Tanzania iliaga michuano ya kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika 2013 baada ya kutolewa na Msumbiji kwa penalti 7-6 kufuatia sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto hapa Msumbiji.
Wenyeji walitangulia kupata bao la mapema katika dakika ya 8 kupitia kwa Jeremies Saito aliyeunganisha krosi ya Helder Pelembe na mashabiki waliona kama tayari wamewang’oa wageni wao ndani ya dakika 90 wakati ubao wa dakika ya majeruhi uliponyanyuliwa.
Beki wa kati na Mshindi wa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka, Aggrey Morris, aliisawazishia timu ya taifa ya Tanzania katika dakika ya pili ya majeruhi na kufufua matumaini yao ya kusonga mbele lakini ndoto za Taifa Stars kucheza fainali za kwanza za Afrika tangu mwaka 1980 zilizimika katika hatua ya kupigiana matuta.
Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alipangua penalti mbili za kwanza za Msumbiji lakini Morris na Kelvin Yondani walikosa penalti zao kabla ya Mbwana Samata kukosa ya tisa iliyopanguliwa na kipa Joas na kuwapa fursa wenyeji kusonga mbele baada ya mchezaji wa ‘The Mambas’, Dominguez, kufunga yake.
Waliopata penalti kwa Stars, ni Amir Maftah, Shomari Kapombe, Shaaban Nditi, John Boko, Frank Domayo, Mrisho Ngasa.
Licha ya kufungwa goli la mapema Stars iliweza kutulia na kucheza soka la kujiamini katika kipindi chote cha kwanza, lakini washambuliaji wake walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Mshambuliaji Samata alikosa bao dakika 24 baada ya kupokea mpira uliomtoka beki wa Msumbiji, lakini alipiga shuti hafifu lililoishia mikononi mwa kipa wa Msumbiji.
Kiungo Frank Domayo alionyesha soka ya kiwango cha juu kwa kutoa pasi za uhakikika na kuwaunganisha vema Ulimwengu na Samata mwanzoni.
Hata hivyo, kocha Kim Poulsen alilazimika kufanya mabadiliko ya kikosi cha kipindi cha pili kwa kuwatoa Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto na Erasto Nyoni na kuwaingiza Haruna Moshi ‘Boban’, John Boko na Amri Maftah mabadiliko yaliyokuwa na faida kubwa kwa Stars.
Wenyeji huku wakishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wao walipoteza nafasi nyingi za kufunga na kuwafanya mashabiki waanze kuzomea kutaka mfungaji wa goli lao atolewe kwa kupoteza nafasi nyingi ambazo zingeweza kuimaliza Stars mapema, ambaombi ambayo yalifanyiwa kazi kwa mchezaji huyo kutolewa.
Aggrey alisawazishia Stars bao dakika ya 90+2 na kufanya mchezo huo kwenda kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2 kufuatia sare ya 1-1 iliyopatikana katika mechi yao ya awali iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Kikosi kilichoanza cha Stars kilikuwa; 1. Juma Kaseja, 20. Shomari Kapombe, 22. Erasto Nyoni, 6. Aggrey Morris, 5. Kevin Yondani, 19. Shaabani Nditi, 8. Mrisho Ngasa, 16. Frank Domayo, 11. Thomas Ulimwengu, 10. Mbwana Samata na 15. Mwinyi Kazimoto.
Wachezaji walioanzia benchi walikuwa; 18. Deogratias Munishi, 17. Amir Maftah, 13. Jonas Mkude, 3. Haruna Moshi, 12. Simon Msuva, 9. Christopher Edward, 14. John Bocco, 7. Ramadhan Singano na 21. Nurdin Bakari.