Kocha wa Yanga Cedric Kaze tangu atue katika timu hiyo michezo minne ishachezwa na amepata alama 10 amepoteza pointi mbili tu.
Wakati Kaze anakuja viongozi wa Yanga pamoja na mashabiki wake walikuwa na imani naye sana katika nafasi hiyo.
Katika mechi nne amefanikiwa sana kwa kukusanya alama kumi ambazo si haba kwa uwiano huo.
Katika alama hizo mechi ya kwanza alicheza dhidi ya KMC ambayo ameshinda 2-1, mechi mbili za nje ya uwanja wao wa nyumbani Polisi Tanzania na Biashara United zote hizo amebutua goli 1-0.
Jumanne timu ya Wananchi imecheza na Gwambina FC ikaambulia alama moja kwa kutoa sare ya bila kufungana na kukamilisha michezo minne.
Katika michezo hiyo Yanga inaonekana bado upande wa mbele haujaanza makeke yake kwani imepata magoli 4 na kufungwa moja tu na kufukisha jumla ya magoli 11 yaliyofungwa msimu huu.
Yanga inaenda kucheza na Simba siku ya Jumamosi uwanja wa Mkapa ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja.
MIFUMO YA KAZE
Baada ya kuona michezo minne ikichezwa watafiti wa mambo wameshaona aina gani ya mpira anaoutaka uchezwe ndani ya timu hiyo, kocha huyu ana mifumo mikuu miwili hadi tulipofikia.
Kaze anaweza kuzuia lakini pia anaweza kushambulia kwa wakati mmoja.
Wakati anafanya hayo pia anamfumo wa Jose Mourinho aliutumia katika mechi na KMC baada ya kupata goli akaamua aweke watu wa kuzuia akitoa washambuliaji.
Katika mifumo hiyo itaweza kumlinda kwa vitu viwili , mosi anapopata goli akiona mambo hayaeleweki anajaribu kuweka watu ambao wanaweza kuzuia ili alinde goli lake na akafanikiwa.
Pili anaanza na mfumo wa kushambulia ili apate goli haraka baadae aje azuie aondoke na alama tatu.
Makocha wachache sana wa ligi kuu Tanzania Bara wanaweza kufanya kitu kama hiki kwa tulivyozoea kwa wengi wanakuwa na mfumo mmoja tu wa kuzuia kutokana na aina ya mchezo au kushambulia.
Kwa mifumo hiyo ambayo tumeanza kuiona tunaweza kutafasiri sasa Kaze amekuja na lengo la kupata alama huku akiingiza mifumo yake ndani ya timu ili ikae sawa na ashinde.
NI KWELI ATAWAVUSHA WANANCHI ?
Kiu ya mashabiki wa Yanga hivi sasa ni kuona timu yao ikipata mafanikio haijalishi ikiwa katika wakati gani kwani timu hiyo ilipotoka palikuwa pagumu sana.
Hivyo basi ni vyema kocha huyo ajue lengo mama la timu na atathimini kipi kifanyike ili afanikiwe zaidi.
Kwa namna anavyoenda nayo timu japo bado ule mpira ambao unahitajika haujapatikana mwanga unaonekana kabisa kuwa timu inaweza kubadilika siku za usoni.
KUBADILISHA KIKOSI
Katika mchezo ambao umeishia na sare ya 0-0 dhidi ya Gwambina FC alibadilisha wachezaji tisa walio katika kikosi cha kwanza.
Hii inaoneasha dhahiri kuwa anahitaji kuangalia kila kiwango cha mchezaji wake.
Anabadilisha sana upande wa ushambuliaji kwa ajiri ya kupata radha ya wafungaji.
Kutokana na mchezo unaofuata huenda pia ikawa njia rahisi ya kuwapunzisha ili wawe salama katika mchezo unaofuata dhidi ya Simba.
Hadi sasa timu hiyo imeruhusu magoli mawili tu ndio ptimu pekee ambayo imepoteza magoli machache zaidi.
Unadhani Kaze ataweza kupata ushindi dhidi ya Simba ilia pate jina zaidi ya lilivyo sasa hivi au atatoa boko.
Maswali mengi ya kujiuliza katika mchezo huo wa Simba na Yanga zote ziko vizuri.
Unampa alama ngapi Kaze hadi hapa tulipofikia ikiwa anaongoza ligi.
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kukusanya alama 23 kwa michezo 9 iliyocheza hadi sasa.
Azam FC iko nafasi ya pili ikiwa na alama 22 huku Simba ikiwa nafasi ya nne ya msimamo wa ligi.
Katika kuleta maendeleo ya timu yoyote ile duniani inatakiwa uvumilivu pamoja na umoja.