PAMOJA na udhamini mnono Dola milioni 4.5 (Sh. bilioni 5.85 za Tanzania ) kutoka Kampuni ya +One Fashion ya Marekani, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), bado limedai halina fedha kuandaa kambi ya timu ya taifa ya vijana chini 20, Ngorongoro Heroes.
Hii ni mara ya pili kwa TFF katika mwaka huu kuibuka kutembeza bakuli kuomba fedha za kusaidia timu zake mara ya kwanza ilikuwa kwenye maandalizi ya timu ya wanawake Twiga Stars iliyokuwa na mchezo wake dhidi ya Ethiopia na sasa Ngorongoro Heroes.
Kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa mwaka jana baina ya TFF na kampuni hiyo ya Kimarekani katika kipindi cha miaka minane, pamoja na mambo mengine utaliwezesha shirikisho hilo kupata fedha taslimu, motisha nyingine nyingi kwa timu zake mbalimbali ambazo ni Taifa Stars, ile ya wanawake, Twiga Stars na vijana, chini ya miaka 23, 20 na 17.
Hata hivyo, jana TFF imewataka wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, Taasisi binafsi na Makampuni kujitokeza kwa ajili ya kuisaidia timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes inayojiandaa na mchezo wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana.
Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema kuwa timu hiyo ili iweze kujiandaa vizuri timu hiyo inahitaji Milioni 45 ikiwa ni pamoja na kambi, chakula, posho nauli za kwenda na kurudi Malawi katika mchezo wao wa awali.
Alisema mpaka sasa TFF, haina hata shilingi moja ila bado wanaendelea na jitihada za kutafuta fedha hizo kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo ya vijana ambao ndio wachezaji wa timu ya Taifa ya baadaye.
Mwakalebela ametoa madai licha ya mkataba wa TFF na +One kubainisha kuwa timu za vijana wenye umri wa miaka 17 na 20 zinatakiwa kupata kiasi cha dola 25,000 (Sh. milioni 25) na pia fedha kama hiyo inatakiwa kupewa Twiga Stars.
+One pia iliahidi kutoa sare za kuchezea michezo 900, sare za mazoezi 900, soksi za michezo 1,200, soksi za mazoezi 1,200, suti za michezo 400 kila mwaka kwa ajili ya timu za taifa.
Licha ya kutogusia udhamini wa +One kwa timu za taifa na kutoweka bayana Ngorongoro, Mwakalebela amewaomba wadhamini kuisaidia timu hiyo hata kwa jezi, chakula na mahitaji mbalimbali.
Kauli hiyo ya katibu mkuu huyo imekuja wakati taarifa za mkataba huo uliosainiwa mwezi Juni 20 mwaka jana unatoa nafasi ya TFF kupata vifaa kwa ajili timu za taifa.
TFF imewasilisha maombi haya huku katika siku za karibuni kukiwa na malalamiko ya wadau kuhusiana na mapato na matumizi ya shirikisho hilo.
Shirikisho hili linapokea kila mwaka fedha za uendeshaji kutoka Fifa, Serengeti, benki ya NMB, Vodacom na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na mapato inamega asilimia 20 kutoka kwenye mapato ya milangoni kwenye mechi za Ligi Kuu na timu ya Taifa.
Katika hatua nyingine; Mwakalebela alisema wachezaji 27 wataondoka kwenda Manungu, Morogoro kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki na Mtibwa Sugar ikiwa ni maandalizi ya mchezo wao na Malawi mwezi ujao.
Aliongeza kuwa timu hiyo imeundwa na vijana hao wengi ambao waliokuwa kwenye timu zilizofanya vizuri kwenye michuano ya Copa Cocacola nchini Brazil na Afrika Kusini.
Mwakalebela alisema timu hiyo ya vijana ndio mwanzo wa kuwa na timu ya Taifa nzuri ambayo imeanzia chini na ina msingi yote na wenye uwezo wa hali ya juu tofauti na sasa.