Menu
in

Taifa Stars yaigaragaza Amavubi 2-1 nyumbani kwao Rwanda Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo ana furaha tele baada timu yake kuwagaragaza Amavubi wa Rwanda, mjini Kigali.

MABAO ya wachezaji chipukizi, Jerry Tegete na Rashid Gumbo jana yalitosha kuipa Taifa Stars ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Amavubi ya Rwanda katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa jana mjini Kigali.

Katika mchezo huo wa kuvutia uliochezwa kwenye uwanja wa Nyamilambo wenye nyasi bandia, bao pekee la Rwanda iliyoko chini ya Mcroatia Branco Tucak lilifungwa na Jamal Mwisenzera.

Matokeo hayo yaliwasononesha mashabiki wa Rwanda ambao walitegemea kwamba timu yao ingeifunga Stars ili kujipa matumaini ya kuishinda Misri katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia, Septemba 5.

Timu ya Rwanda, maarufu kama Amavubi ikiwa bila wachezaji wake sita tegemeo wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, ilionekana kutawala zaidi kipindi cha kwanza ikiwatumia zaidi wachezaji sita wapya toka kwenye klabu zinazocheza ligi kuu nchi hiyo.

Katika mchezo huo, Amavubi ilikosa nafasi tatu muhimu kipindi cha kwanza ilipokuwa ikishambulia kama nyuki huku Stars ikionekana kuusoma mchezo na kuendana na makelele ya mashabiki wa Rwanda.

Stars ambayo ilimchezesha kipa wake majeruhi, Shaaban Dihile, ilianza kipindi cha pili kwa kasi ya ajabu ambapo Gumbo aliipatia bao la kwanza dakika 52, kabla ya Rwanda kusawazisha dakika ya 55 kupitia kwa Jamal.

Kutokana na mabadiliko ya wachezaji sita yaliyofanywa na kocha Marcio Maximo , Stars iliongeza bao la pili na la ushindi dakika 60 baada ya beki ya Rwanda kuchanganyana na kushindwa kuendana na kasi ya Stars.

“Rwanda walishindwa kuendana na kasi ya Tanzania leo kwa vile tulitumia zaidi wachezaji wapya kama sita hivi ambao hawajazoeana vizuri na wenzao, lakini wamejitahidi kipindi cha kwanza kipindi cha pili ikashindikana,”alisema Henry Muhire mwandishi wa habari za michezo wa Rwanda aliyezungumza na Mwananchi.

“Kutokuwepo kwa wachezaji walioko Ulaya kumeisumbua Rwanda na mashabiki wamekata tamaa, hawana matumaini kwamba timu yao itaweza kuishinda Misri kwenye mechi ya Kombe la Dunia,”aliongeza mwandishi huyo huku kocha Tucak akigoma kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo.

Kwa upande wake, kocha Maximo aliisifu timu yake na kudai kwamba, imecheza kama kundi na wachezaji chipukizi walikuwa na uchu mkubwa ndio maana wameshinda ugenini.

“Kipindi cha kwanza hatukucheza kwa nguvu, lakini kipindi cha pili vijana wangu waliingia kwa nguvu na vijana wamefanya kazi kubwa, wamecheza kama kundi, wamecheza vizuri,”alisema kocha huyo ambaye jana ilikuwa ni mechi yake ya kwanza ya kirafiki kushinda ugenini.

“Hii inatia matumaini kwamba timu yetu inazidi kupiga hatua na vijana wanajituma, “aliongeza Maximo ambaye mkataba wake unaisha Julai mwakani.

Kikosi cha kwanza cha Stars kilichoanza ni Dihile, Erasto Nyoni, Juma Jabu, Salum Sued, Kelvin Yondan, Shaaban Nditi,Nurdin Bakari, Mwinyi Kazimoto, John Boko,Mrisho Ngassa na Kigi Makassi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version