Wakati natazama mechi ya jana kati ya Zambia na Tanzania kichwani kwangu kulikuwa na swali moja tu ambalo lilikuwa linazunguka kichwani kwangu. Swali lenyewe lilikuwa, yuko wapi Jonas Mkude ?
Hili ndilo lilikuwa swali gumu kichwani kwangu. Kwanini nilimuwaza sana Jonas Mkude? Nilimuwaza kwa sababu ndani ya misimu mitatu iliyopita amefanikiwa kucheza mechi nyingi za kimataifa ngazi ya klabu.
Tukumbuke kwenye msimu wa mwaka 2018/2019 Simba walifanikiwa kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika huku Jonas Mkude akicheza kama kiungo wa kuzuia kwenye mechi takribani zote.
Kwa kifupi kwenye msimu huo ambao Simba walifanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Jonas Mkude alifanikiwa kucheza mechi zaidi ya kumi za ushindani wa kimataifa.
Msimu uliofuata wa ligi ya mabingwa barani Afrika yani msimu wa mwaka 2019/2020 Simba walitoka mapema lakini Jonas Mkude alifanikiwa kucheza mechi mbili za ushindani wa kimataifa.
Msimu huu wa mwaka 2020/2021, Simba wamefanikiwa kufika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Msimu huu Simba mpaka sasa hivi wamecheza mechi nne za ushindani wa kimataifa na Jonas Mkude amefanikiwa kucheza mechi tatu za ushindani wa kimataifa.
Kwa hiyo ndani ya misimu mitatu, Jonas Mkude amefanikiwa kucheza mechi zaidi ya kumi na mbili za kiwango cha kimataifa akiwa na klabu yake pekee ya Simba.
Hii ina maana gani? Jonas Mkude tayari ameshakuwa na uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa. Ile presha kubwa ya mechi za kimataifa ashaizoea. Namna ya kucheza mechi za ushindani wa kimataifa anajua.
Michuano ya CHAN ambayo sisi tunashiriki kwa mara ya pili baada ya kufanya hivo mwaka 2009 ni michuano ambayo ni ya kimataifa na inahitaji wachezaji ambao wanauzoefu sana na michuano hii ya kimataifa.
Siyo dhambi kutapeliwa vijana wapya kuzoea presha ya mechi za kimataifa, lakini hawa vijana wapya wangetumika kama wachezaji wa ziada dhidi ya wachezaji wazoefu.
Ni kitu kizuri kwa Baraka Majogoro kuonekana kama chaguo la pili mbele ya Jonas Mkude ambaye kwa kiasi kikubwa ana uzoefu mkubwa sana na mechi za kimataifa.
Kikosi cha jana kilikuwa na wachezaji wengi ambao hawakuwa na uzoefu na mechi za kimataifa kibaya zaidi ni kwenye michuano ya kimataifa.
Ili kuleta uwiano kulitakiwa kuwepo na wachezaji wenye uzoefu wa mechi za kimaitaifa ambao washazoea joto la mechi za kimataifa kwa kiasi kikubwa.