Menu
in

Sven wa Simba Ajiandae Kisaikolojia

Kadri siku zinazoenda utagundua kuwa Sven Vandenbroeck siku za kukalia kiti cha kocha mkuu wa timu ya Simba inazidi kuwa finyu kwa matokeo pamoja na mitafaruku na wachezaji.

Simba imeshapoteza michezo miwili mfululizo hadi sasa huku timu ikioneka kwenda katika njia mbaya.

Mtu wa kwanza kubeba gunia la misumari ni kocha mkuu wa timu hiyo Sven kisha dirisha la usajili likifika ndipo mchezaji naye atapata kile alichokipanda.

Michezo miwili ambayo Simba imepoteza ni pamoja na Tanzania Prisons na ule wa Ruvu Shooting yote hiyo kafa 1-0.

Uhalisia wa kikosi kipana unzidi kupotea kwakuwa vipigo vyote viwili vilipatikana baada ya kukosekana baadhi ya wachezaji wao nyota.

Hali hii inamrudia kocha Sven kwakuwa hafanyi ‘Rotation’ ya wachezaji wakati wote wakiwa wazima hawana majeraha.

Kocha atakuwa ana msala mkubwa kama ataendelea kupoteza michezo ya ligi mara kwa mara huku mbele ana michuano ya klabu bingwa Afrika.

KUTOELEWANA NA WACHEZAJI

Hali hii ilianza kwa Meddie Kagere japo waliyafich hawakutaka kusema lakini inaeleweka dhahiri kuwa Sven na Kagere hawana maelewano mazuri na sasa angalau mambo yamekaa sawa.

Tanzania Sports
Sven…

Lakini pia kuna wengine ambao nao haelewani nao, hii huwa inatokea ndani ya timu wakati mwingine ila kocha mkuu ndio baba kwa wachezaji hivyo anatakiwa afanye mambo ya kiutuuzima.

MVURUGANO WA KITAMBAA CHA UNAHODHA

Katika mchezo waliopoteza dhidi ya Ruvu Shooting kitambaa alivaa Jonas Mkude ambaye zamani alikivaa pia.

Hapa kulizuka maswali mengi sana, wengi wakihoji  kwanini apewe Mkude wakati nahodha msaidizi alikuwepo uwanjani ambaye ni Mohamed Hussein.

Watu waliendelea kuhoji kwanini  alipoingia John Bocco Mkude hakuvua kitambaa.

Huko tunakoiga huwa nahodha akikaa nje anapoingia huwa anapewa jukumu lake kama kawaida katika mchezo ule Mkude alisahau au alipokea maelekezo ya kocha.

Baada ya mchezo wazee wa kuunganisha matukio wanasema kuwa Sven hawataki tena John Bocco na Mohamed Hussein kuwa viongozi wa wachezaji kwa wanachodai kuwa kuliibuka mtafuruku mkubwa baina yao.

Lakini kitambaa kitu cha kawaida kwa mujibu wa wachambuzi wa Kibongo hawaoni tatizo kwa kilichoendelea siku ile.

Kauli ya kocha Sven aliposema kuwa kuna mengine hatuwezi kuyaongelea hapa yanahusu ndani anamaana gani?

Waza haraka haraka unamuona wapi bwana Sven hadi kufikia X-mass kama bado tuko hai tutakula sote ?

Kocha huyo alitaka kuondoshwa tangu msimu uliopita lakini alipata watu wakubwa walimtetea sana ila sasa kila mmoja amechoka na lugha inayozungunzwa sasa ni ile ya kingereza kuwa ‘Coaches are hired to be fired’.

Kumvumilia kocha yataka moyo sana hasa anapokuwa katika wakati wa majanga kama haya.

CAF SASA

Simba inaelekea katika michuano  migumu ya CAF unadhani kwa namna hali inavyoendele hapa ndani unaipa alama ngapi kutoboa huko ?

Tumeona namna timu zinavyocheza kwa nguvu Zote huku zikijitoa kwa ajiri ya timu zao kweli zile ‘Khamsa’ za AS Vita na Al Ahly zitarejea.

Hapa sasa ndipo unakumbuka kwanini Wenge B.C.B.G waligombana na kutengeneza kundi lingine kwa wale wenye nguvu, Werrason Ngiama Makanda kaanzisha lake huku JB Mpiana naye ameanzisha lake, basi kazi iliishia hapo.

Mr Nice miaka ya 2000 aliwahi kuimba wimbo unaitwa ‘Kikulacho’ kwa uhalisia ule wimbo tuliimbaga watoto ila yeye amechukua fursa na kuimba katika mahadhi ya ‘TAKEU’ na alipiga pesa.

Nawaomba mashabiki na viongozi wa Simba wakaupitie wimbo huu na kuyazingatia mashairi ya MR Nice, wausikilize wote hadi mwisho, nafikiri katika vikao wautumie.

MASHABIKI

Wengi wanasema kuwa timu haichezi vizuri bado lawama zinaelekezwa kwa kocha imefika mahali hadi mshabiki mmoja ameweka wazi kuwa sasa lile jina la ‘Utopolo’ waliowap watani wao Yanga sasa limerudi kwao.

Yasini Matope wa Kinondoni Moscow yeye ameweka wazi kuwa kocha anatakiwa awaachie timu hapa ilipo inatosha.

“Kocha alipotufikisha inatosha sasa tutafute mtu mwingine wa kutusaidia kutuvusha hapa,” alisema.

Ayoub Chiba naye ameungana na wengine akisema kuwa kocha ameshindwa kuitengeneza timu inapokuwa na matatizo hata msimu uliopita ilikuwa hivi.

“Kocha ameshindwa kuitengeneza timu msimu uliopita tulifungwa baada ya kubadilisha wachezaji wasiopata nafasi ya kikosi cha kwanza, hawezi kuendelea na Simba,” alisema.

Wewe una maoni gani ? au una povu unataka kulitoa juu ya yanayoendelea, basi tuwekee katika mitandao yetu ya kijamii.

Written by Amini Nyaungo

For the past 9 years, I have been working as the Sports news Journalist in online and print media this experience help me to be utilized by the different sports events where I have got chances to the media as the football pundit in different media in Tanzania.

Leave a Reply

Exit mobile version