MATARAJIO ya Tanzania kutwaa Medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola imebaki kwa Wanariadha saba, Mabondia wawili na mwanamichezo mmoja wa michezo ya walemavu baada ya wachezaji watatu kutolewa jana katika mashindano hayo.
Wanamichezo waliotolewa jana ni bondia ambaye alifanya vizuri katika hatua ya kwanza ya pambano lake Nasser Mafuru na waogeleaji Hilal Hilal na Yahaya Khalid Rushaka ambao walishindwa kung’ara katika mashindano yao.
Mkuu wa Msafara wa Tanzania Juliana Yasoda, aliiambia Mwananchi jana kwa njia ya Simu kutoka New Delhi, kuwa bondia Nasser mafuru ambaye alionyesha ahueni kwa Tanzania jana alishindwa kufurukuta mbele ya bondia Jai Bhagwan wa India na kujikuta akipokea kipigo katika pambano lake la uzito wa Light Kg 60.
“Tayari bondia wetu amepigwa na waogeleaji Hilal na Rushaka wameshindwa kutamba ambapo Hilal ameshika nafasi ya nne na Rushaka amekuwa wa saba katika kundi lao mchezo huru wa kuogelea mita 50.
“Bondia Seleman Kidunda ambaye alifanya vizuri katika pambano lake la awali leo (jana) usiku atapanda ulingoni kupambana na Afaese Fata, endapo akifanya vema atakuwa amefuzu kuingia katika hatua ya robo fainali hapo kesho”, alisema Yasoda.
Wachezaji ambao hadi sasa bado hawajacheza kwa upande wa mabondia ni pamoja na Leonard Machichi anayezichapa katika uzani wa Light Kg 81 na Haruna Swaga anayezichapa katika uzani wa Heavy Kg 91.
Wengine ni Marco Joseph ambaye atakimbia mbio za mita 10,000 na 5,000, Frank Martin atakimbia mita 800, Barae Hera atakimbia Mita 1500 na 800 wakati Shamba Kitin, Samson Ramadhan na Patrick Nyangero watakimbia mbio za Marathon (km 42).
Kwa upande wa wanawake Restituta Joseph ataiwakilisha Tanzania katika mbio za Marathoni (KM 42) na mchezaji mmoja wa Paraolimpiki.