De Gea anauzwa pauni milioni 50
*Hummels akataa kuhama, Reid awataka Arsenal
Manchester United wametafakari kufuatwa fuatwa kwa kipa wao aliye kwenye kiwango cha juu, David De Gea na kuamua kwamba wakitokea wenye pauni milioni 50 watamuuza.
Pamekuwa na tetesi kwamba Real Madrid, klabu wanaoongoza kwa kununua wachezaji kwa bei kubwa, wanamtaka De Gea (24) kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao, na sasa United wameweka bei hiyo kubwa ili kuwakatisha tamaa mabingwa hao wa Ulaya.
United wamedhamiria kumshawishi kipa huyo mzaliwa wa Madrid, Hispania kubaki, kwa kumpatia mshahara wa pauni 200,000 kwa wiki na mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya pauni milioni 52 hivi.
De Gea hana tatizo kubaki Manchester, isipokuwa anaweza kuvutwa na kishawishi cha kurejea nyumbani ambako angekuwa mrithi wa muda mrefu wa kipa, Iker Casillas, japokuwa aliingia Old Trafford akitokea Atletico Madrid.
United wanataka kuhakikisha anabaki, lakini akikataa mjadala wa mkataba mpya wanaweza kumuuza mapema, ili wanunue mwingine na pia kupata faida baada ya kuwa wamemnunua kwa pauni milioni 18.6 kwa mkataba wa miaka mitano mwaka 2011.
mlinzi wa kimataifa wa Ujerumani, Mats Hummels (26) amewakata maini Man United, Liverpool na Chelsea waliokuwa wakimtaka, akisema anapenda kubaki Borussia Dortmund.
Arsenal wamepata habari njema, kwani beki wa kimataifa wa New Zealand, Winston Reid (26) amewaambia West Ham kwamba hatasaini nao mkataba mpya kwa sababu anataka kujiunga na Arsenal.
Wolfsburg wanaoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani wapo tayari kutoa pauni milioni 23 kumsajili mshambuliaji Andre Schurrle ( 24) lakini Chelsea wanataka pauni milioni 30.
Kiungo wa Arsenal anayechipukia na aliyeitwa kutoka Charlton alikokuwa kwa mkopo Desemba hii, Francis Coquelin (23) anatarajiwa kupewa mkataba mpya Emirates baada ya kumfurahisha Arsene Wenger dimbani anakocheza vyema na Santi Cazorla.
Kiungo mkongwe wa Manchester United, Darren Fletcher (30) anahusishwa na kuhamia Valencia nchini Hispania kutokana na kuwa na wakati mgumu wa kupata namba chini ya kocha Louis van Gaal. Hata hivyo, West Ham wameonesha nia ya kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Uskochi.
Mshambuliaji matata wa Palermo anayedaiwa kuwa na bei mbaya, Paulo Dybala (21) hatahama katika dirisha hili dogo la usajili la Januari, klabu hiyo imedai, lakini huenda
West Bromwich Albion wapo tayari kumwongezea mshahara mshambuliajo wao Saido Beraniho (21) kwa zaidi ya maradufu ili abaki Hawthorns. Beraniho ana asili ya Burundi, alikwenda England akikimbia vita na ameshapewa uraia wa England na yupo timu ya taifa.
Kipa wa Club Brugge, Mathew Ryan (22) amethibitisha kwamba anataka kucheza ligi kuu ya England na tayari Liverpool wamesema wapo tayari kumchukua.
Mshambuliaji wa Tottenham aliyeshuka kiwango, Roberto Soldado (29) anatakiwa na klabu ya Ujerumani ya Bayer Leverkusen.
Manchester United wanaandaa dau la pauni milioni 15 kwa ajili ya kumrejesha England beki wa Barcelona, Gerard Pique (27). Hata hivyo, si rahisi Barca wamwachie kwa sababu hawaruhusiwi kusajili wachezaji hadi msimu ujao.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers amesema kwamba uhusiano wake na Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho umedorora.
Spurs wanaandaa ofa ya mkataba mpya na mnono kwa mshambuliaji wao aliye juu kwa kiwango na upachikaji mabao sasa, Harry Kane (21).