*Pogba atoa barua kutaka kuondoka Juve
- Pellegrini shinikizo chini, Ibe atia wino
Kocha wa Real madrid, Carlo Ancelotti amesema hajui kama atabaki kuwa kocha wa klabu hiyo iliyotema ubingwa wa Ulaya Jumatano hii.
“Sijui kama nitakuwa hapa msimu ujao. Tuna siku 15 zimebaki tumalize ligi kuu na baada ya hapo tutazungumza na klabu. Leo hakuna haja ya kuzungumza juu ya hatima yangu,” akasema Ancelotti.
Ancelotti huenda akakosa kombe lolote msimu huu, kwani hata kabla ya kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Juventus, keshakosa Kombe la Mfalme.
Kwenye La Liga nako mambo yameenda kombo, wakiwa nyuma ya Barcelona kwa pointi nne huku zikiwa zimebaki mechi mbili.
Mtaliano huyo alishuhudia vijana wake wakivuliwa ubingwa na Wataliano wenzake, Juve, kwa kwenda sare ya 1-1 Santiago Bernabeu huku wakiwa wamepoteza mechi ya mkondo wa kwanza kwa 2-1 ugenini San Siro.
Ancelotti amepata kuwafundisha Juventus na Chelsea msimu uliopita aliwaongoza Real kutwaa Kombe la Mfalme, Kombe la Dunia la Klabu na ubingwa wa Ulaya.
Kiungo wa zamani wa Chelsea, Kevin De Bruyne anatarajiwa kurudi Ligi Kuu ya England (EPL).
Mchezaji huyu wa kimataifa wa Ubelgiji anayechezea Wolfsburg anawindwa na Manchester City walio tayari kutoa pauni milioni 35.
Hata hivyo, City wana ushindani kutoka kwa wapinzani wao ndani ya EPL, Arsenal na Manchester United wanaotaka kuimarisha eneo lao la kiungo kwa kumchukua De Bruyne, 23.
Mchezaji huyu anasema alifanya uamuzi sahihi kuondoka Chelsea Januari mwaka jana na hatarajii kurudi tena huko, pengine kwa vile hawaivi na kocha Jose Mourinho.
Mchezaji wa Juventus, Paul Pogba anaelezwa kwamba amewasilisha barua ya kutaka kuondoka klabuni hapo wakati Juve wakisherehekea kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Man City wanamtafuta mchezaji huyo wa zamani wa Man United kwa udi na uvumba na maofisa wake wamekwenda Torino kujadiliana na wale wa Juve juu ya fedha kiasi gani wanataka au wawape mchezaji gani.
Habari zilizotokea sasa zinasema kwamba Arsenal na Man United nao wameonesha nia ya kumtaka mchezaji anayeonekana kwamba anatakiwa zaidi sasa duniani.
Arsenal wamepata pigo kwa mahitaji yao ya huduma za mshambuliaji wa Palermo, Paul Dybala, kwani klabu hiyo imesema kwamba Juventus wapo katika nafasi nzuri zaidi ya kumpata.
Kocha wa Besiktas na beki wa zamani wa West Ham, Slaven Bilic yupo tayari kwa mazungumzo na klabu yake hiyo ya zamani ili achukue mikoba ya Sam Allardyce anayetarajiwa kuondoka kiangazi hiki.
Kiungo wa Manchester City, Frank Lampard, 36, atavuna mshahara wa pauni milioni 3.8 kwa mwaka atakapojiunga na klabu dada ya New York City msimu huu wa kiangazi.
Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini, 61, anatarajiwa kubaki kwenye nafasi hiyo msimu ujao, kutokana na mapitio ya hali ya timu yaliyofanywa na wakuu wa Etihad.
Mkurugenzi wa Soka wa QPR, Les Ferdinand amesema mfungaji wao bora, Charlie Austin, 25, hatauzwa kwa bei rahisi, licha ya klabu hiyo kushuka daraja.
QPR wamevunja mkataba wa mkopo na mshambuliaji wa West Ham, Mauro Zarate, 28, baada ya kuonesha hasira na kutoka uwanjani Anfield kutokana na kutopangwa kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Liverpool.
Swansea wamsema kipaumbele chao katika majira haya ya usajili ni kuhakikisha kocha wao, Garry Monk anabaki na kusaini mkataba wa muda mrefu kwa klabu hiyo ya Wales.
Winga wa Liverpool, Jordon Ibe, 19, amekubali mkataba mpya na klabu hiyo na anatarajiwa kusaini kubaki Anfield kwa miaka mitano zaidi.
Mkurugenzi wa Soka wa Southampton, Les Reed ana imani kwamba beki wao wa kulia anayetakiwa na Manchester United, Nathaniel Clyne atabaki klabuni hapo na kusaini mkataba mpya kabla ya uliopo haujamalizika mwakani.
Chelsea wamempa ofa ya mkataba wa miaka mitano mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Vijana ya England (U-21) Patrick Bamford, 21, aliye kwa mkopo Middlesbrough.
Bamford ananyemelewa na klabu za Everton, Aston Villa na Crystal Palace.
Winga Mreno wa Manchester United, Nani, 28, aliye kwa mkopo kwao katika klabu ya Sporting Lisbon anatarajiwa kurudi Old Trafford, na kuongezea United mzigo pauni milioni 17 katika mishahara. Nani amesema hataki kubaki Lisbon.