*JULIO, MKWABI, WASOTA
*WAMBURA AKATA RUFAA
MAAFISA kutoka katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) jana waliivamia Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba iliyokuwa inaendesha zoezi la usaili kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchukua nakala za vyeti na nyaraka nyingine zilizowasilishwa na wagombea uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi.
Hatua hiyo imetokana na mmoja wa wagombea kuwasilisha taarifa katika taasisi hiyo kwamba baadhi ya wanachama wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi wanadaiwa kuwasilisha vyeti ‘feki’ na wengine wametoa rushwa kwa kamati ili wapitishwe hali ya kuwa hawana sifa zilizotajwa kwenye kanuni na katiba ya Simba.
Maafisa hayo kutoka TAKUKURU waliwasili kwenye ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi na kuanza kuzungumza na kamati hiyo na baada ya wao kuondoka saa 6:45 mchana, wajumbe walikaa kwa zaidi ya dakika 20 wakijadiliana na kabla ya kuendelea na zoezi hilo la kuwasaili wagombea.
Habari zilizopatikana jijini zinaeleza kuwa kamati hiyo huenda ikajiuzulu endapo italazimishwa kufanya maamuzi kinyume na kanuni na katiba ya Simba.
Pia kila mjumbe aliyekuwa anatoka katika usaili huo alieleza kwamba wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali watakapohitajika kufanya hivyo.
“Uchaguzi huu umeingiliwa na vyombo vya serikali, kwa hiyo endapo utatafutwa na vyombo hivyo uwe tayari kutoa ushirikiano,” aliliambia gazeti hili mmoja wa wagombea.
JULIO, MKWABI WASOTA
Wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, beki na kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Swedy Mkwabi, ndiyo wagombea pekee waliohojiwa kwa muda mrefu na kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti, Damas Ndumbaro.
Julio aliingia kwenye ukumbi wa usaili saa 4:58 asubuhi na kutoka saa 5:24 wakati Mkwabi ambaye alichelewa kufika katika usaili huo alihojiwa kwa dakika 33.
Hata hivyo zoezi hilo liliendeshwa bila ya kufuata herufi za wagombea katika nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Andrew Tupa ndiyo alikuwa mgombea wa kwanza kuitwa kuanza kuhojiwa na kufuatiwa na Evans Aveva wote wanawania nafasi ya Urais wa klabu hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na kamati hiyo, kesho Ijumaa ndiyo siku ya kutangaza majina ya wagombea waliopita kwenye usaili huo kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
WAMBURA AKATA RUFAA
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Klabu ya Simba, Michael Wambura, leo Alhamisi amewasilisha rasmi rufaa katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akipinga kuondolewa katika mchakato wa uchaguzi.
Wambura aliwasilisha pingamizi hilo na kueleza kwa kifupi kwamba ndani lina hoja 14.
Kamati ya Uchaguzi ya Simba ilitangaza kumuengua Wambura ikieleza kwamba si mwanachama halali kufuatia kusimamishwa na uongozi uliokuwa madarakani mwaka 2010.