*Walters ajifunga mawili na kukosa penati
*Reading, Southampton, Sunderland safi
Mshambuliaji wa Stoke City, Jonathan Walters hataisahau Jumamosi hii, kwa kujifunga magoli mawili na kukosa penati dhidi ya Chelsea.
Wakiwa nyumbani uwanja wa Britannia, Stoke walionyesha kandanda safi, lakini waliishia kufungwa idadi kubwa zaidi waliyopata kufungwa kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) ya 4-0.
Kadhalika, ilikuwa mara ya kwanza kwa vijana hao wa kocha Tony Pulis kupoteza mchezo nyumbani msimu huu.
Walters (29) anayekipiga pia timu ya taifa ya Ireland alijifunga wakati mchezo ukielekea mapumziko, kwa kulala na kupiga kichwa ambacho kingekuwa safi kwa lango la upinzani.
Baadaye katika kipindi cha pili, Walters tena akitaka kuokoa kona ya Juan Mata. Huyu ni mchezaji aliyesifiwa sana kwa uchezaji wake katika mechi 99, lakini hii ya 100 imegeuka shubiri, kwa kumbukumbu ambayo hataisahau, na aliishia kulia machozi.
Wachezaji wengine waliopata kujifunga mabao mawili kwenye mechi moja ya EPL ni Gary Breen wa Coventry dhidi ya Manchester United mwaka 1997; Jamie Carragher wa Liverpool, pia dhidi ya United mwaka 1999 na Michael Proctor wa Sunderland dhidi ya Charlton mwaka 2003.
Chelsea walipata mabao mengine kupitia kwa penati ya naibu nahodha, Frank Lampard kwa penati baada ya Mata kuangushwa eneo la hatari.
Eden Hazard aliongeza furaha ya vijana wa Rafa Benitez kwa kupachika bao zuri la nne, lakini mzimu wa uzomeaji uliibuka upya kutoka kwa washabiki kadhaa wa Chelsea dhidi ya kocha wao wa muda.
Kwa ushindi huo, Chelsea wameshika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 41 wakati Stoke wamebaki nafasi ya 10 kwa pointi zao 29.
Chelsea walipoteza mechi zao mbili zilizopita nyumbani, moja dhidi ya wanaoshika mkia, Queen Park Rangers (QPR) waliowafunga bao 1-0 na nyingine kwenye nusu fainali ya kwanza ya Capital One Cup, walipobinywa na Swansea kwa mabao 2-0.
Kwingineko, Reading walibadilika, tofauti na walivyozoea kulegea dakika za mwisho na kufungwa, Jumamosi hii waliimarika na kuwafunga West Bromwich Albion mabao 3-2.
Goli la dakika za lala salama la Mrusi Pavel Pogrebnyak lilikuwa zawadi ya washabiki ambao hawakuondoka kwa kukata tamaa na mwelekeo wa Reading kufungwa.
Iwapo West Brom wangeshinda, wangekwea juu ya Arsenal wanaoshika nafasi ya sita, na dalili za ushindi zilionekana awali, kwa mabao mawili ya mshambuliaji wao, Romelu Lukaku aliye kwa mkopo kutoka Chelsea.
Hata hivyo, Reading walibadili mwelekeo wa mechi kuwa juu chini, kwa kupata ushindi wao wa tatu tu msimu huu kwa magoli matatu ndani ya dakika nane za mwisho.
Jimmy Kebe aliungisha wavuni majalo ya Garath McCleary, ambapo zikiwa zimebaki dakika mbili Reading walipata penati iliyowekwa wavuni na Adam Le Fondre baada ya Jonas Olsson kumwangusha Kebe.
Pogrebnyak aliwahakikishia Reading kuwa juu ya QPR kwa pointi mbili katika msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 16.
QPR walikuwa wanaombea Reading wafungwe ili wawe nafasi ya 19, kwani katika mechi ya awali walitoshana nguvu na Tottenham Hotspurs bila kufungana.
Vijana hao wa Harry Redknapp walielekea kuridhishwa na suluhu hiyo, kutokana na mwelekeo wa hivi karibuni wa Spurs wanaofundishwa na Andre Villas-Boas ambao wamekuwa na uwiano mkubwa wa ushindi kwenye EPL.
