*Alex Song ajiunga West Ham, Remy Chelsea?
*Agger arudi Denmark, Blind atua Man United
Kiungo wa zamani wa Arsenal, Alex Song, amesajiliwa kwa mkopo na West Ham kutoka Barcelona.
Song (26) alitambulishwa kwa washabiki kabla ya mechi dhidi ya Southampton Jumamosi hii, na amesema kwamba hiyo ni klabu inayoelekea kuwa kubwa katika muda mfupi ujao.
Hata hivyo, Song aliyeondoka Arsenal 2012 amesema kwamba anahitaji muda kuwa fiti ili awape raha washabiki wa klabu hiyo ya mashariki mwa London. Alichezea Arsenal mechi 206 tangu 2005 wakati Nou Camp amecheza mara 39 tu.
West Ham, maarufu kama Hammers wameeleza kwamba walipambana na klabu kadhaa kubwa zaidi za Ulaya hadi kufanikiwa kumsajili Song kwa mkopo wa msimu mmoja. Song ameeleza kufurahishwa na ukweli kwamba klabu watahamia Uwanja wa Olimpiki kutoka walipo sasa msimu wa 2016/17.
Song anaingia West Ham kukutana na wengine wapya ambao ni Mauro Zarate, Cheikhou Kouyate, Enner Valencia, Diafra Sakho, Carl Jenkinson kutoka Arsenal, Aaron Cresswell na Diego Poyet.
AGGER WA LIVERPOOL ARUDI KWAO DENMARK
Mlinzi wa Liverpool, Daniel Agger amerudi kwao Denmark, ambapo atachezea klabu ya Brondby.
Agger (29) ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya hapa na pale kwa miezi 12 iliyopita, alilia kumwomba bosi Brendan Rodgers amruhusu aondoke klabuni hapo, baada ya kubaini hangepata nafasi kubwa kwenye kikosi cha kwanza.
Alikuwa akihusishwa na uwezekano wa kusajiliwa Arsenal, lakini haikutokea, na sasa ameshaondoka Liverpool kurudi nchini mwake, lakini amesema imekuwa ngumu kwake kuondoka kutokana na jinsi alivyoipenda na kukaa Liverpool kama nyumbani.
“Imetokea fursa kwangu kurudi nyumbani, nami nikaona katika hatua hii ni vyema nikafanya uamuzi wa kurudi kucheza huko,” alisema Agger.
Mchezaji huyo alikuwa akikataa kuondoka Anfield siku zilizopita, hata baada ya Manchester City kutaka kumsajili, lakini baada ya Liverpool kumsajili beki mwenzake, Dejan Lovren anayepewa kipaumbele zaidi kwenye ngome, ameona ni wakati mwafaka kuondoka.
Mdanishi huyu alijiunga Liverpool kutoka Brondby mwaka 2006 kwa £5.8m, akacheza mechi 232 kwa klabu hiyo ya Merseyside. Brondby wamesema katika taarifa yao kwamba amekubali kupunguziwa mshahara kwa kiasi kikubwa.
DALEY BLIND AINGIA MAN UNITED
Manchester United wamefikia makubaliano na Ajax kumsajili mchezaji Daley Blind kwa £13.8m. mchezaji huyu ni Mdachi aliyewika na Lous van Gaal kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil hivi karibuni.
Blind (24) hucheza kama beki wa kushoto au kiungo mkabaji. Licha ya makubaliano baina ya klabu mbili hizo, bado mchezaji hajakaa na Man U kujadili maslahi yake binafsi na pia kupimwa afya yake, mambo yatakayowezesha mkataba kusainiwa.
WEST BROM WAMSAJILI BLANCO
West Bromwich Albion wamekamilisha usajili wa winga wa Argentina, Sebastian Blanco kutoka klabu ya Ukraine, Metalist Kharkiv.
Blanco (26) amesaini mkataba wa miaka miwili na Baggies, huku kukiwa na kipengele cha uwezekano wa kuongeza mkataba huo. Blanco amechezea timu ya taifa lake katika mechi mbili na ni mchezaji wa 11 kusajiliwa na klabu hiyo katikia majira haya ya kiangazi.
