Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amemshukuru Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kwa kusajili
Katiba ya TFF toleo la 2013 kutokana na marekebisho yaliyofanywa na Mkutano
Mkuu Maalumu uliofanyika Julai 13 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Agosti 5 mwaka huu),
Rais Tenga ameishukuru Serikali, Msajili, Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Naibu wake Amos Makala na
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ushirikiano ambao wametoa kwa TFF
katika kufanikisha suala hilo.
Amesema baada ya kupokea usajili huo, kinachofuata ni Katibu Mkuu wa TFF
kumwandikia rasmi Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili aanzishe mchakato wa
uchaguzi wa viongozi wa TFF.
Kuhusu kauli ya Naibu Waziri Makala kuwa marekebisho hayo yasingeweza
kusajiliwa kwa sababu hayakufuata Katiba ya TFF, Rais Tenga amesema alikuwa
ana haki ya kusema hivyo kwa sababu hakuwepo kwenye Mkutano huo, na
kuongeza:
“Makala hakuwepo kwenye mkutano ndiyo maana alisema hivyo. Ana haki ya
kuuliza, nina hakika sasa atakuwa ameeleweshwa na ameelewa kwa sababu ni
msikivu. Kuhusu marekebisho hayo kupigiwa kura, hilo lisingewefanyika kwa
sababu hakukuwa na mjumbe aliyepinga marekebisho,” amesema.
Rais Tenga amesema marekebisho hayo yalipitishwa kwa kauli moja (unanimous)
hivyo hakukuwa na sababu ya kuanza kunyoosha mikono kupiga kura, kwa maana
hiyo mkutano ulipitisha marekebisho kwa asilimia 100 wakati Katiba ilikuwa
ikihitaji theluthi mbili tu.
“Hakukuwa na dispute (mabishano) kuhusu marekebisho, isipokuwa wajumbe
walitumia muda mwingi kuboresha kanuni na kutoa ushauri wa aina ya watu
ambao wangeingia kwenye kamati mbalimbali zikiwemo zile mpya za Maadili,”
amesema.
Ameongeza kuwa kwa vile wote walioingia kwenye Mkutano Mkuu huo Maalumu ni
watu wa mpira wa miguu wasingeweza kupinga marekebisho kwa vile yametokana
na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
“Labda itokee aliyeingia kwenye mkutano alikosea njia. Mtu yeyote wa mpira
wa miguu ni lazima afahamu kuwa maagizo ya FIFA ni lazima yatekelezwe, na
Katiba ya TFF inasema hivyo,” amesema Rais Tenga.
Pia Rais Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kushawishi watu wenye
sifa na uwezo wa kuongoza kujitokeza kwa wingi wakati Kamati ya Uchaguzi
itakapotangaza mchakato na tarehe ya uchaguzi huo.
*AZAM YAANZA ZIARA KWA KUIKABILI KAISER CHIEFS*
Makamu bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Azam wanaanza rasmi ziara ya
mechi za kirafiki nchini Afrika Kusini leo kwa kuikabili timu ya Kaiser
Chiefs ambayo inacheza Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL).