Menu
in

Stars yalala, Chamakh afukuzisha kocha

Matumaini ya timu ya taifa ya soka ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, kufuzu kwa fainali zao za kwanza za Mataifa ya Afrika tangu mwaka 1980, yalipata pigo baada ya kulala 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Afrika katika mechi iliyochezwa hapa Bangui jana.

Wenyeji waliotawala kipindi cha kwanza katika uwanja uliokuwa ukiteleza kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha, walipata bao la kuongoza katika dakika ya 39 na likadumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Stars, Mdenmark, Jan Poulsen, katika kipindi cha pili kwa kuwatoa John Bocco na Mwinyi Kazimoto na kuwaingiza Mbwana Samata na Athumani Machuppa, yalileta uhai kwa Stars ambao walisawazisha goli hilo katika dakika ya 75 kupitia kwa Shaaban Nditi.

Stars almanusura iwe mbele kwa magoli 2-1 wakati Machuppa alipofunga kwa kutumia mpira wa krosi katika dakika ya 77 lakini mwamuzi alilikataa goli hilo kwa maelezo kwamba kipa alikuwa amesukumwa na wenyeji wakapata goli la ushindi katika dakika ya 80 kutokana na makosa ya kujichanganya katika safu ya ulinzi ya Stars.

Kwa matokeo hayo, Stars imeangukia katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Kundi D ikibaki na pointi zake nne nyuma ya vinara Morocco waliowasambaratisha majirani zao Algeria 4-0 na kukaa kileleni mwa kundi hilo wakiwa na pointi 7. Afrika ya Kati wamefikisha pointi 7 pia lakini tofauti nzuri ya magoli inawaweka Morocco juu, huku Algeria ambao pia wana pointi 4 sawa na Tanzania, wakiburuza mkia kwa kufungwa magoli mengi.

Mehdi Benatia alifungua milango ya Algeria kufuatia kona ya dakika ya 21 na mshambuliaji wa Arsenal, Marouane Chamakh, akauwahi mpira mtamu wa pasi ya kupenyezewa kutokea katikati ya uwanja na kufanya matokeo yawe 2-0 katika dakika ya 38.

Youssouf Hadji aliongeza goli la tatu katika dakika ya 60 kabla ya Oussama Asaidi kukamilisha kipigo hicho kizito kwa timu hiyo iliyocheza fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka jana.

Kocha wa Algeria, Abdelhak Benchikha, aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu jana, siku moja baada ya kipigo hicho cha Jumamosi, taarifa ya shirikisho la soka la Algeria lilisema. Benchikha alichukua madaraka hayo Septemba mwaka jana kutoka kwa Rabah Saadane na ameiongoza kushinda mechi moja tu kati ya nne.

Mjini Yaounde, vikosi vya usalama vya Cameroon vilitumia maji ya kuwasha jana ili kuwasambaratisha mashabiki wa soka waliokasirishwa na sare dhidi ya Senegal ambayo imezidi kutokomeza matumaini yao ya kufuzu kwa fainali hizo CAN 2012.

Nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o, alikosa penalti ya dakika ya 87, ambayo ingewasaidia kupunguza pengo la pointi dhidi ya vinara wa kundi lao Senegal, na kuchokoza hasira za mashabiki walioanza kufanya vurugu kuzunguka eneo la uwanja wa Ahmadou Ahidjo na kumsababisha Eto’o kuomba msamaha hadharani.

Mashuhuda walisema watu kadhaa walijeruhiwa wakati wa vurumai hizo, na mashabiki wa soka waliojaa hasira walivunja vioo vya magari na kuchana jezi zenye jina la Eto’o kutoka kwa mashabiki waliozivaa. Maafisa wa usalama hawakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo.

Baadaye jana, katika mahojiano mafupi na televisheni ya nchi hiyo, mshambuliaji huyo wa Inter Milan aliomba mashabiki wamsamehe.

“Ninapofunga magoli mnanibeba juu, lakini leo nimekosa penalti ambayo ingeweza kutupa ushindi na nawajibika kucheza chini ya kiwango,” alisema. “Najua jamii ya Wacameroon wanataka tushinde ili wawe na furaha. Lakini nimekosa penalti na naomba msamaha.”

Sare ya jana imeongeza uwezekano wa mabingwa hao mara nne wa Afrika kukosa kufuzu kwa fainali hizo za CAN 2012 zitakazochezwa Guinea ya Ikweta na Gabon baada ya kufanikiwa kufuzu kwa fainali nane mfululizo zilizopita.

Cameroon wana pointi tano baada ya mechi nne za kufuzu, zinazowaweka pointi tano nyuma ya vinara wa Kundi E, Senegal.

Vurugu zilitokea pia kwenye kitongoji cha mji mkuu wa Senegal wa Dakar jana baada ya umeme kukatika na kuzima televisheni na radio wakati wa mechi ikiendelea. Polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki waliokuwa wakirusha mawe.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version