Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amewataka waombaji uongozi ambao hawaridhiki na uamuzi wa Kamati ya Rufani
ya Uchaguzi kutafuta haki yao kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo (Februari 16
mwaka huu) mchana, Rais Tenga amesema TFF ni moja ya taasisi ambazo zina
utaratibu unaoeleweka kwa wadau wake.
“Wote tunafahamu taratibu ambazo tumejiwekea juu ya wagombea wetu
wanachaguliwaje. TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu unaoeleweka.
Hii ni kuanzia wilayani. Kama kuna tatizo zipo njia za kufuata.
“Katika mchakato wa uchaguzi wengine wanafanikiwa, wengine wanaachwa.
Wameachwa kwa sababu zilizotolewa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi. Ambaye
haridhiki anafuata taratibu tulizojiwekea. Atafute haki yake kwa mujibu wa
taratibu,” amesema.
Rais Tenga amesisitiza kuwa kikatiba hana uwezo wa kuingilia uamuzi
unaofanywa na kamati ambazo ameziunda, kwani utawala bora ni kusimamia
kanuni ambapo wanaofanya uamuzi lazima waweke wazi sababu za uamuzi
waliofikia.
Amesema ambao hawakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya
TFF dhidi yao wana njia tatu za kufuata. Njia hizo ni kuiomba Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi ipitie uamuzi iliofanya (review), kuandika Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuomba liingilie au kwenda Mahakama ya
Usuluhishi ya Michezo (CAS).
“Hata ukiweka ngazi nne, mtu akiathirika ataona ameonewa tu. Kwa Katiba
yetu hapa (Kamati ya Rufani ya Uchaguzi) ndiyo mwisho. Hakuna chombo
kingine. Ukiwaomba FIFA waingilie, watakuja na tutawaeleza mchakato wote
ulivyokwenda. Tunapenda kuwahakikishia hawa (waathirika) kuwa kwa maslahi
ya mpira wa miguu tutasaidia katika hilo wapate haki,” amesema Rais Tenga
na kuongeza kuwa tayari waathirika wawili wa uamuzi wa Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi wameomba marejeo (review) kwenye kamati hiyo hiyo.
Amesema TFF imelazimika kuzungumzia suala hilo kwa sababu limekuwa
likizungumzwa kinazi zaidi wakati taratibu ziko wazi, hivyo kwa maslahi ya
mpira wa miguu ni vizuri taratibu zikafuatwa.
“Nawaomba washabiki wa mpira wa miguu, tumejenga chombo hiki (TFF) kwa muda
mrefu. Bado tunaomba watu watusaidie, kwa hiyo matusi hayawezi kubadili
kitu. Tunachowahakikishia ni kuwa, mtu anapoomba msaada tutampa kutafuta
haki yake.
“Hizi ni kamati huru, lazima ziheshimiwe. Ukianza kuziingilia utakuwa umeua
mpira wa miguu. Uongozi ni utumishi, tusionekane tunagombana. Huu si
ubunge, mbunge anachaguliwa anakwenda kulipwa mshahara. Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya TFF halipwi mshahara. Tusirudi kwenye matusi, tulishaondoka
huko,” amesema.
Kuhusu mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika kwa njia ya waraka, Rais Tenga
amesema yamefanyika kwa mujibu wa taratibu, na haikuwa siri. Maeneo
yaliyofanyiwa marekebisho ilikuwa ni lazima, kwani mengi yalikuwa ni
maagizo kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yamefuata taratibu na hakuna udanganyifu
katika hilo, kwani ridhaa ya kutumia waraka iliombwa, na Mkutano ni watu
ambao ndiyo wamepitisha mabadiliko hayo.
“Mkutano Mkuu ni watu, si kikao. Katika dunia ya leo mikutano inafanyika
kwa tele conference, si lazima watu wakutane sehemu moja,” amesema na
kuongeza kuwa mabadiliko hayo yalipitishwa kwa kura 70 dhidi ya 33
zilizokataa.
Kuhusu Kanuni kusainiwa kabla ya Katiba, Rais Tenga amesema tarehe ya
kuanza kutumika Katiba ni siku ridhaa ilipopatikana, na si siku mhuri wa
Msajili ulipopigwa. Mabadiliko ya Katiba yalipita Desemba 15 mwaka jana,
Kanuni zilisainiwa Januari 7 mwaka huu.