*Rooney anabaki Man U? Eto’o kupokewa Chelsea
*Arsenal na Angel Di Maria, Mesut Ozil, Cabaye
Habari nyingi zinachipukia wakati usajili wa wachezaji msimu wa kiangazi ukielekea ukingoni, ambapo inadhaniwa Wayne Rooney atabaki Manchester United na hata kuongeza mkataba.
Hata hivyo, habari zinasema kwamba Kocha David Moyes atamwalika Rooney kwa mazungumzo ya kusaini nyongeza ya mkataba baadaye iwapo ataonesha kujitoa kwa kila namna uwanjani kama alivyofanya dhidi ya Chelsea usiku wa Jumatatu.
“Wenzake Rooney wameona kubadilika kwake kitabia hasa baada ya kuingia akitoka benchi kwenye mechi dhidi ya Swansea na kisha kwenye mechi dhidi ya Chelsea…ameacha kulalamika na sasa tabasamu lake limerejea,” chanzo kimoja cha habari kinasema.
Hata hivyo, haitarajiwi kwamba ataongezwa mshahara kutoka pauni 250,000 anazopata sasa kwa wiki, bali ataachwa aendelee na mkataba wake kwanza.
CHELSEA WAMGEUKIA SAMUEL ETO’O
Chelsea waliokwishapeleka ofa mbili na kukataliwa na United kwamba Rooney hauzwi, sasa umemgeukia mchezaji wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o kwa ajili ya kuimarisha safu ya usmabuliaji.
Kulikuwa na tetesi kwamba Eto’o ameshaanza kuaga klabuni kwake Anzhi Makhachkala, ikidhaniwa makubaliano yanaweza kufikiwa kwa Chelsea kutoa pauni milioni 32 kama walivyofanya kwa Willian siku chache zilizopita wakiwapiga kumbo Tottenham Hotspur waliokuwa hatua za mwisho kumchukua.
GARETH BALE AKASIRISHWA NA SPURS
Winga nyota wa Tottenham Hotspurs, Gareth Bale amekasirishwa na hatua ya klabu yake kumkawiza kuhamia Real Madrid, na hakutokea mazoezini.
Inaaminika kwamba viongozi wa Spurs wanataka kuhakikisha kwanza wanasajili winga mwingine kabla ya kumwachia aondoke.
Hata hivyo, inadaiwa kwamba kuna klabu nyingine inayosaka saini ya Bale, hivyo kuwaweka roho juu Madrid wanaodhani tayari wamempata Bale kwa pauni milioni 85 hivi.
Spurs wanataka kumsajili Erik Lamela wa AS Roma lakini nao Roma wanasitisha mauzo hadi kwanza wampate mchezaji wa Fiorentina, Adem Ljajic.
Ilitarajiwa Spurs wangejitahidi kwa kadiri wanavyoweza kumzuia Bale kuondoka, lakini mchezaji mwenyewe anaonekana ameshapachoka na lazima ataondoka msimu huu, ndiyo maana amekacha mazoezi.
ARSENAL NA ANGEL DI MARIA
Arsenal wanaelekea kuwa kwenye nafasi nzuri ya kumpata winga Angel Di Maria kuliko wachezaji wengine Karim Benzema na Mesut Ozil wa Real Madrid.
Inasemekana kwamba iwapo Real Madrid watampata Bale watakuwa tayari kuwauza Ozil na Di Maria, lakini wakala wa Benzema amesema kwamba mchezaji huyo hataondoka Santiago Bernabeu na Madrid pia wanamtegemea katika kama mpachika mabao.
Arsenal wanasemekana kutenga kiasi cha pauni milioni 80 kwa ajili ya kuwanasa wachezaji hao watatu, ikishindikana wawili au mmoja na kupata wengine kutoka klabu tofauti.
Inaelezwa kwamba Arsenal wamemtengea Di Maria pauni milioni 24 na anaweza kucheza wingi ya kulia na kushoto.
Iwapo atajiunga na Arsenal, wengi watafikiria kwamba ni mbadala wa Lukas Podolski anayedaiwa kutaka kurudi kwao Ujerumani, licha ya kupachika mabao mawili mechi iliyopita dhidi ya Fulham. Anadaiwa kuumia na huenda akawa nje ya dimba kwa wiki mbili au tatu.
Wenger amesema atakataa ofa yoyote kutoka kwa klabu ya Schalke 04 ya Ujerumani inayodaiwa kumnyemelea, akisema anacheza vizuri kwa kujituma na kufunga mabao, hivyo hana sababu ya kumuuza.
Arsenal wamemweka katika orodha yao mshambuliaji wa Chelsea, Michu na mlinzi wa kati, Ashley Williams, lakini klabu hiyo ya Wales imekuwa ikikanusha kwamba watauzwa kwa Arsenal.
YOHAN CABAYE: NAENDA ARSENAL
Kiungo matata wa Newcastle United, Yohan Cabaye anadaiwa kuiambia klabu yake kwamba hataki tena kukaa hapo, na mawazo yake yote yako Arsenal.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alipeleka ofa ya kwanza ya pauni milioni 10. 2 iliyokataliwa, lakini kocha Allan Pardew alimwondosha kwenye kikosi chake kilichocheza na Manchester City.
Wakati Arsenal wakijiandaa kupeleka of ya pili, Pardew amedai kwamba uwezekano wa Mfaransa huyo kwenda Emirates ni nusu kwa nusu.
Kiungo huyo amewakasirisha Newcastle kwa kuanza mgomo na ameachwa nyumbani Newcastle wanaposafiri kwenda Morecambe kuchuana nao kwenye mechi ya Kombe la Ligi.
Hata hivyo, Pardew amemwambia Cabaye kwamba atatakiwa kucheza dhidi ya Fulham kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi, lakini mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa haelekei kucheza.
Mmiliki wa Newcastle, Mike Ashley anasema anatarajia Arsenal watoe pauni milioni 20 hivi ili wampate Cabaye, lakini Wenger amekaa kimya, hivyo kumwacha Cabaye katika sintofahamu.
Iwapo Arsenal watawapata Di Maria na Ozil, si rahisi kuongeza dau kwa Newcastle kumpata Cabaye
Newcastle wameanza tena mazungumzo kwa ajili ya kumsajili mpachika mabao wa Lyon, Bafetimbi Gomis, mazungumzo yaliyovunjika dakika za mwisho mwezi uliopita baada ya bei yake kuongezwa.