*Ni kwa kumng’ata bega beki Mtaliano
*Mara ya tatu anakula nyama za watu
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeanzisha mchakato wa uchunguzi wa kinidhamu dhidi ya mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez anayedaiwa kumng’ata mchezaji wa Italia, Giorgio Chiellini.
Mchezaji huyo bora wa mwaka wa England, anadaiwa kumng’ata Chiellini Jumanne hii katika mechi ambayo ilimalizika kwa Uruguay kushinda 1-0 na kuwatoa Italia kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Fifa wamewapa Suarez na Chama cha Soka (FA) cha Uruguay hadi saa moja jioni Jumatano hii kujieleza na kuwasilisha utetezi wowote wanaoona unafaa.
Hii ni mara ya tatu Suarez anadaiwa kufanya kitendo hicho na kuna uwezekano wa kufungiwa kwa muda mrefu kucheza licha ya mwamuzi wa mechi kutomwadhibu kwa vile hakuona tukio hilo.
Fifa wamesema kwamba ikithibitika Suarez atakuwa amekiuka kanuni za nidhamu za shirikisho hilo kwa kufanya kitendo cha kumshambulia mchezaji na pia kukosa uungwana mchezoni.
Suarez na Chiellini walikabiliana kwenye eneo la penati la Uruguay dakika 10 kabla ya mechi kumalizika, ambapo Chiellini alivuta jezi yake kumwonesha mwamuzi alama za meno ya Suarez baada ya kumng’ata begani.
Kadhalika Suarez alikaa chini huku akiwa ameshikilia meno yake baada ya kituko hicho kinachojirudia kwa mara ya pili katika karibu mwaka mmoja.
Wataliano walikuwa bado wakilalamikia kitendo hicho wakati Diego Godin alipofunga bao pekee dakika moja tu baada ya ung’ataji kufanyika.
Chiellini alieleza mshangao wake kwa Suarez kutotolewa nje wakati alionesha ushahidi wa wazi wa jinsi alivyomng’ata.
Suarez mwenyewe anapinga madai hayo akisema ni kawaida tetesi kama hizo kutolewa uwanjani ambapo anadai Chiellini alimpiga kwa bega lake kwenye meno.
Kocha wa Uruguay, Oscar Tabarez alidai kwamba hakuona tukio hilo na kudai mshambuliaji huyo wa Liverpool aliyeongoza kwa mabao msimu wa ligi kuu England uliomalizika anaonewa tu.
Suarez alipigwa marufuku kucheza mechi 10 England baada ya kumng’ata Branislav Ivanovic mwishoni mwa msimu wa ligi wa 2012/2013 na mwaka 2010 aliadhibiwa kukosa mechi saba kwa kumng’ata Othman Bakkal wa PSV Eindhoven, enzi hizo Suarez akichezea Ajax Amsterdam.
Alikosa mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi miaka minne iliyopita baada ya kupewa kadi nyekundu alipodaka mpira uliokuwa unaelekea langoni mwake na kuwanyima Ghana nafasi ya kuingia robo fainali.
Kanuni za Fifa zinaruhusu kutumiwa picha za video na ushahidi mwingine wowote uliochukuliwa uwanjani kwa ajili ya kuwaadhibu wachezaji watovu wa nidhamu.
Adhabu ya juu zaidi inayowekwa na kanuni za Fifa ni mchezaji kuzuiwa kucheza mechi 24 au miaka miwili lakini adhabu kubwa zaidi ambayo Fifa imepata kutoa katika michuano hii ni kukosa mechi nane.
Adhabu hiyo ilitolewa kwa Mauro Tassotti wa Italia kwa kumvunja pua Luis Enrique wa Hispania 1994. Enrique ndiye kocha wa sasa wa Barcelona.
Suarez amepata pia kuadhibiwa vikali kwa kutoa lugha ya matusi na kibaguzi dhidi ya Patrice Evra wa Manchester United.