TFF, POULSEN WAKUBALIANA KUVUNJA MKATABA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen wamekubaliana kuvunja mkataba katika makubaliano ambayo ni siri kwa pande zote mbili.
Uamuzi huo umetangazwa leo (Februari 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Kocha Poulsen mbele ya waandishi wa habari.
Rais Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa shukrani za dhati kwa Kocha Poulsen kwa ushirikiano na mchango ambao ameutoa kwa Tanzania kuanzia kwenye mpira wa miguu wa vijana.
Naye Kim amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi cha miaka mitatu alichokaa nchini kuanzia Mei 2011 alipoteuliwa kuwa kocha wa timu za Taifa za vijana, na baadaye Taifa Stars.
Akizungumzia benchi jipya la ufundi la Taifa Stars, Rais Malinzi amesema linatarajiwa kutangazwa hivi karibuni likiongozwa na kocha kutoka nje ya Tanzania.
Amesema kwa upande wa mechi dhidi ya Namibia itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Stars itaongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi akisaidiwa na kocha Hafidh Badru kutoka Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Kocha Madadi amewaondoa wachezaji watano wa Yanga katika kikosi kilichotajwa awali ili wapate fursa ya kuitumikia timu yao kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri.
Wachezaji hao ni Athuman Idd, David Luhende, Deogratius Munishi, Frank Domayo, Kelvin Yondani na Mrisho Ngasa. Pia kipa Ivo Mapunda ameondolewa katika kikosi hicho baada ya kupata msiba.
Nafasi zao zimezibwa na wachezaji Abdi Banda (Coastal Union), Himid Mao (Azam), Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Said Moradi (Azam) na Shabani Kado (Coastal Union).
Taifa Stars itaingia kambini keshokutwa (Machi 1 mwaka huu) jioni kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam, na itaondoka Machi 3 mwaka huu alfajiri kwa ndege ya South African Airways na kurejea nchini Machi 7 mwaka huu saa 8.15 mchana.
TWIGA STARS IMEWIVA, SHEPOLOPOLO YATUA
Wakati Zambia (Shepolopolo) imewasili leo mchana (Februari 27 mwaka huu), Twiga Stars imesema mazoezi yamewaingia barabara tayari kwa mechi dhidi ya Wazambia hao itakayochezwa kesho (Februari 28 mwaka huu).
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itafanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni, na hakutakuwa na kiingilio.
Wakizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage na nahodha wa timu hiyo Sophia Mwasikili wamesema kikosi chao kimewiva kwa ajili ya mpambano huo baada ya kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi ya kwanza.
Twiga Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu jijini Lusaka kwa mabao 2-1, na inahitaji ushindi ili iweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika Oktoba mwaka huu nchini Namibia.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv itacheza raundi ya mwisho na Zimbabwe.
Msafara wa Shepolopolo una watu 26 ambapo wachezaji ni Anita Mulenga, Annie Kibanji, Carol Howes, Debora Chisanga, Emelda Musonda, Esther Mukwasa, Grace Zulu, Hazel Nali, Hellen Mubanga, Lweendo Chisamu, Meya Banda, Mirriam Katamanda, Misozi Zulu, Mupopo Kabange, Noria Sosala, Rachel Lungu na Susan Banda.
Viongozi ni Maclean Daka, Charles Bwale, Kaluba Kangwa, Enala Phiri, Cornelia Chazura, James Nyimbili, Besa Chibwe, Dorothy Sampa na Kabungo Katongo.