Nigeria wametangaza kikosi cha kukabiliana na Tanzania kwenye mechi ya mkondo wa kwanza kufuzu kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017.
Kocha mpya wa Super Eagles, Sunday Oliseh amekitaja kikosi ambacho si kipya sana, bali kinachobeba wengi waliokuwa wameitwa na mtangulizi wake, Stephen Keshi.
Walioitwa wapya ni pamoja na mshambuliaji Emmanuel Emenike anayecheza Mashariki ya Kati; mshambuliaji wa Werder Bremen ya Ujerumani, Anthony Ujah na viungo Lukman Haruna na Obiora Nwankwo. Hata hivyo, kiungo wa Chelsea, John Mikel Obi na winga Victor Moses wameachwa.
Nwanko anayecheza Académica de Coimbra aliwekwa pembeni tangu taifa hilo lilipotwaa taji la mashindano haya 2013, wakati Haruna wa Anzhi Makhachkala hajapata kuchezea taifa lake tangu fainali za Kombe la Dunia 2010.
Mshambuliaji wa timu iliyopanda daraja msimu huu nchini England, Watford, Odion Ighalo ameitwa kikosini. Nigeria walianza mechi hizi kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Chad Juni mwaka huu na mapema mwezi ujao watakabiliana na Stars jijini Dar es Salaam.
Kipa na nahodha, Vincent Enyeama ataongoza wachezaji 18 wa kigeni waliopangwa na Oliseh kuwabomoa Stars na wanatarajiwa wawe Abuja walau Agosti 18 kuungana na wale wanaopiga soka ndani ya Nigeria.
Stars wananolewa na kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa katika mkataba wa mpito baada ya kocha wa awali kuondoshwa. Nigeria nao walimwondosha Keshi kwenye kazi hiyo hivi karibuni.
Oliseh alisema angechagua wachezaji wanaocheza mara kwa mara kwenye klabu zao, na pengine ndiyo maana Obi na Moses wameachwa kwani hawapati nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya England.
Msemaji wa Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF), Ademola Olajire amesema Oliseh ametekeleza vyema ahadi yake.
Akasema kwamba hii ni fursa mpya kwa wachezaji wa zamani walioitwa tena pamoja na wale waliokuwamo kuonesha kiwango chao na kulibeba taifa hilo kubwa barani Afrika.
Orodha kamili ya wachezaji na klabu zao kwenye mabano ni makipa Enyeama (Lille, Ufaransa) na Carl Ikeme (Wolverhampton Wanderers, England).
Walinzi ni Leon Balogun (FSV Mainz 05, Ujerumani); Kingsley Madu (AS Trencin, Slovakia); Godfrey Oboabona (Rizespor, Uturuki);
William Troost Ekong (FK Haugesund, Norway) na Kenneth Omeruo (Kasimpasa, Uturuki)
Viungo watakaobeba jahazi hi Joel Obi (Torina FC, Italia); Izunna Ernest Uzochukwu (FC Amkar Perm, Urusi); Obiora Nwankwo (Coimbra FC, Ureno); Lukman Haruna (Anzhi, Urusi) na Rabiu Ibrahim (AS Trencin, Slovakia)
Super Eagles itakuwa na washambuliaji Ahmed Musa (CSKA Moscow, Urusi); Emem Eduok (Esperance, Tunisia); Emmanuel Emenike (Al Ain, Emarati); Anthony Ujah (Werder Bremen, Ujerumani); Sylvester Igboun (FC UFA, Urusi) na Moses Simon (KAA Gent, Ubelgiji).