*Wakili wake akimbilia Cas
Barcelona wamekamilisha usajili wa Luis Suarez kutoka Liverpool baada ya kulipa ada ya pauni milioni 75.
Hata hivyo, utata uliopo sasa ni iwapo wataruhusiwa kumtambulisha Suarez Camp Nou kwa washabiki wao kama walivyofanya kwa wachezaji wengine, kama Neymar, Cesc Fabregas , Zlatan Ibrahimovic na David Villa.
Hiyo inatokana na uamuzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kumfungia mshambuliaji huyo wa Uruguay kujihusisha na shughuli zote za soka kwa miezi minne baada ya kumng’ata mchezaji wa Timu ya Taifa ya Italia, Giorgio Chiellini.
Baadhi ya wajuzi wa sheria wanasema kutambulishwa kwake uwanjani ambapo maelfu ya washabiki huhudhuria au kufanya mkutano na wanahabari kutakuwa kinyume na kufungiwa kwake na kunaweza kuongeza adhabu.
Hata hivyo, mwanasheria wake, Alejandro Balbi amesema kwamba wanakata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (Cas) na matarajio yake ni kwamba adhabu hiyo aliyodai ni ya kizamani, kikatili na kifashisti itafutwa.
Wanaweza pia kuwauliza Fifa iwapo wanaweza kumtambulisha mchezaji wao huyo mpya na aghali atakayeungana na akina Neymar, Messi na wengineo Oktoba mwaka huu kwenye La Liga.
Suarez (27) alikosa mechi kadhaa za mwisho za Ligi Kuu England msimu wa 2012/13 na za mwanzo za 2013/14 kwani alikuwa akitumikia adhabu ya Chama cha Soka cha England kwa kumng’ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic wakati akiwa Liverpool.
Mbali ya kupigwa marufuku kucheza miezi mine, Suarez pia amezuiwa kucheza mechi tisa za kimataifa, kulipa faini ya dola 66,000 na rufaa hiyo ikikatwa kweli inaweza kuwa jaribio kubwa la kutikisa au kupunguza nguvu za Fifa iliyokataa rufaa ya mchezaji huyo wiki hii.
Suarez alikana kumng’ata Chiellini akisema waligongana meno yakamuumiza lakini kwamba hata yeye aliumia. Baadaye alimwomba radhi Mtaliano huyo. Baada ya kumng’ata Ivanovic aliomba pia radhi na kuahidi kutorudia tena tabia hiyo mbovu.