Kampuni ya bia Tanzania (TBL) imetishia kusitisha udhamini wake kwa klabu ya Yanga kufuatia uongozi wa timu hiyo kutangaza kujitoa katika mashindano ya Kombe la Tusker, ambayo yamepangwa kufanyika kuanzia Desemba 15 kwenye Uwanja wa Taifa wa zamani, jijini, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka kwa viongozi wa juu wa TBL, zinasema kuwa hatua ya Yanga kutangaza kuwa haitashiriki katika mashindano ya Tusker kimewakatisha tamaa na kusema kuwa maamuzi hayo yamekiuka makubaliano yaliyopo katika mkataba walioingia mapema mwaka huu.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa maamuzi ya Yanga kujitoa kimewafedhehesha wadhamini wa mashindano hayo, ambao pia ni wadhamini wa klabu hiyo na Simba kupitia bia yake ya Kilimanjaro katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Aliongeza kuwa katika mkataba ambao Yanga na Simba waliingia wenye thamani ya zaidi ya bilioni moja kwa mwaka, walikubali kuwa watashiriki mashindano yoyote yanayodhaminiwa na kampuni hiyo ambayo malengo yake ni kuinua kiwango cha soka hapa nchini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela alisema kuwa shirikisho hilo limeendelea kuwa na mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Yanga na kusema kuwa bado wameshikilia msimamo wao wa kujitoa.
Alisema kuwa endapo hawatabadili msimamo huo, sekretarieti itakutana mapema wiki hii ili kufanya maamuzi ya kutangaza timu nyingine itakayoziba nafasi hiyo.
Wakati huo huo, kuna habari kuwa viongozi wa Yanga wanatofautiana juu ya maamuzi ya kutoshiriki mashindano hayo kama ilivyotangazwa na mwenyekiti wao, Imani Madega.
Chanzo kingine kutoka Yanga kinasema kuwa hakuna kikao chochote cha Kamati ya Utendaji kilichokutana na kufikia maamuzi ya kujitoa.