John Terry alitangazwa kujiunga na Aston Villa juzi Jumatatu baada ya safari ndefu akiwa na Chelsea. Mei 21 mwaka huu alicheza mchezo wake wa 717 na wa mwisho akiwa kwenye jezi ya Chelsea. Alimalizia kipindi chake cha zaidi ya miongo miwili alichowatumikia mabingwa hao wa EPL kwa mtindo wa kuvutia. Hiyo ni baada ya kuwemo kwenye kikosi kilichowasambaratisha Sunderland mabao 5-1.
La muhimu zaidi akashiriki kwenye sherehe za ubingwa wa EPL kwa mara ya tano kama nahodha wa Chelsea.
Hata hivyo safari hii Terry hakuwa na mchango mkubwa kwenye ubingwa wa Chelsea. Alipata nafasi ya kuanza kwenye michezo sita pekee ya EPL huku akitokea benchi kwenye michezo mingine mitatu. Hakuwa muhimu tena kwenye kikosi cha kwanza cha Chelsea. Katika umri wa miaka 36 asingepata nafasi ya uhakika kwenye kikosi chenye vijana kama David Luiz, Gary Cahill, Cesar Azpilicueta na wengine waliokuwa kwenye kiwango kile.
Hakuna pengo analoacha nahodha John Terry kwenye kikosi cha Antonio Conte kwa kiwango anachoondoka nacho kutokana na umri. David Luiz na wenzie wanaweza kuwa bora zaidi msimu ujao. Sio tu kwenye EPL, wanaweza kuwa tishio pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wanayorejea baada ya kukosekana kwenye msimu uliopita. Kama watakuwa kwenye kiwango kinachotarajiwa Terry hatakuwemo kwenye kumbukumbu za watu Chelsea wanaposhuka dimbani.
Ubora wa safu ya ulinzi ya Chelsea kwenye msimu uliopita ulikuwa na mchango mkubwa mno kwenye ubingwa waliotwaa. Walicheza michezo 16 pasipo kuruhusu bao. Walikuwa vinara kwenye kipengele hicho. Walinzi wao wawili walikuwemo kwenye kikosi bora cha mwaka cha EPL kinachofahamika kama ‘PFA Premier League Team of the Year’. Hao ni David Luiz na Gary Cahill. Kinga ya kiwango cha juu waliokuwa wakipata kutoka kwa N’Golo Kante iliwafanya kuwa bora zaidi.
Terry haachi pengo ndani ya Chelsea. Kizuri zaidi mbinu za mwalimu Antonio Conte zinaleta matumaini ya ziada. Mfumo wake maarufu wa 3-4-3 umezipelekea klabu za EPL matatizo makubwa. Mara nyingi wapinzani walilazimika kuiga mfumo huo walipokuna na Chelsea kwenye msimu uliopita. Hilo halikuizuia safu ya ulinzi ya Chelsea kuonesha makali yake na kuzipamba zaidi mbinu za Muitaliano Antonio Conte. Halikuwazuia Chelsea kuonesha muendelezo wa uimara na hatimaye kuibuka mabingwa.
Hata hivyo uimara wa David Luiz na wenzie, mbinu kali za ulinzi za Antonio Conte pamoja na mafanikio yoyote ya kiwango chochote watakayoweza kupata misimu kadhaa ijayo havitafuta alama ya John Terry ndani ya Chelsea. Ikiwa tunatarajia alama ya Terry inaweza kufutwa ndani ya Chelsea kutokana na umahiri wa walinzi waliopo sasa ama watakaokuja inatupasa tufikiri vizuri.
Terry ameacha alama ndani ya Chelsea. Unapoichezea zaidi ya michezo 700 moja kati ya klabu zenye mafanikio zaidi ndani ya EPL kwenye miongo miwili ya karibuni unakuwa umeacha alama kubwa mno isiyofutika. Unapodumu kwenye kikosi cha kwanza cha Chelsea kipindi kirefu kiasi hicho huwezi kusahaulika hata kama unahamia Aston Villa ambayo haishiriki kwenye Ligi Kuu ya England.
Ni alama kubwa mno isiyofutika kushikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kuliko mlinzi mwengine yeyote kwenye historia ya Ligi Kuu ya England. John Terry ndiye mwenye rekodi hiyo. Ni mlinzi mwenye mabao mengi zaidi kwenye historia ya EPL akiwa ameweka wavuni mbao 41. David Unsworth aliyewahi kuchezea timu kama Everton, West Ham na Aston Villa ndiye anayemfuatia akiwa na jumla ya mabao 38.
John Terry aliiongoza safu ya ulinzi ya Chelsea kuweka rekodi ya kuruhusu mabao machache zaidi kwenye msimu mmoja kwenye historia ya EPL. Akiiongoza safu ya ulinzi ya Chelsea kwenye msimu wa 2004/05 timu hiyo iliruhusu mabao 15 pekee msimu mzima na kuweka rekodi inayodumu mbaka sasa. Terry alicheza michezo 36 na kukosekana kwenye michezo miwili pekee kwenye msimu huo wa rekodi. Ndiye aliyetunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa EPL wa msimu huo.
Kuepuka kurefusha maneno ni vyema tusitaje rekodi zake za kuwemo kwenye vikosi bora vya EPL, UEFA na FIFA kwenye misimu mingi tofauti. Muda wa Terry ndani ya Chelsea ulishakwisha na sasa timu hiyo ipo chini ya uangalizi wa uhakika wa David Luiz na wenzie waliofanya kazi nzuri msimu uliopita. Ni sahihi kusema kuwa hakuna pengo linaloachwa na John Terry ndani ya Chelsea. Hata hivyo ameacha alama isiyofutika katika klabu hiyo na kwenye soka la England pia.