Menu
in

Taifa Stars ijiandae vyema kukutana na Ivory Coast yenye DROGBA!

Kocha mpya wa timu yetu ya taifa ya soka (Taifa Stars), Kim Poulsen ameteua kikosi kilichoingia kambini wiki iliyopita kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi dhidi ya Ivory Coast itakayochezwa Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan.

Uteuzi huo ambao sisi tunaamini kwamba ni bora kabisa, umelalamikiwa na baadhi ya mashabiki ambao hudhani kwamba soka linaendeshwa kisiasa.

Kwamba kwa kuwa kutoka Simba wamechaguliwa wachezaji 11 basi ni lazima wachaguliwe idadi kama hiyo kutoka Yanga. Pole yao , kwa sababu soka linazingatia viwango.

Katika msimu uliomalizika ambao Yanga walitumia muda mwingi kulumbana kuliko kupigania ubingwa, wachezaji wao wengi waliong’aa walikuwa ni wa kigeni. Ungetarajia vipi kocha Kim Poulsen awaite Stars?

Wachezaji wazawa wa Simba na wa Azam ndio waliong’aa. Isingekuwa haki kama kocha Kim asingewazawadia haki yao ya kucheza kwa bidii kwa kuwaita kwenye timu ya taifa.

Lakini tunaposema wachezaji wetu wameng’aa kwa viwango, ni vyema tusivimbe vichwa na kudhani kwamba ni viwango vya dunia. Ni kwa viwango vya hapa Tanzania , ambavyo vinaifanya nchi yetu kushika nafasi ya 145 katika viwango vya FIFA vya ubora wa soka duniani.

Tukitambua udhaifu wetu na kuacha kujidanganya kwamba tunaweza, tutajua namna ya kutatua matatizo yetu wakati tunapoenda kuivaa Ivory Coast ya Didier Drogba katika michuano hii mikubwa.

Kwenye Ligi ya Klabu Bingwa UIaya, Chelsea ya Drogba ilifahamu kwamba ni dhaifu mbele ya Barcelona . Ilijua kwamba haipaswi kujidai inajua kumiliki mpira na kupiga chenga nyingi mbele ya akina Lionel Messi, Iniesta na Xavi.

Walikubali kuwa hawawezi kushindana kupiga pasi dhidi ya Barca hivyo wakatafuta mbinu mbadala ya kukabiliana nao. ‘Walipaki basi’ langoni mwao. Wakawaacha Barcelona wapasiane, huku Drogba akajifanya ameumia kila dakika, jambo lililoongeza fadhaa kwa Barca kadri muda ulivyokuwa ukienda. Mashambulizi machache ya kustukiza yakawasambaratisha Barca, Chelsea ikasonga mbele.

Na juzi ikacheza kwa mbinu hizo hizo za kuwaruhusu wapinzani wawashambulie, wakae na mpira, wapige kona nyingi, lakini mwisho wa mechi wakaondoka na kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwenda nalo London kwa mara ya kwanza katika historia, kinyume na matarajio ya wengi.

Soka la siku hizi mbinu zinaleta matunda. Hatukatai kwamba bahati pia inahitajika, lakini hata ukiamua kucheza soka la wazi bado unahitaji bahati ili kusonga mbele.

Hivyo basi, tunapaswa kuanza kujiuliza maswali hapa kabla ya kwenda kuikabili Ivory Coast iliyojaa wachezaji nyota na wanaocheza katika ligi kubwa Ulaya kama Drogba na Salomon Kalou (Chelsea), Yaya Toure, Kolo Toure (Manchester City), Cheick Tiote (Newcastle), Gervinho (Arsenal), je sisi ni bora kuliko wao? Tunaweza kucheza pasi nyingi kuliko wao? Tunaweza kukaa na mpira kuliko wao?

Baada ya maswali hayo. Tunachopaswa kufanya ni kutafuta mbinu mbadala ya kuwakabili. Tunafahamu kwamba Drogba wakati akienda kuwakabili Barcelona , alikuwa akijua kwamba yeye ni mnyonge ndio maana akacheza kama alivyocheza.

Lakini akija hapa hatacheza vile, kwa sababu anajua sisi ndio wanyonge kwake.
Je tuingie uwanjani kushindana kucheza soka kama lao? Je wakikaa na mpira, wachezaji wetu wachanganyikiwe kwa hofu ya kupigwa nyingi?

Maswali yote haya yanapaswa kutafutiwa majibu sasa wakati wachezaji wetu wameingia kambini kujiandaa kucheza dhidi yao .

Baada ya Simba kutolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho, kocha wa klabu hiyo, Milovan Cirkovic, alikaririwa akisema ataibomoa safu yake ya ulinzi kufuatia udhaifu ulioruhusu wakafungwa magoli matatu ndani ya dakika 15 na kisha kutolewa kwa penalti na Al Ahly Shandy nchini Sudan .

Kama tunakiri kuwa sisi ni dhaifu, na kama tutafanyia kazi mapema onyo la kocha Milovan kwamba safu yake ya ulinzi ina mapungufu, huku tukitambua kuwa mabeki watano wa safu ya Milovan wameteuliwa katika kikosi cha Stars, tunapaswa tujipange. Tujipange tena sana, kabla ya kuwakabili akina Drogba.

Tunapaswa kutambua kwamba, kama mabeki wa Simba walionekana kusumbuliwa na mipira ya juu dhidi ya Al Ahly Shandy katika mechi waliyolala 3-0 nchini Sudan, tutakuwa na kazi ngumu ya kuwadhibiti wachezaji warefu wa Ivory Coast kama Yaya Toure, au Drogba, ambaye ni mzuri hewani, aliyefunga goli la kichwa lililoiamsha Chelsea hadi kutwaa ubingwa wa UEFA juzi usiku.

Tunaamini kwamba kocha Kim anatambua kuwa hatuwezi kujilinganisha na Ivory Coast. Basi tusijifanye tunajua sana dhidi yao. Mazoezi ya sasa Stars yalenge kuja kucheza kwa mbinu zaidi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version