*Man United wamng’ang’ania Ronaldo
*Bilioni 36 kumpeleka Gomes Chelsea
*Arsene Wenger amtaka Marco Reus
Msimu wa usajili haujafika, lakini makocha, mawakala na wachezaji wanahaha kuona msimu ujao utakuwaje na nani atakuwa anachezea timu ipi.
Ndoto ya Manchester United kumrejesha mshambuliaji wao wa zamani, Cristiano Ronaldo zinaendelea, na safari hii wapo tayari kuwapa Real Madrid kitita cha pauni milioni 80.
Ronaldo (30) aling’ara akiwa United na aliuzwa Madrid enzi za Sir Alex Ferguson, lakini sasa Louis van Gaal analalamika kwamba hana mshambuliaji, licha ya kuwapo akina Wayne Rooney, Robin van Persie na Radamel Falcao.
Ronaldo amekuwa akisema kwamba anawaheshimu sana United na hata akiwafunga bao hawezi kushangilia, kutokana na alivyoshirikiana nao enzi zake.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amepanga kumchukua kiungo mshambuliaji wa Valencia, Andre Gomes (21).
Mourinho anaelezwa kwamba yupo tayari kutoa pauni milioni 36 ili kumnasa Mreno mwenzake huyo katika jitihada za kuimarisha timu inayoelekea kulegalega, hasa kwenye kiungo.
huku ikielezwa kwamba kuna vikwazo katika kutiliana mkataba mpya baina ya Arsenal na kiungo mshambuliaji Theo Walcott, Arsenal wanataka kumchukua kiungo wa Borussia Dortmund, Marco Reus.
Ilidaiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Walcott na Wenger walibwatukiana majuzi, lakini mchezaji huyo Mwingereza alijitokeza haraka kukanusha na kueleza kwamba hawajakutana kwa mazungumzo yoyote.
Reus (25) ni mchezaji mzuri ambaye amekuwa akihusishwa kuhamia London Kaskazini tangu msimu uliopita, lakini haijulikani kama Dortmud watamwachia.
Katika tukio jingine, Man United wanaelezwa kwamba wanajiandaa kuikataa ofa ya pauni milioni 12 kutoka Arsenal kwa ajili ya kumpata mlinzi wao, Chris Smalling.
Kocha Van Gaal atakuwa makini katika kuuza wachezaji, hasa kwa klabu pinzani, kutokana na yaliyomkuta baada ya kumuuza Danny Welbeck Arsenal, akarudi kuwajeruhi majuzi kwenye mechi ya Kombe la FA.
West Ham wameonesha kutokuwa na nia ya kumchukua moja kwa moja kiungo aliye kwa mkopo hapo kutoka Barcelona, Alex Song, kwa maelezo kwamba kiwango chake kimeshuka.
Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal alipata kusema anahitaji muda kurejea katika hali yake ya juu kisoka, na alitarajiwa awali kwamba angerejea Arsenal, lakini huko kuna chipukizi wengi kwenye kiungo.
Kadhalika West Ham wanataka kumchukua mshambuliaji wa Hull City, Abel Hernandez (24) lakini Newcastle nao wanadaiwa kumhitaji.
Manchester United wamepata pigo kwa beki wa pembeni waliyekuwa wanamtaka, Marquinhos (20), kusaini mkataba mpya na Paris St-Germain. Amejipiga kitanzi hapo hadi 2019.
Matumaini ya Liverpool kumsajili beki wa pembeni, Miralem Pjanic yameongezeka kutokana na habari kwamba raia huyo wa Bosnia anataka kuondoka kwenye klabu yake ya Roma.
Manchester City, kwa upande mwingine, wanafuatilia kwa karibu kiwango na mwenendo wa kiungo wa Lazio, Felipe Anderson (21) kwa ajili ya kuimatisha kikosi chao msimu ujao.
Tottenham Hotspur nao wanataka kujiimarisha kwenye ushambuliaji kwa kumsaka mpachika mabao wa Juventus na Hispania, Fernando Llorente.