MASHINDANO ya EURO 2020 yanayoendelea katika miji mbalimbali barani Ulaya yametuleta mshtuko ambao kila kona dunia iliduwaa kwa muda ili kungojea hatima yake. Ni mashindano ambayo yamekuja katika nyakati ngumu, kwa sababu kibano cha idadi ya mashabiki viwanjani na muundo wa ukaaji vinazingatiwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa virusi vya corona. Angalau kwa sasa tunawaona mashabiki viwanjani, lakini bado mwendo ni wa kobe na furaha haijafika kwa asilimia 100.
Mojawapo ya matukio makubwa yaliyotokea katika mashindano hayo ni kuanguka kwa mchezaji Christian Eriksen wa Denmark wakati wa mchezo kati ya taifa lake dhidi ya Finland kutokana na tatizo la mshtuko wa moyo. Ulikuwa mchezo ambao mashabiki walijua utasisimua na kuoneshwa ufundi wa timu zao. Bahati mbaya Erikssen akiwa anatuliza mpira wa kurushwa pembezoni mwa uwanja ili aelekee lango la adui, ghafla akaanguka na kupoteza fahamu.
Mwili wake ulijitupa chini bila kinga yoyote. Jambo ambalo liliwashtua watu. Hata hivyo nahodha wake aliyekuwa karibu Simon Kjaer aliwahi kudhibiti shingo ya shingo ya mwanasoka huyo isiendelee kulala ardhini ili kumpa nafasi ya kuweka vizuri na kuepusha madhara zaidi. Yaliyotokea ni simulizi za kusitikisha katika soka.
Dunia imewashuhudia nyota kadhaa wakianguka viwanjani baadhi yao kupoteza maisha. Marc Vivien Foe nyota wa zamani wa Manchester City na Cameroon alipoteza maisha wakati mchezo unaendelea. Kutoka tukio la Foe hadi Erikssen ni wazi mabadiliko kadhaa yamefanyika ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa wachezaji wanaoshiriki mchezo kuwa na afya njema.
Utimamu na uimara wa miili yao ndicho kitu kinachosisitizwa zaidi. kwa hiyo timu ya madaktari zimekuwa katika maandalizi ya kutosha kukabiliana na matukio kama ya Erikssen kuliko ilivyo huko nyuma.
Mchezo wa soka miaka nyuma haukuwa na matukio ya namna hii. Lakini kutokea kwake yanatukumbusha kuwa yapo miongoni mwetu. Ni matukio ambayo si
kwamba yanawaumiza wachezaji na viongozi wao, bali mashabiki wa timu zote ambao kama binadamu husikitishwa na kutokea kwake.
Mpaka sasa nyota huyo angalipo hospitali akiendelea kupatiwa matibabu ambapo kocha wa tiu ya taifa ya Denmark, Morten Boesen ameviambia vyombo vya habari kuwa nyota wao Erikssen atawekewa kifaa maalumu cha ambacho kitaaluamu kinaitwa ICD kwa sababu mapigo ya moyo yamekuwa ya kasi kuliko kawaida.
Mwaka 2019 tukio lingine lilimhusisha beki wa Ajax Amsterdam, Daley Blind ambaye alipata tatizo la moyo, lakinio alirejea uwanjani Februari mwaka 2020 baada ya kuwekewa kifaa cha ICD. Blind naye yupo katika kikosi cha tiu ya taifa ya Uholanzi kinachoshiriki mashindano ya Euro 2020 na alicheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Ukraine.
Maka 2016 mchezaji mwingine wa mchezo wa Kriketi wa Uingereza, James Taylor naye alilazimika kukatisha maisha ya kucheza mchezo huo baada ya kuwekewa kifaa cha ICD kutokana na matatizo ya moyo.
Sasa, tukiachana na mashindano ya Euro tuangalie Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea katikla viwanja mbalimbali. Suala la Afya za wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara sioni kama limepewa kipaumbele.
Afya ya wachezaji wetu wakiwa uwanjani bado ni suala linalotia mashaka zaidi, huku Shrikisho la soka Tanzania halionekani kuchukulia uzito mkubwa matatizo ya wachezaji viwanjani.
TFF ndiye mlezi na msimamizi wa mchezo wa soka kote nchini pamoja na kuwasimamia wanachama wake ambao ni vilabu vya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Daraja la Pili na kadhalika.
