Menu
in , , ,

Taifa Stars fedheha

*Wapigwa tena Cosafa, watupwa nje
*Mabadiliko yanatakiwa kwa CHAN

Soka ya Tanzania imeanza safari ya kasi kwa kudidimia, baada ya Taifa Stars kuonesha vituko ugenini kwa kufungwa na timu ndogo.

Japokuwa kocha Mart Nooij alichagua sura ‘zile zile’ pengine kwa kigezo cha uzoefu kwenye michuano ya kimataifa, Stars waliambuliwa kipigo cha pili na kutupwa nje ya michuano hiyo waliyokuwa waalikwa.

Stars walioanza Jumatatu kwa kupigwa 1-0 kutoka kwa Swaziland, moja ya mataifa madogo Afrika, Jumatano waliongezewa dozi kama mgonjwa anayezidiwa homa, kwa kufungwa 2-0 na Madagascar.

Wachezaji wazuri na chipukizi waliong’ara kwenye Ligi Kuu ya Tanzania iliyomalizika hivi karibuni hawakupewa nafasi kwenye michuano hiyo, badala yake waliitwa walizoeleka pamoja na sura chache mpya.

Kocha wa zamani wa Stars, ambaye amekuwa mwajiriwa katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk Mshindo Msolla amenukuliwa akisema kiwango cha soka cha timu hiyo kinasikitisha na kuonesha kwamba hatua zinatakiwa kumhusisha pia kocha Nooij.

Ijumaa hii, Stars watashuka dimbani kucheza dhidi ya Lesotho katika mechi ya kukamilisha ratiba, ambapo hata wakishinda watajiandaa kurudi.

Maelezo ya kocha kabla ya kuondoka ni kwamba wachezaji hao na waliobaki kwa matatizo mbalimbali wataanza kambi kujiandaa na mechi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN), lakini wadau wanaona iwapo busara ingetumika timu ingevunjwa na kuundwa upya.

Wakati Tanzania ikiwa na idadi ya watu milioni 49.25, Swaziland walioanza kuchafua nyota ya Stars wana watu milioni 1,106,000 (milioni moja na laki moja na elfu sita).

Swaziland washika nafasi ya 176 katika ubora wa kiwango cha soka kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), hawajapata kufuzu kwa Kombe la Dunia wala CHAN na wanafundishwa na kocha Harris ‘Madze’ Bulunga, raia wa Swaziland.

Madagascar wanashika nafasi ya 150 kwa kiwango cha soka duniani na wanafundishwa na Franck Rajaonarisamba wa huko huko Madagascar. Hii ni nchi yenye watu 22,005,222, pungufu kabisa ya nusu ya Watanzania.

Tanzania kwa mujibu wa takwimu za Fifa, kwa sasa inashika nafasi ya 107. Ilipata kupanda hadi ya 65 Februari 1995 na kushuka hadi ya 175 Oktoba 2005.

Maneno ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ya Tanzania kuwa sawa na kichwa cha mwendawazimu ambacho kila mmoja hujaribu kunyoa, yanatakiwa sasa kujirudia rudia vichwani mwa viongozi wa soka wa ngazi mbalimbali.

Kwa namna ya pekee Shirikisho la Soka (TFF), benchi la ufundi la timu na wachezaji wenyewe, ili wabadili mwelekeo kabla hali haijawa mbaya. Katika makundi ya CHAN Tanzania wamepangwa na Nigeria, Misri na Chad. Kwa hali ilivyo, hata Chad wangeweza kuwafunga Tanzania. Ni wakati wa mabadiliko sasa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version