KOCHA wa zamani wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Dk. Mshindo Msolla, amesema baada ya kushindwa kupata tiketi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazopigwa mwakani nchini Ghana, hakuna kupoteza muda, isipokuwa ni kujipanga upya kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Dk. Msolla, aliyekuwa akiinoa Stars pamoja na Ali Bushiri kabla ya kumpisha Mbrazil, Marcio Maximo, alisema ingawa inasikitisha kuona timu iliyopewa huduma zote ikishindwa, lakini hakuna kupoteza muda kwa hilo, bali ni kusonga mbele.
Alisema, katika historia ya Tanzania, hakuna timu ya taifa ambayo wachezaji wake na makocha wake wamepata matunzo yenye hadhi ya juu kama ilivyo sasa, lakini bado wakashindwa kufanya maandalizi mazuri na ya uhakika.
Dk. Msolla, msomi aliyebobea katika sayansi ya udongo, alisema maandalizi ya timu si kwenda nje ya nchi, bali ni jinsi gani timu husika inavyojiandaa kwa mashindano yaliyo mbele yake.
Alisema, kwa timu iliyo na wafadhili wa uhakika, haikupaswa kwenda Uswisi, Brazil au Denmark na kuishia kucheza mechi na timu ndogo za klabu, kwani ilipaswa kujipima na timu kubwa sawa na hadhi yake.
Dk. Msolla alisema, si kwamba, anakosoa, lakini analizungumzia suala hilo kitaalamu zaidi ili kuwa changamoto kwa siku za usoni, kwa sababu dhamira ya kila Mtanzania, ni kuona timu hiyo inapata mafanikio makubwa.
Alisema kama kulikuwa hakuna uhakika wa Stars kucheza na timu kubwa katika ziara ya Brazil, Uswisi na Denmark, kulikuwa hakuna sababu ya kupoteza muda na fedha nyingi kwenda na kucheza na timu ndogo ambazo si kipimo sahihi kwa Stars.
“Tumeteleza, hivyo tunatakiwa kujipanga upya kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, lakini dosari zilizojitokeza zinapaswa kuwa kama changamoto ya kutorudia makosa siku za usoni.
“Kama kuna timu ya taifa ambayo kwa hakika imepata matunzo mazuri, tena ya hali ya juu, ni Stars hii chini ya Maximo, hivyo hata kushindwa kwetu, hakutokanani na ukata, bali ni mipangiliao tu ya nini kifanyike katika kuiandaa timu vema.
“Hivi chini ya udhamini mnono kabisa wa Bia ya Serengeti na wengineo, kulikuwa na haja gani ya kupoteza mamilioni ya fedha kwenda Brazil, Denmark na Uswisi na kuishia kucheza na klabu? Stars ilipaswa kujipima na timu za taifa si klabu.
“Tanzania tulikuwa tukijiandaa na timu za Senegal, fedha zile zingetumika kuzialika au kuzifuata timu za taifa za Afrika kama Afrika Kusini, Ghana, Cameroon, Nigeria na nyinginezo nyingi za Afrika, kwa sababu fedha zilikuwepo.” Alisema Dk. Msolla.
Alisema, Stars chini ya makocha wazalendo, ilikuwa katika mazingira magumu yasiyoelezeka, hivyo kushindwa kufanya maandalizi ya maana kutokana na ukata, lakini kwa vile fedha ipo, Stars ilipaswa kujipima nguvu na timu za ‘saizi’ yake.
Dk. Msolla alisema, ziara za Brazil na Ulaya, hazikuwa na manufaa kwa wachezaji hao kiuchezaji, kwani waliishia kuona viwanja na mandhari za huko na kucheza na timu ndogo, ambazo hazikuwa na faida yoyote kiuchezaji.
Alisema, wadhamini wa timu hiyo wanapaswa kuliona hilo ili kosa hilo lisijirudie kwa sababu, wachezaji wa Stars walipoteza muda na fedha nyingi kwa ziara ambayo haikuwa na maana kiuchezaji, kwani haitofautiani na ziara ya kitalii.
“Stars kwenda Denmark na Uswisi na kuishia kucheza na klabu ndogondogo badala ya timu za taifa, ilikuwa ni kupoteza muda bure, kwani ilipaswa kujipima nguvu na timu za taifa hata za hapa Afrika kwa sababu uwezo wa fedha ulikuwepo,” alisema Dk. Msolla.
Alisema ni imani yake kuwa, wahusika wataliona hilo na kulifanyia kazi ili siku nyingine ziara za nje ziambatane na mechi za kirafiki na timu zinazoeleweka, si kuishia kujipima nguvu na timu za ‘mchangani’ kwa vile hazina msaada wa Stars.
Kuhusu maandalizi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, Dk. Msolla ameshauri nguvu zielekezwe kwenye timu za vijana wa chini ya miaka 17, 20 na 23 ili kupata timu ya wakubwa.
Alisema, wakati msukumo ukielekezwa kwa timu hizo, huku Mbrazil Maximo naye aendelee na programu yake ya timu ya wakubwa, akichomoa wachezaji kutoka timu za vijana watakaoonekana wamefikia kiwango.
Dk. Msolla ametoa pongezi kubwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kujali soka na michezo kwa ujumla na kusema, hali ikiendelea kama ilivyo sasa, Tanzania itapiga hatua kubwa kwa siku za usoni na kuomba fedha za wadhamini zitumike vema.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Stars kufungwa 1-0 na Msumbiji katika mechi ya mwisho ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Ghana, hivyo kupoteza matumaini kwa kumaliza ya tatu katika kundi lake la saba, kwa pointi nane.