WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) inaondoka nchini leo Alhamisi kuelekea Harare Zimbabwe kuwakabili wenyeji wao, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Salum Mayanga, amesema malengo waliyoyaweka kama benchi la ufundi katika timu hiyo yameanza kutimia.
Taifa Stars na Zimbabwe zinatarajia kurudiana Juni Mosi kwa ajili ya kuwania tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazochezwa Morocco mwakani.
Akizungumza jana Jumatano baada mchezo wa kirafiki juzi dhidi ya Malawi, Mayanga, alisema Stars imeanza kutekeleza yale waliyofundishwa na mwalimu hasa kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mechi yao na Zimbabwe.
Mayanga alisema katika mchezo wa kwanza na Zimbabwe wa kufuzu kucheza fainali za AFCON, Taifa Stars ilikuwa na mapungufu kadhaa hasa kwenye safu ya ushambuliaji na kiungo na kwamba kupitia mechi ya kirafiki waliyocheza juzi na Malawi makosa hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Alisema kutokana na hali hiyo wanaamini mechi ya marudiano na Zimbabwe kikosi hicho kitafanya vizuri zaidi hasa baada ya kuonesha matumaini makubwa katika mchezo wao na Malawi.
Katika mchezo huo wa kirafiki Stars ilitawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ambapo mchezo huo ulikuwa maalumu kwa maandalizi ya kurejeana na Zimbabwe.
Katika mchezo wa Jumapili huko Harare Taifa Stars itahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili waweze kusonga mbele katika michuano hiyo .
Afisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura, alisema wapo watanzania wengi watakaosafiri hadi Harare kuisapoti timu hiyo ili iweze kusonga mbele.
Wambura alisema kuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ndiye atakuwa mkuu wa msafara wa timu hiyo ambayo ilicheza fainali hizo kwa mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1980.