Kama ni katika dakika 90 za mchezo basi tungesema kuwa kuvunjika kwa safari ya timu ya Serengeti Boys kwenda Uingereza, basi kulitokea katika dakika za majeruhi. Zilikuwa ni dakika ambazo ukifungwa goli ujue siku hiyo hutakuwa na ujanja wa kufanya isipokuwa kukubali kushindwa.
Tukio la Kampuni ya Global Scouting Bureau GSB kufuta tiketi za vijana kwenda Uingereza, baada ya matangazo na majigambo makubwa, halitaweza kusahaulika katika historia ya michezo Tanzania.
Uwanagenzi wa safari na hamu ya kupokea misaada iliifanya TFF, Shirikisho la Soka la Tanzania, lisihoji vitu vingi, lisifuatilie vitu vingi…kiasi ambacho safari inaweza kuvunjwa bila ya mtu au tuseme kampuni iliyofanya hivyo kuweza kuwajibika kwa yaliotokea.
Ina maana TFF na GSB walikuwa wanataka kufanya biashara kubwa kama hiyo ya kutoa vijana kwenda Ulaya bila ya kuwa na maandishi kwa maana ya mkataba wa aina yoyote ile zaidi ya mali kauli, maana kama hiyo haikuwa mali kauli ilikuwa ni kitu gani basi.
GSB ikajigamba timu itakwenda Ulaya, ikajigamba kwa kununua tiketi, ikajigamba kwa timu itacheza na Chelsea na timu nyengine ya daraja la kwanza, itakuwa pia chini ya makocha wenye uzoefu na wenye sifa.
TFF ikameza yote hayo bila ya kufanya utafiti wa kina. Hasa kufika mpaka kukubali kuwapeleka vijana, bila ya kampuni kama hiyo kuweka rubuni kwa ajili ya afya na usalama wa vijana wanaoondoka.
Hilo lilikuwa ni kosa ambalo TFF wasithubutu kulirejea tena kabisa. Jee ingetokea vijana wanafika Uingereza, na kampuni ya GSB na wamiliki wake hawaonekani kabisa, kipi kingefanywa.
Kwni huyu Jack Pemba wa GBS ni nani? Si mtu mwenye maelezo ya kutosha wala haujulikani kabisa nchini Tanzania katika rubaa za mchezo wowote tu.
Jack Pemba alizuka ghafla mwanzoni mwa mwaka huu na kuja na maelezo ya kupamba juu ya mpango wake huo wa kuichukua timu ya Tanzania na kuipeleka Ulaya ambako ni tunu kwa vijana wetu wote.
Ukimtafuta Jack Pemba kwenye mtandao unamuona. Lakini katika mtandao huo wenye jina la kampuni yake huoni maelezo yoyote yanayomhusu yeye zaidi ya kutakiwa ulipe fedha kupata huduma?
Sio utani, hivyo ndivyo ambavyo Jack Pemba anavyotajwa. Hakuna yeye ni nani, amefanya nini katika mchezo au kwa maneno mengine anaielewa vipi soka mpaka aweze kuwa ni wakala wa mchezo huo…kiza kabisa.
Na kwa sababu hiyo ndio imekuwa ni rahisi kwa yeye kufanya aliyoyafanya kwa kuwa hapakuwa na makubaliano yanayofungana baina ya pande zinazohusika na kwa sababu kwa vyovyote iwavyo yeye hajulikani na mtu, nani atamkamata?
Labda TFF ilihadaika kwa kuona kuwa Jack Pemba anatokea Ulaya basi atakuwa ni msema kweli na muandalizi wa kweli wa mechi, wapi bwana, hata Ulaya matapeli wanakaa.
Sasa hilo limekuwa ni funzo kwa TFF na nchi nzima. Kila kitu kichunguzwe na kila kitu kiwe katika mikataba, kwa njia hiyo tutasalimika.
Kwa sababu kama hatukujifunza leo, tutakuwa katika wakati mbaya zaidi pale milango ya wachezaji wetu kupata fursa ya kucheza vilabu vya nje, na kukutana na matapeli wa kweli kweli wa soka ambao hata Shirikisho la Soka Duniani FIFA, linawahaha na kila siku kutoa tahadhari juu yao.