Kwamba TFF na wanachama wake ambao ni vilabu na vyama vya soka nchini vinatakiwa kuliangalia kwa umakini tukio la kuanguka Erikssne. Mara nyingi tunaweza kudhani labda hayatatokea kwenye Ligi yetu, lakini ukweli ni kwamba mwili wa binadamu aitwaye mchezaji ni sawa na ule wa Erikssen.
Tofauti ya mchezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Erikssen ni malezi na elimu ya mchezo wa soka. Erikssen amekulia katika maizngira bora ya
vifaa,walimu,ataalamu wa saikolojia,wachua misuli,madaktari na huduma zingine ambazo zinamwezesha mchezaji kuwa bora zaidi ya kipaji anachokuwanacho.
Kwa mazingira hayo klabu nyingi Tanzania si jambo rahisi kukutana na wataalamu wa saikolojia au wachua misuli na wale wanaohusika na afya ya mwili na akili ya binadamu katika utendaji wa kazi kwa ufanisi.
Ndiyo maana mwezi uliopita taarifa kutoka moja ya klabu kubwa ya soka nchini ilibainisha kuwa kocha wao anahitaji wataalamu wa saikolojia kwa ajili ya kuwaweka sawa wachezaji wake.
Hilo lilikuwa na maana pamoja na kushiriki mchezo wa soka na kupata fedha nyingi bado mazingira ya utendaji wa kazi hususani miundombinu ya viwanja na elimu na rasilimali watu ni changamoto. Wachezaji wa Ligi Kuu wanapitia changamoto nyingi.
Makocha wengi wa timu za Ligi Kuu wanakabiliwa na kibarua kigumu, wakati wao wanajua kufundisha mbinu za mchezo na maendeleo ya mchezaji lakini suala la saikolojia ya wachezaji wao bado linahitaji wataalamu.
Vilevile, huduma za afya katika viwanja vingi ni duni kuanzia miundombinu na uongozi wa timu unavyochukulia masuala ya afya za wachezaji. Suala la majeruhi ya mchezaji si kuumizwa katika mchezo au mazoezini bali pia kuumia kihisia ausaikolojia yake. hilo ni jambo ambalo linahitaji kukutanishwa na wanasihi(wataalamu wa saikolojia) ambao wanafanya kazi ya kushughulikia afya ya akili.
TFF na wanachama wake wanatakiwa kujua suala la afya ya mchezaji ni la kwanza, na inapotokea tatizo la ghafla uwanjani haliwezi kutibiwa kwa kuweka barafu pekee ambazo mara nyingi zimekuwa zikionekana viwanjani.
Madaktari wa timu wanatakiwa kuwezeshwa kuwa na vifaa maalumu vya kukabiliana na matatizo kama ya Erikssen. TFF wanatakiwa kuketi na vilabu vya soka kuangalia mara mbili mbili suala la afya za wachezaji vinginevyo kuna siku tunaweza kupoteza wachezaji kutokana na matatizo mfano ya moyo kama Erikssen.
Ni muhimu TFF kukagua masuala la utabibu kwa matatibu wote wa vilabu vya Ligi Kuu. Vitengo vya afya vya vilabu vinatakiwa kuangalia suala la Erikssen kama sehemu yao ya kuonesha ujuzi na kuokoa maisha ya wachezaji sio kuzoea kujiandaa kwa matatizo madogo madogo kama mchezaji kuchubuka,kugongana na kuumia kwa kawaida.
Madatakari wa timu za Ligi Kuu Tanzania bara wanapaswa kujua kilichotokea kwa Erikssen kinawezekana kutokea kwenye viwanja vya Jamhuri, Majaliwa, Sokoine,Majimaji,Uhuru,Taifa,Kambarage,Kirumba na vingine.
Ni wakati wa TFF kuhakikisha wanajiandaa kuepusha kupoteza maisha ya wachezaji kama vile Marc Vivien Foe. Wanajiandaa kwa matukio ya Erikssen. Kama TFF,Vilabu na vyama vyama vya soka nchini vinadhani mchezo wa soka unahusu kuendesha na kumaliza ratiba bila afya za wachezaji basi kuna siku tutashudia maafa kizembe kabisa. Mwenendo wetu katika Ligi hauridhishi hususani suala la afya za wachezaji. Inaogopesha sana.