Wachezai wengine ambao West Brom wamewasajili ni pamoja na Joleon Lescott, Chris Baird, Sebastien Pocognoli, Andre Wisdom, Jason Davidson na Cristian Gamboa.
Kadhalika kuna viungo Craig Gardner na Silvestre Varela na washambuliaji Brown Ideye na Georgios Samaras .
CHELSEA SASA WANAMCHUKUA LOIC REMY
Jose Mourinho amebisha hodi Queen Park Rangers (QPR) kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji Loic Remy, baada ya kumtoa kwa mkopo wa miaka miwili mshambuliaji wake Mhispania asiye na ufanisi, Fernando Torres.
Kocha Harry Redknapp alikuwa ameshampanga Remy kwenye mechi ya leo dhidi ya Sunderland, lakini ilibidi aondoe jina lake baada ya Chelsea kutoa dau linalofikia kipengele cha mkataba wake, la pauni milioni 8.5.
Mchezaji huyo wa Timu ya Taifa ya Ufaransa mwenye umri wa miaka 27 alikuwa amemwambia Redknapp kwamba alikuwa tayari kucheza mechi ya leo lakini kocha huyo mkongwe akaamua kumuacha baada ya dau la Chelsea kuwekwa mezani saa sita kamili mchana.
“Inaelekea kana kwamba dili tayari limeshafanyika, kwa hiyo nikaamua kufanya mabadiliko,” akasema Redknapp juu ya mshambuliaji aliyekwenda Liverpool na kudaiwa kukwama kwenye vipimo vya afya na pia alitakiwa Arsenal ikashindikana kutokana na mshahara mkubwa anaotaka.
ARSENAL WATAMPATA SCHNEIDERLIN?
Arsenal wanajaribu kurudi Southampton kwa ajili ya kumsajili kiungo Morgan Schneiderlin waliyekataliwa awali, na sasa wanadaiwa kuwa tayari kutoa pauni milioni 27.
Kiangazi hiki Arsenal wamemsajili Calum Chambers (19) kutoka huko huko Southampton, na Liverpool waliwabomoa Saints kwa kuwanunua Adam Lalana, Rickie Lambert na beki Dejan Lovren huku Manchester United wakimchukua beki Luke Shaw.
Southampton walikuwa wamesema hawatakubali tena kuuza mchezaji wao mwingine, lakini Arsenal kufikia dau hilo inadaiwa kwamba wataweza kumchukua Schneiderlin (24) kabla ya dirisha kufungwa Jumatatu hii.
Schneiderlin amekuwa akitaka kuondoka hata kwa kulazimisha, lakini alionywa na kocha wake, Ronald Koeman, ambapo ilifika mahali kiungo huyo mkabaji alisema anajihisi hayupo tayari kucheza.
Schneiderlin aliyecheza vyema kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa Ufaransa, alikuwa anawindwa pia na wapinzani wa Arsenal wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur. Arsenal wanaweza kutoa mmoja wa wachezaji wake kwa Saints, kama vile Ryo Miyaichi, Serge Gnabry au Joel Campbell.
PELLEGRINI AWAONESHA MLANGO WACHEZAJI WANNE
Kocha Mkuu wa Manchester City, Manuel Pellegrini amewaambia walinzi Micah Richards na Matija Nastasic, pamoja na kiungo Scott Sinclair na mshambuliaji John Guidetti kwamba wanaweza kuondoka Etihad kabla ya siku ya mwisho ya dirisha la usajili, Jumatatu hii.
Hata hivyo, City hawajapokea ofa kubwa kwa ajili ya Alvaro Negredo licha ya Pellegrini kudai kwamba kuna klabu kdhaa za Hispania zinamtaka mshambuliaji wake huyo chaguo la nne.
Arsenal wameruhusiwa kuendelea na jitihada za kumsajili winga Alessio Cerci, baada ya Rais wa Torino, Urbano Cairo kuweka bayana kwamba mchezaji huyo anaweza kuuzwa kwa bei sahihi.
Kuna utata juu wanakokwenda washambuliaji wawili, Radamel Falcao wa AS Monaco na Edinson Cavani wa Paris Saint-Germain wanaotajwa kuwindwa na Real Madrid, Arsenal na Manchester City.