*Lalana nje wiki sita
*Khedira apunguza madai ili ajiunge Arsenal
*Thomas Vermaelen kubadilishwa na Nani?
*Madrid wawataka Romelu Lukaku na Falcao
Liverpool wanaojaribu kuziba pengo la Luis Suarez kwa kusajili wachezaji wengi, wamepata pigo baada ya kiungo wao mpya wa kimataifa wa England, Adam Lalana kuumia goti.
Lalana aliyesajiliwa kwa pauni milioni 25 kutoka Southampton aliumia kwenye mazoezi timu ikiwa katika ziara nchini Marekani na sasa atakosa mechi za mwanzo za Ligi Kuu inayoanza mwezi ujao.
Lalana (26) alijiunga na klabu hiyo mwezi huu lakini hatahitaji upasuaji, japokuwa lazima atulie kwa ajili ya tiba kufanya kazi yake. Alicheza kwenye mechi za England katika fainali za Kombe la Dunia, ambapo England walitolewa baada ya mechi mbili tu.
Liverpool wamekubaliana pia kumsajili mlinzi wa Southampton, Dojan Lovren kwa dau la pauni milioni 25, baada ya Saints kusuasua wakikataa kumuuza beki wao huyo, kwani klabu imebomolewa kwa wengi kuchukulia, akiwamo Rickie Lambert aliyehamia Liverpool pia.
Liverpool walikuwa katika mchakato wa kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa QPR, Loic Remy ambaye amekwama kwenda Arsenal kwa sababu ya kutaka mshahara mkubwa ambao Arsenal hawapo tayari kumpa.
Arsenal nao wanamchukua kiungo Morgan Schneiderlin kutoka klabu hiyo hiyo, lakini pia wapinzani wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur wanamfukuzia. Kocha mpya wa Southampton, Ronald Koeman amekuwa katika wakati mgumu, akikataa kuuza wachezaji lakini shinikizo likizidi na fedha kuongezeka huwaachia.
Katika hatua nyingine, Louis van Gaal anataka kumchukua nahodha wa Arsenal, Thomas Vermaelen ambaye Wenger anasema kwamba gharama yake ni pauni milioni 12 lakini hataachiwa kabla ya mabeki wengine wa kati walio likizo hawajarejea kazini.
Hata hivyo, Man U wanaweza kupata wepesi baada ya Arsenal kutafakari kumchukua winga wao, Nani katika sehemu ya dili la kumwondosha Vermaelen. Van Gaal anadaiwa kumworodhesha Nani miongoni mwa wachezaji 10 wanaotakiwa kuuzwa ili kupunguza gharama ya mishahara.
Danadana za Sami Khedira zinaendelea, ambapo inasemekana amewaambia Arsenal kuwa yupo tayari kupunguza madai ya mshahara kwa wiki hadi pauni £134000 badala ya zile za awali £150,000 kwa wiki.
Khedira amebakiza mkataba wa mwaka mmoja Real Madrid lakini anaona nafasi yake kucheza inaweza kuwa finyu kutokana na usajili unaoendelea kufanywa, ukiwa ni pamoja na wa mfungaji bora wa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia, James Rodriguez anayeweza kucheza kama winga na kiungo mshambuliaji.
Real Madrid wamejitokeza tena kutaka kuwasajili washambuliaji Radamel Falcao wa Monaco kwa mkopo na kumnunua Romelu Lukaku ambaye anaonekana hatakiwi Chelsea lakini wanadai bei yake ni pauni milioni 30.