Man U sahani moja na Gareth Bale
*Arsenal ni Deeney, Elneny au Ighalo
*Chelsea, City, Juve wanamtaka Isco
Manchester United wapo tayari kuvunja benki na kutoa pauni zaidi ya
milioni 75 kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji wa Real Madrid, Gareth
Bale, 26, baada ya klabu hiyo kumfukuza kazi Rafael Benitez.
United wanaona kuondoka kwa Benitez kunaweza kutoa mwanya wa kumpata
Bale, kwani alikuwa akichanua chini ya Mhispania huyo na pia
inatambulika kwamba Bale amechukizwa kuondoshwa kwa bosi Benitez. Hata
hivyo, mrithi wa Benitez, Zinedine Zidane amepata kusema kwamba Bale
hauzwi, lakini huenda United wakisisitiza watampata ‘mtu wao’ huyo.
Benitez alikuwa akijaribu kujenga kikosi chake kiongozwe na Bale
aliyenunuliwa kwa pauni milioni 85 kutoka Tottenham Hotspur. United
wanahitaji cheche ya kuwaamsha kwenye ushambuliaji na kipaumbele chao
kikuu ni raia huyo wa Wales.
United wanaamini kwamba Bale angependa kurudi kwenye soka ya England,
karibu na kwao. Atakuwa sasa akisubiri kujua mipango ya Zidane kwake.
Inatambulika, hata hivyo, kwamba Rais Florentino Perez ana mikakati ya
kuona Bale akiwa mrithi wa Ronaldo pindi akiondoka, ikizingatiwa
Ronaldo ana umri wa miaka 30 tayari. United watakuwa na kazi nzito
kumpata.
Pamoja na hayo, Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Man U, Ed Woodward
anatafuta kwa kila namna kitu cha kuwaliwaza na kuwafurahisha
washabiki wa Old Trafford, baada ya kuboronga mara kadhaa kwenye
usajili aliokwenda kusimamia.
Arsenal wanafikiria kutoa ofa kwa ajili ya kumpata mshambuliaji na
nahodha wa Watford, Troy Deeney, 27. Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger ni
shabiki wa mshambuliaji huyo mwenye nguvu kubwa, aliyefunga mabao sita
katika mechi 11.
Wenger anafahamu wazi kwamba Watford hawangependa kumuuza nahodha wao
wala mshambuliaji mwenzake, Odion Ighalo – aliyeingia Ligi Kuu ya
England kwa kishindo, akifunga mabao 14 katika mechi 20 lakini yumo
sokoni kupimana ubavu na wenzake ili atwae ubingwa wa Ligi Kuu ya
England (EPL) baada ya miaka 12.
Arsenal wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili na Mfaransa huyu
ameshasema kwamba atasajili walau wachezaji wawili. Kiungo wa Basel,
Mohamed Elneny (23) ni mmoja wao, na kuna tetesi kwamba leo ataingia
London kusaini mkataba kwa ada ya pauni milioni saba.
Kwingineko jijini London, West Ham wana nia ya kumuuza mshambuliaji
wao, Andy Carroll, 26, kwa pauni milioni 18, huku Sunderland na
Newcastle wakimtolea macho, ili ikiwezekana akawaokoe na jinamizi la kushuka
daraja.
Mshambuliaji wa Lokomotiv Moscow, Oumar Niasse, 25, anatarajia kuingia
EPL, Chelsea, Manchester United na Spurs wakitajwa kumhitaji Msenegali
huyo anayekadiriwa kwamba bei yake ni pauni milioni 15.
Chelsea, Manchester City na Juventus wanataka kumsajili kiungo Isco,
23, kutoka Real Madrid Januari hii. Manchester City wameambiwa kwamba
kiungo wa Schalke, Leroy Sane, 19, atawagharimu walau pauni milioni 40
wakisisitiza kumchukua.
Leicester wanapanga kumpa mkataba mpya mshambuliaji wa kimataifa wa
England, Jamie Vardy, 28, Januari hii na kumwongezea maradufu mshahara
wake.
Bournemouth wanamtaka mshambuliaji wa Chelsea, Patrick Bamford, 22,
baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo klabuni Crystal Palace mapema.
Kiungo Marouane Fellaini, 28, hatarajiwi kuondoka Manchester United
Januari hii, na hiyo ni kwa mujibu wa kocha Louis van Gaal.
Bosi wa Stoke, Mark Hughes amekataa kata kata kwamba mchezaji wake,
Bojan Krkic, 25, ataondoka wakati wa dirisha hili, akisema hakuna
kipengele kwenye mkataba wake kinachoruhusu kununuliwa mchezaji huyo.
Crystal Palace watatoa ofa ya pauni milioni 10 kwa ajili ya kumsajili
kiungo wa Swansea, Jonjo Shelvey, 23.
Arsenal wamemwita nyumbani kiungo wao, Serge Gnabry, 20, kutoka West
Bromwich na wanatarajia kumtoa kwa mkopo kwa klabu iliyo Ligi Daraja
la Kwanza – Championship.