Mchezo wa soka ni biashara. Hii ni biashara inayotambuliwa vema na serikali za mataifa ya Afrika magharibi ndiyo maana yanakazania kuajiri wataalamu wenye vigezo vya hali ya juu.
Ukanda wa Afrika mashariki bado kasi ya maendeleo ya soka iko chini ingawaje kwenye mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ukanda huu ulishuhudia mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda na Burundi yakishiriki kwa mara kwanza pamoja.
Inawezekana ikatajwa kuwa hayo ni mafanikio lakini bado safari ndefu. Je ni mambo gani yanayaoweza kubadili hali ya soka nchini Tanzania? makala haya yanaangazia masuala muhimu..
Mosi, kuanzisha mfumo rasi wa kufundisha Shule za soka maarufu kama Academy. Kuwa na makocha wa Academy wenye leseni ya TFF. Na TFF kuzikagua academy rasmi ikiwemo kuzisajili na kuzitambua pamoja na kuzipatia fursa za hali na mali.
Mfano TFF inaweza kuitupia jicho Moro Kids ama Mwaisabula Academy kama mojawapo ya nyenzo za kuwezesha kuibuka vipaji vilivyofundishwa shuleni. Njia hii itasaidia kuwa na wachezaji wanaofundishika na wenye kupatiwa mafunzo ya soka wangali watoto.
Njia hii iyawezesha kuongeza kasi ya maendeleo ya makocha ambao watatambuliwa kupitia Academy. Njia hii itarasimisha Academy kuwa sehemu ambayo inatoa mafunzo ya soka darasani na viwanjani.
Makocha wenye leseni na sifa stahiki wanapofundisha vijana maana yake wanachangia kutengeneza makocha wa toleo lijalo ambao watakuwa wanaendeleza elimu waliyopatiwa. Njia hii itawezesha wachezaji kumudu majaribio na kwenda sambamba na dunia ya kileo ya kucheza soka kiufundi mbali ya kutegemea vipaji vyao.
Pili, kuandaa mashindano ya vijana kama Rollingstone ya Ally Mtumwa aliyokuwa yanafanyika jijini Arusha. Tunakumbuka mashindano ya Kombe la Taifa na Copa Cocacola yaliibua vipaji vingi ambavyo vilisambaa katika timu mbalimbali za Ligi Kuu, Daraja la kwanza na Pili.
Kwa mawazo yangu mashindano hayo yanaweza kutumiwa kuendeleza vijana kupitia Academy zinazosajiliwa. Mfano kila mkoa chama cha soka kinaweza kuendesha mashindano ya soka ngazi ya Academy na kupata washindi wa kushiriki taifa.
Mashindano ya Kombe la Taifa tangu enzi za Leodgar Tenga hayajafanyika tena, lakini yalikuwa na umuhimu saba. Kwahiyo kanuni zipige marufuku mchezaji wa Ligi Kuu, Daraja la Pili na Kwanza au Tatu asiye na umri chini ya miaka 18 kushiriki mashindano ya academy. Njia hii itawezesha kutegeneza vipaji vipya kwenye soka pamoja na kuunda timu za taifa zenye wachezaji waliopikwa kisasa.
Tatu, kuanzisha mashindano ya kutosha kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara. Katika soka la Tanzania mchezaji anacheza mechi chache mno; Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la soka nchini. Zaidi ya hapo anacheza michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo kwa msimu ni mara moja.
Katika hali ya kawaida utimamu wa miili ya wachezaji unakuwa wa chini mno. Hii ina maana ili wachezaji wabakie na utimamu wa miili pamoja na kuboresha viwango vyao ni lazima kuwe na mashindano mengine yanayokuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya soka. kwa mfano, Kombe la Mapinduzi haliwezi kuchukua nafasi ya Kombe la Muungano.
Kwamba inawezekana kabisa TFF na ZFA zikafanya majadiliano ya kufufua mashindano ya Kombe la Muungano kila msimu ambayo yanaweza kujumuisha timu 6 za Tanzania Bara na Zanzibar. Mashindano mengi ndiyo yanachochea uwingi wa uwekezaji yaani pesa.
Barani Ulaya wanashindana namna ya kuboresha ama kuanzisha mashindano ya vilabu vikubwa barani humo. vilabu viklubwa vinataka fedha zaidi kwa kuanzisha mashindano ya European Super League kupitia haki za Televisheni, wadhamini,motisha na zawadi za mashindano.
Hii ina maana ikiwa vilabu hivyo vitaanzisha Ligi hiyo maana yake kutakuwa na mechi nyingi zaidi na kuchochea mapato. Tanzania Bara kuna mashindano machache, mchezaji kucheza mechi chini ya 20 kwa msimu ni kudunisha uwezo wake.
Mashindano ya CECAFA yanasuasua, hayaelekei kuwa na mwendelezo. Mashindano ya Mto Nile yaliibuka na kuyeyuka kama barafu kwahiyo timu zinakuja zina mchi chache, wachezaji hawakui,mapato hayatoshi. Kwahiyo kuanzisha mashindano kama Muungano hata kwa kubadili muundo wake bado ni sehemu muhimu ya kuboresha soka Tanzania. Ukweli ni kwamba kutegemea mashindano mawili ya Ligi Kuu na Shirikisho hayawajengi wachezaji wetu.
Nne, serikali kuwekeza kiasi cha kutosha. Mojawapo ya mafanikio ya soka Afrika magharibi ni kwa serikali za nchi hizo kuwekeza kwa kiasi cha kutosha kupitia academy na taasisi nyingine zinazohusiana na kandanda. Wachezaji wao waliopata kucheza nje ya nchi wanajitokeza kuwekeza kwao na serikali inawasaidia kuhakikisha wanakamilisha ndoto zao.
Lengo la serikali ni kuwezesha uwekezaji wao kwa vile wanafahamu namna fedha za soka zilivyo tamu. Mabilioni ya fedha kwa kila mwaka yanayotokana na sekta ya michezo yanaingia nchi mbalimbali maeneo hayo. Serikali ya Tanzania haijatupia jicho michezo nab ado inaonekana kuichukulia kama sehemu ya burudani badala ya biashara.
Zama za kujisifia sera za ujamaa huku wananchi wanakuwa masikini zimepitwa na wakati. Wananchi wanaweza kutumia vipaji vyao na kuleta tija kwa taifa. Pale serikali itakapokubali utamu wa pesa za michezo ndipo tunaweza kufanya miujiza kwenye kandanda.
Mafanikio ya timu hayapatikani kwa kuunda kamati ambazo ni za ulaji tu pasipo kuleta mabadiliko. Ni aibu kuajiri kocha wa mpira wa kikapu, pete, riadha na mingine kutoka nje wakati ndani hakuna mipango ya maendeleo wala moundombinu. Tunawajiri ili waje kufanya nini sasa?
Nihitimishe makala haya kwa kusema, hayo ni machache kati ya mengi ambayo yanatakiwa kubadilishwa nchini ili kuimarisha sekta ya michezo nchini. Kila mchezo unao manufaa yake, lakini soka linaongoza kuliko mingine.