CHAMA cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA), kimeanza kuwapatia mafunzo ya wiki moja makocha wa mchezo huo wa Zanzibar kwa ngazi ya kwanza.
Mafunzo hayo yaliyoanza juzi jioni, yanashirikisha makocha 42, ambao wanafundishwa mbinu mbalimbali zitakazowawezesha kuwafundisha wachezaji wanaoanzia ngazi za chini.
Mkufunzi wa mafunzo hayo Alfred Selengia kutoka kamati ya Maendeleo ya mchezo huo, amesema mafunzo hayo yanafanyika chini ya ufadhili wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Wavu (FIBV) kupitia mfuko wake wa maendeleo.
Alisema, FIVB kupitia mfuko wake huo, imetoa vifaa vya kuendesha mchezo huo ikiwemo mipira 80 na nyavu kumi vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 21.8.
Alifahamisha kuwa, mafunzo hayo ni mpango wa TAVA wa kuendeleza mchezo huo Tanzania ambapo kwa kuanzia wameanza na Zanzibar na baadae wataendelea katika mikoa ya Tanga, Mwanza, Morogoro, Manyara,
Kilimanjaro, Arusha na Dar es Salaam, na kila mkoa utapatiwa vifaa hivyo.
Aliongeza kuwa, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwanyanyua wachezaji wachanga pamoja na kupata wachezaji wengi wenye ujuzi sahihi katika mchezo huo.