*Lukaku amekataa kutupwa West Ham
*Man United wamtaka Schweinsteiger
*Ramires, Cazorla, Cech, Reina watakiwa
Mpachika mabao wa Ubelgiji na Chelsea, Romelu Lukaku aliye kwa mkopo Everton amekataa kupelekwa tena West Ham United.
Lukaku aliyefunga mabao 15 akiwa na Everton msimu uliomalizika kabla ya hapo alikuwa West Bromwich Albion pia kwa mkopo.
Alikuwa na ndoto za kucheza Chelsea na kuwa kama Didier Drogba, lakini Kocha Jose Mourinho anaonekana kutompenda wala kumweka kwenye mipango yake.
Lukaku (21) amekataa uamuzi wa Mourinho kumpeleka West Ham na sasa anafikiria kuhamia Wolfsburg ya Ujerumani.
MAN UNITED NA SCHWEINSTEIGER
Baada ya kukataliwa kumsajili Toni Kroos wa Bayern Munich, Manchester United wanajaribu kumpata Mjerumani mwingine, kiungo Bastian Schweinsteiger (29).
Kroos alikataa kujiunga na United na klabu yake pia ilisema hauzwi. Amebakiza mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake.
United pia wamekwama kumsajili Thomas Muller na Arjen Robben wa klabu hiyo hiyo.
ARSENAL WAMFIKIRIA PEPE REINA
Arsenal wanadaiwa kuwa tayari kutoa pauni milioni tano ili wamsajili kipa wa Liverpool anayecheza kwa mkopo Napoli ya Italia, Joseph ‘Pepe’ Reina.
Reina (31) si chaguo la Kocha Brendan Rodgers wa Liverpool lakini mchezaji huyo anapenda kurudi Ligi Kuu ya England (EPL).
Arsenal wanatafuta kipa wa kuchukua nafasi ya pili iliyoachwa na Lukasz Fabianski aliyeondoka kama mchezai huru na kujiunga na Swansea.
Arsenal pia wanahangaika kuwatuliza washabiki wao baada ya kukataa kuteka fursa iliyokuwa wazi ya kumrejesha nahodha wao wa zamani, Cesc Fabregas ambaye sasa amejiunga na Chelsea.
The Gunners wanadaiwa kupanga kumsajili mlinzi wa Brazil, Bressan (21) anayechezea Gremio ya huko huko.
Arsene Wenger anadaiwa kuwa katika hatua za mwisho kumrejesha kundini mpachika mabao wa Real Sociedad, Carlos Vela (25) kwa pauni milioni 3.5 tu.
Liverpool wanachuana na Arsenal na Chelsea pia kumchukua mchezaji wa Schalke, Max Meyer (18) anayeuzwa kwa pauni milioni nane.
ALEX SONG RUKSA KUONDOKA BARCA
Baada ya kumuuza Cesc Fabregas, Barcelona wamemwambia kiungo wao, Alex Song (26) kwamba anaweza kuondoka Nou Camp.
Manchester United wanadaiwa kutaka kumsajili mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal.
MADRID WAKOMALIA USAJILI WA RAMIRES
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ameagiza hatua zichukuliwe haraka kuhakikisha wanamsajili kiungo wa Chelsea, Ramires (27).
Uamuzi huo umetolewa licha ya Chelsea kuonekana kutotaka kumuuza raia huyo wa Brazil anayeshiriki Kombe la Dunia.
Katika hatua nyingine, Paris Saint-Germain (PSG) wameweka bayana kwamba hawamuuzi mchezaji wao mwenye umri wa miaka 21, Marco Verratti, licha ya Real Madrid kumtaka.
PSG wameweka wazi kwamba wangependa kumsajili kipa wa Chelsea, Petr Cech ikiwa Blues wataamua kuachana naye.
ATLETICO WAMTAKA SANTI CAZORLA
Mabingwa wa Hispania wanafikiria kumsajili kiungo wa Arsenal, Santi Cazorla kwa pauni milioni 18.
Hata hivyo si rahisi Arsenal wamwachie Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 29, kwani tayari wameacha fursa ya kumsajili Fabregas kutokana na uwapo wa Cazorla na wenzake.
Kiungo mshambuliaji wa Chelsea na Ubelgiji,
Eden Hazard amesema hajapata ofa zozote kutoka kwa PSG licha ya ripoti zake kusambaa.