Ilikuwa mara ya kwanza pia kwa Redknapp kukabiliana na klabu yake ya zamani alikofukuzwa kabla ya Mreno huyo kuajiriwa mwaka jana.
Golikipa wa QPR alitoka shujaa nyumbani kwao Loftus Road kwa kuokoa hatari nyingi zilizoelekezwa na washambuliaji wa Spurs, wakiwamo Emmanuel Adebayor, Jermain Defoe, Gareth Bale Clint Dempsey na wengineo.
Matokeo hayo yaliwazuia Spurs mwanya wa kuwasogelea Manchester City kwa pungufu ya pointi mbili na wangeshika nafasi ya tatu.
Aston Villa wameendelea kupoteza mwelekeo, baada ya kufungwa na Southampton bao 1-0, na kubadilishana nafasi za eneo la kushuka daraja, moja ikitoka na nyingine kuingia.
Alikuwa Rickie Lambert aliyewazamisha Villa kwa bao la penati katika dakika ya 34, baada ya Enda Stevens kuadhibiwa kwa kumchezea rafu Jay Rodriguez.
Ushindi huo umewapaisha Saints hadi nafasi ya 15 na kuacha machungu kwa Villa ambao katikati ya wiki walifungwa mabao 3-1 na timu ya daraja la nne ya Bradford City katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Capital One Cup.
Everton nao walitumia vibaya uwanja wa nyumbani wa Goodison Park, walipopata nafasi za kuwapandisha kwenye nafasi nne za juu, baada ya kutoka suluhu na Swansea.
Swansea wanaofundishwa na Mmarekani Michael Laudrup waliwatuliza wenyeji, na kuhakikisha hawafungi bao.
Kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Vincente Del Bosque alikuwa uwanjani, ambapo yupo nchini Uingereza kufuatilia kiwango cha mchezaji wake, Miguel Michu wa Swansea.
Del Bosque alitamka kabla ya Krismasi kwamba Michu angepewa nafasi kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Uruguay mwezi ujao.
Wanyonge wengine wa EPL, Wigan waliambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Fulham. Franco di Santo aliwakomboa Wigan dakika ya 71 baada ya Fulham kutangulia kufunga kupitia kwa kiungo Mgiriki, Giorgos Karagonis dakika ya 22 ya mchezo.
Fulham wameshinda mechi mbili tu kati ya 14 zilizopita za EPL, matokeo hayo yanawaacha wakichungulia eneo la kushuka daraja, wakiwa na pointi sita tu juu ya Villa.
Newcastle United wa Alan Pardew wameendelea kuchechemea baada ya kutoka suluhu na Norwich City walio katikati ya msimamo wa ligi.
Newcastle wamebaki pointi mbili tu juu ya eneo la hatari, huku kocha Chris Hughton wa Norwich akiridhishwa kwa matokeo hayo dhidi ya waliomfukuza kazi Desemba 2010.
Hata hivyo Pardew atakuwa amepumua kidogo, kwani amesitisha mfululizo wa vipigo vinne dhidi ya kikosi chake kilichokuwa kikiandamwa na majeruhi na kuondokewa na mfungaji bora wa mzunguko wa kwanza, Demba Ba aliyekimbilia Chelsea.
Sunderland walipunguza hofu ya kushuka daraja, baada ya kuwatandika West Ham United mabao 3-0 katika hali ya kushangaza.
Martin O’Neill alionekana mwenye furaha kwa matokeo hayo, ambapo kabla ya mchezo alionesha wasiwasi, akisema kocha wa wapinzani wake, Sam Allardyce ni mahiri mno.
Kwa ushindi huo, Sunderland wapo pointi sita juu ya eneo la hatari. Mabao yao yalipachikwa na winga wa kulia kutoka Sweden, Sebastian Larsson na Waingereza Adam Johnson na James McClean.
Baada ya mechi hizi, viwanja viwili vitawaka moto Jumapili hii, ambapo Manchester United wanaoongoza ligi wanawakaribisha Liverpool huku Arsenal wakiwa nyumbani dhidi ya wanaoshika nafasi ya pili, Manchester City.