemu ya maandalizi yao kwa msimu unaofuata. Hivyo wanapoalikwa wanaweza kuingiza kwenye programu yao ya kujipanga kwa msimu mpya.
Inawezekana ikiwa ushawishi wa TFF kwa wadhamini utakuwa umejipanga vema kuona fursa kubwa kuzidi hali ya sasa ya Ngao ya Jamii kwa timu nne zilezile za Ligi Kuu na hakuna la nyongeza wala kivutio kipya.