Man U wamtaka Mandzukic
Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal anataka kumsajili mpachika mabao wa Atletico Madrid, Mario Mandzukic, 29.
Mchezaji huyo ametimiza mwaka mmoja tu tangu alipohamia Hispania akitoka Bayern Munich kwa uhamisho wa pauni milioni 18.5.
Van Gaal bado ana hofu asipofanya biashara mapema atakuwa na safu butu ya ushambuliaji kama ilivyokuwa msimu uliomalizika, licha ya kuwa na akina Wayne Rooney, Robin van Persie na Radamel Falcao.
United pia wanafikiria kumwendea beki wa kulia wa Paris St-Germain, Gregory van der Wiel, 27, baada ya kumkosa yule wa Barcelona na Brazil, Dani Alves, 32, aliyeamua kubaki Nou Camp.
Wazo jingine kwa Van Gaal ni kumsajili beki wa kulia wa Southampton, Nathaniel Clyne, 24.
Barcelona wameamua kumbakisha kocha wao aliyewapa mataji matatu, Luis Enrique licha ya uvumi kwamba angeondollewa kwa kushindwa kuweka soka ya kuvutia kwa vijana wake.
Kocha mpya wa West Ham, Slaven Bilic anatarajiwa kupewa kitita cha usajili kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa kati wa Chelsea, Loic Remy, 28, na kiungo wa Barcelona, Alen Halilovic, 18.
Kipaumbele cha kwanza cha The Hammers, hata hivyo, ni kiungo wa Hispania anayekipiga Sampdoria, Pedro Obiang, 23 anayekadiriwa kugharimu pauni milioni 4.4.
Kocha mpya wa Derby County, Paul Clement aliyeajiriwa akitoka kuwa kocha msaidizi wa Real Madrid analenga kumsajili mchezaji wa Hull, Tom Ince, 23, anayekadiriwa kuwa na dau la pauni milioni sita.
Kiungo wa PSG, Yohan Cabaye, 29, atakubali kuhamia Crystal Palace iwapo bosi wake wa zamani waliyekuwa naye Newcastle, Alan Pardew atamwita.
Bosi wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino anataka kumsajili mshambuliaji wa kati wa Stuttgart, Timo Werner, 19, wakati huu anapotaka kufumua safu yake ya ushambuliaji.
Kocha wa Borrusia Dortmund aliyeachia ngazi, Jurgen Klopp amesema baada ya mapumziko ya muda atakuwa tayari kujiunga na klabu ya Ligi Kuu ya England.
Alikuwa akihusishwa na Liverpool, lakini sasa wamiliki wamesema kocha wao, Brendan Rodgers ataendelea na kazi yake msimu ujao, pengine wakimsubiri Klopp amalize mapumziko.
Mshambuliaji wa Manchester City, Alvaro Negredo, 29, anatarajiwa kutia mkataba wa kudumu kuchezea Valencia alikokuwa kwa mkopo.
Kiungo wa zamani wa Manchester United, Nicky Butt anatarajiwa kupewa nafasi ya kunoa akademia ya Man U baada ya Brian McClair kuondoka kwenda kufanya kazi Shirikisho la Soka la Uskochi.
Manchester City wanataka kuanzia mechi zao msimu ujao viwanja vya ugenini ili wapate fursa ya kuongeza viti 6,000 kwenye uwanja wao wa Etihad.