Menu
in , , ,

Tatizo lilianza kwenye chozi la Salah

Tanzania Sports

Mohamed Salah thanks to Allah for every goal he scores for Liverpool.

Mwanzo mwa msimu ulianza na tabiri nyingi kuhusu maisha ya Zinedine Zidane pale Santiago Bernabeau. Wengi waliamini miguu yake haiwezi kudumu kukanyaga nyasi za Santiago Bernabeu.

Tulimpa mwezi wa kuwepo Santiago Bernabeu, tukampa wiki mbili, Mwisho wa siku tukampa mechi tatu lakini akili ya Perez haikuwa kama tulivyokuwa tunawaza na kutamani sisi kwenye mioyo yetu.

Alimvumilia , akamwamini na kuendelea kumpa nafasi Zinedine Zidane, nafasi ambayo ilikuwa na misukosuko mingi sana. La Liga ilikuwa ngumu kwake, hakuweza kushindana sehemu hii, ilifika hatua mpaka akili yake ikawa imeamini kwa sasa ni ngumu kwake yeye kuchukua La Liga.

Nguvu akazihamishia kwenye michuano ya usiku wa ulaya, alihakikisha kila usiku wa katikati ya juma ametengeneza chakula kitamu cha usiku.

Safari yake ilikuwa ngumu sana, hakukutana na wepesi kuanzia kwenye kundi alilokuwepo, kundi ambalo lilikuwa na timu zenye ushindani kama Borrusia Dortmund na Tottenham Hotspurs, alipigana na kufanikiwa kukimbia kuelekea walipokuwa kina Juventus, PSG na Bayern Munich.

Alionekana anaenda kukutana na miamba mizito, miamba ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kuchukua kombe hili, na kikubwa zaidi miamba ndiyo mabingwa wa ligi zao.

Hapa ndipo dalili za Real Madrid kuonekana wana nguvu kubwa ya kuchukua kombe hili zilianza kuonekana kwa sababu kabla ya jana alikuwa ameshakutana na ng’ombe na alikuwa amefanikiwa kumaliza kumtafuna ng’ombe mzima na akabakiza mkia peke yake.

Mkia pekee ndiyo uliobaki, mkia ambao ulionekana hauna nguvu na haukuwa umejiandaa kushindana kwenye fainali hii.

Dalili za kuonekana kuwa hawakuwa wamejiandaa kushindana na kuchukua kombe hili ilianza pale Mohamed Salah alipotolewa nje baada ya kupata majeraha.

Kila kitu kinachohusu Liverpool kilikosa kitu cha kufanya , nguvu ya mashabiki wa Liverpool ya kushabikia mwanzo hadi mwisho wa mchezo zilipungua na kuondoka ƙkabisa, uso wa Jurgen Klopp ulionesha hakuwa amejiandaa na tukio la kumkosa mchezaji nyota ndani ya kikosi.

Wachezaji ndani ya uwanja walitoka wote akabaki Saido Mane na vivuli vya wachezaji kumi. Hii yote ilionesha hawakuwa wamejiandaa kuishi bila Mohamed Salah.

Utaanzaje kupanga maisha bila ya mtu ambaye amekubeba msimu mzima?, mtu ambaye wakati yupo uwanjani aliwafanya wachezaji watano wa Real Madrid wasiwe na uhuru mkubwa wa kusogea eneo la mbele?

Marcelo ni moja ya chachu kubwa ya mashambulizi ya Real Madrid lakini wakati Mohamed Salah yupo hakuwa huru kusogea mbele mara kwa mara kushambulia, hofu ya kuwepo kwa mchezaji aina ya Mohamed Salah ilimfanya Marcelo awe na tahadhari kubwa sana.

Ulimuona Casemiro? Muda wake mwingi aliuwekeza nyuma na kushindwa kusogea mbele hali iliyowafanya Toni Kroos na Luka Modric wawe wanashuka chini kutafuta mipira, wakati huo Sergio Ramos akiwa nyuma muda mwingi mwa mchezo.

Mohamed Salah aliwafanya RealMadrid wacheze hivi, wachezaji watano nyota wakalazimishwa na Mohamed Salah kuwepo katika eneo lao.

Hapo ndipo uti wa mgongo wa Liverpool ulipokuwa, Liverpool ikaonekana hai ndani ya dakika20, walizidi kutuaminisha mechi itakuwa ngumu, nguvu zao za kupigana zilikuwa kubwa sana.

Nguvu ziliwaishia baada ya wao kuona chozi la Mohamed Salah, chozi ambalo liliwavunja moyo, hawakuwa na nguvu tena ya kupigana kama awali na kibaya zaidi hawakuonekana kama wana njia mbadala ya kuishi baada ya kuondokewa na mchezaji wao nyota.

Vivuli vilibaki ndani ya uwanja, vivuli ambavyo vilijikuta vinafanya makosa mengi binafsi hasa hasa golikipa, hakukuwepo na mtu kwenye benchi wa kubadili hali kama ilivyokuwa kwa Real Madrid.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version