Utawala wa kocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani, Joacim Loew umefika tamati. Mafanikio makubwa,kuendeleza na kukiongoza kizazi kipya cha wanasoka wa Ujerumani pamoja na kuweka falsafa mpya ya soka ni miongoni mwa sifa zinazombeba Joachim Loew. Hata hivyo zama zimefika tamati.
Baada ya kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew kutangaza kuwa ataachana na ukocha wa kuinoa Ujerumani mara baada ya kumalizika mashindano ya EURO 2020 ambayo yanatarajiwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu, tayari zipo taarifa kuwa Jurgen Klopp ndiye kocha anayefikiriwa kuchukua nafasi yake.
Kwake Loew, ameinoa Ujerumani tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 alipokuwa kocha msaidizi na kufika nusu fainali akiwa Jurgen Klinsmann. Tangu alipopokea kibarua hicho kutoka kwa Jurgen Klinsmann amefanikiwa kutwaa taji la Euro na Kombe la Dunia. Loew ameiongoza Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika kusini, 2014 nchini Brazil, na nchini Urusi mwaka 2018. Vilevile ameongoza kwenye fainali za Euro mwaka 2008, 2012,2016 na za mwaka 2020.
Wakati Jrgen Klopp akihusishwa kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani, upande mwingine nyota wa zamani wa Liverpool Steven Gerard anatajwa kuwa mrithi wake. Chama cha soka cha Ujerumani kimedaiwa kupanga kumpa kazi Klopp ili kuchukua mikoba ya Loew, ikiwa na maana iwapo atakubali kuchukua kibarua hicho Liverpool watakuwa sokoni kutafuta kocha mpya.
Jina linalojitokeza ni la Steven Gerrard. Steven Gerrard akiwa anazidi kuimarika na kuthibitisha ubora wake akiwa katika klabu ya Rangers ya Scotland anatajwa kama mrithi wa Klopp kwenye klabu ya Liverpool.
Licha ya kutofanya vizuri msimu huu Liverpool lakini mashabiki wa Liverpool wanaonekana wana imani na Jurgen Klopp. Naye Jurgen Klopp mwenyewe amethibitisha kuwa ataendelea na kibarua chake cha kuinoa Lverpool na kuipa mafanikio zaidi.
Aidha, mwanzoni mwa mwezi huu katika mahojiano ya chombo cha habari alieleza kuwa suala la yeye kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani ni la baadaye sana, lakini mazingira ya kuingia kuifundisha timu hiyo hayakuzingatiwa na kujadiliwa. Na sasa Loew anatarajiwa kuondoka kwenye nafasi yake mapema hali ambayo inaweza kubashiriwa kuwa Klopp anaelekea kuinoa Ujerumani kuanzia Julai mwaka 2021, hivyo kuwa na nafasi pekee kwa Gerrard kuinoa Liverpool.
Kwa uzoefu wa mpira wa miguu wanajua ni vigumu kuamua maneno ya makocha na wachezaji haswa linapokuja suala la kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine ama fursa moja kwenda nyingine ya juu zaidi. Kwa Jurgen Klopp kuteuliwa kuifundisha Ujerumani ni suala la heshima ya juu zaidi kwa nchi yake na maisha yake binafasi.
Kwahiyo Klopp anaweza kuachana na Liverpool ili kutii maombi ya nchi yake na ndoto zake kuinoa nchi yake. Iwapo Gerrard atapewa jukumu hilo litakuwa suala la ndoto yake kuinoa timu yake aliyochezea hadi kustaafu. Ni wazi Gerrard anajiandaa kuinoa Liverpool, ingawaje haijasemwa ni lini. Klopp amewahi kutamka jambo hilo misimu ya nyuma kuwa nyota huyo wa zamani wa Anfield anaweza kurithi mikoba yake kwani anaonesha ujuzi na kujifunza kufanya vizuri.
Swali linalobaki kwa sasa ni je, Gerrard yupo tayari kurithi mikoba ya Klopp au aendelee kujifunza zaidi kazi ya ukocha kuliko kukimbilia kama ilivyokuwa kwa Frank Lampard? Hata hivyo wengine watajiuliza, ataendelea kujifunza hadi lini?
Gerrard anasifika kwa kukata ngebe za Celtic ya Scotland ambayo ilikuwa ikitamba katika Ligi Kuu nchi hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu miaka 10 mfululizo. Ujio wa Gerrard umevunja ngebe hizo baada ya wiki iliyopita kuipa ubingwa Rangers kwa mara kwanza katika kipindi cha miaka 10 ikiwa ni kumaliza ufalme wa Celtic uliokuwa umekita mizizi.
Huo ni ubingwa wa kwanza kwa Steven hali ambayo inampa ari ya kusonga mbele. lakini Liverpool ni klabu kubwa kuliko Rangers. Mahitaji yake ni makubwa, historia yake ni kubwa, jina lake ni kubwa, inashiriki Ligi ngumu ulaya na zaidi inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa mara kwa mara. Ina wachezaji wakubwa ambao Gerrard atakuwa anakutana na wachezaji wenye ego tofauti na hivyo kuwa na kibarua cha kuwaweka sawa kwa maslahi ya timu hiyo.
Wakati mjadala wa kocha mpya wa Ujerumani na Liverpool ndio kwanza unanawiri kwa upande mwingne Liverpool wana mtihani mzigo msimu huu Ligi Kuu England, hasa kupata nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Kibarua cha kufuzu Ligi ya Mabingwa kipo mikononi mwa Jurgne Klopp. Lakini matumaini ya kumaliza nafasi nne za juu msimu huu yanaoenekana kufifia. Liverpool.