Menu
in , , ,

TETEMEKO MAN UNITED

Van Gaal kufumua timu na kuunda upya
*Aonya wiki ijayo kikosi kitakuwa tofauti
*Alonso aenda Bayern, usajili waendelea
*Torres aenda AC Milan

Harakati za usajili kwa msimu huu mpya zinaelekea ukingoni, kwani dirisha linafungwa Jumatatu hii na bado baadhi ya klabu hazijapata wachezaji wa kutosha kuwawezesha kufanya vyema.

Moja ya klabu hizo ni Manchester United, ambayo kocha wake, Louis van Gaal amewaambia wazi wachezaji wake baada ya chakula cha mchana kwamba huenda wiki ijayo kukawa na kundi jipya kabisa la wachezaji.

Amesema kwamba mambo aliyoachiwa na watangulizi wake, Sir Alex Ferguson aliyestaafu na David Moyes aliyefukuzwa ni magumu na yanahitaji kufanyiwa kazi kubwa licha ya kwamba tayari ametumia pauni milioni 130 kuwasajili Angel Di Maria, Ander Herrera, Luke Shaw na Marcos Rojo.

“Nimekuwa na mazungumzo na wachezaji baada ya mlo wa mchana, nikawaambia kwamba baada ya wikiendi hii nadhani tutakuwa na kundi jingine. Wachezaji wataondoka na wengine watakuja. Tusubiri tuone ni akina nani.

“Sasa nimeshatoa uamuzi juu ya wachezaji wote na baada ya hapo naweza kuchukua hatua nitakazo, lakini uzuri ni kwamba tunajua vyema ni akina nani tunaowataka. Wakati mwingine unaweza kubaki nao, lakini unaweza pia kuachana nao, inategemeana na klabu, lakini kwa wachezaji pia, maana wapo wanaotaka wenyewe kuja kuchezea United,” akasema Mdachi huyo kwa kujiamini.

United bado wanajaribu kupigana ili wawasajili William Carvalho wa Sporting Lisbon na Arturo Vidal wa Juventus, ambaye hata hivyo anadaiwa kusema anataka kubaki Italia. Mdachi Daley Blind pia anatakiwa Old Trafford.

Wakati hayo yakijiri, tayari Wilfried Zaha amepelekwa kwa mkopo Crystal Palace huku Aston Villa wakitaka kumsajili Tom Cleverley, kuwapunguzia mzigo United. Van Gaal amesema kwamba timu itaanza kushinda, akitabiri wataanzia ushindi Burnley Jumamosi hii katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL). Hull na Valencia pia wanamtaka Cleverly.

Tetesi zilizopo ni kwamba Arsenal walikuwa wakimuwania mshambuliaji wa Monaco, Radamel Falcao kwa mkopo wa pauni milioni 20 kwa mwaka, lakini Real Madrid wanadaiwa kuwa mbele yao kwa kufikia dili naye na timu yake.
 
Shinji Kagawa wa Manchester United alipanda ndege Ijumaa hii kwenda Ujerumani kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo vya afya kabla ya kuirudia klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund. Van Gaal amesema kwamba Mjapani huyo ameshindwa kumudu mfumo wake.

Arsenal wanatarajia kumsajili mlinzi wa Kigiriki wa Borussia Dortmund, Sokratis Papastathopoulos (26) lakini hawataki kutoa ada inayotakiwa ya pauni milioni 20. Danny Wellbeck naye anatarajiwa kuondoka Old Trafford, akipelekwa Tottenham Hotspur kwa mkopo.

Chelsea wanadaiwa kutoa ruhusa kwa mshambuliaji waliyemnunua kutoka Liverpool kwa pauni milioni 50, Fernando Torres kuzungumza na Inter Milan ya Italia kwa ajili ya kuhamia huko. Roma wamewakatalia Chelsea kuwapa mshambuliaji wao, Mattia Destro.

Manchester United wanamfukuzia kiungo nyota wa Stromsgodset mwenye umri wa miaka 15,  Martin Odegaard, aliyeweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kukipiga na Timu ya Taifa ya Norway; alicheza dhidi ya Emarati.

Valencia na Juventus wanapigana vikumbo kupata saini ya mshambuliaji wa Man U, Javier Hernandez ‘Chicharito’, ambapo Man U wanataka dau la pauni milioni 15.

Mpachika mabao wa QPR, Loic Remy ametupilia mbali uwezekano wa kurudi Newcastle alikokuwa kwa mkopo. Besiktas wanataka kumsajili Hatem Ben Arfa kutoka Newcastle. Kiungo wa zamani wa Arsenal, Alex Song anataka kurudi EPL, na huenda akajiunga na Liverpool au Spurs.

Wakati huo huo, kiungo wa Real Madrid, Xabi Alonso (32) amesajiliwa na Bayern Munich kwa dau lisilojulikana, baada ya kuwa amenunuliwa hapo Real Madrid kwa pauni milioni 30 kutoka Liverpool mwaka 2009.

Mhispania huyo alisaini mkataba wa miaka miwili Januari mwaka huu Santiago Bernabeu lakini sasa anataka kwenda kufanya kazi na Pep Guardiola. Ameichezea Timu ya Taifa ya Hispania mechi 114.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version