Kesho Jumapili timu ya taifa ya Tanzania itacheza na Malawi katika mchezo wa marudiano wa mzunguko wa awali wa kuwania kushiriki Kombe la Dunia 2018. Stars inakwenda kwenye mchezo huo utakaopigwa ndani ya dimba la Kamuzu Stadium jijini Blantyre ikiwa mbele kwa mabao mawili kufuatia ushindi iliyoupata siku ya Jumatano jijini Dar-es-salaam dhidi ya wapinzani wao hao.
Kwa mara nyingine tena niwapongeze Stars kwa kuweza kuutumia vyema uwanja wa nyumbani hapo Jumatano. Hili litamfanya mwalimu Charles Boniface Mkwasa aliyepewa mkataba wa kudumu wa kuinoa Stars siku chache zilizopita kuwa kwenye hali ya utulivu kuelekea mchezo wa hapo kesho.
Na pia kuwa mbele kwa mabao hayo mawili kunawafanya wachezaji wa Stars kuwa kwenye hali ya kujiamini. Ni vizuri zaidi pia kuwa ushindi huo umewafanya washabiki na wadau wa soka nchini Tanzania kuendelea kuwa na imani na kikosi cha Taifa Stars chini ya mwalimu Charles Boniface Mkwasa. Hivyo Stars itakuwa ikiungwa mkono kwa kiasi cha kutosha na mashabiki hapo kesho.
Hata hivyo nikumbushe kuwa mchezo dhidi ya Malawi bado uko wazi mno. Wachezaji wetu hawatakiwi kuamini kuwa kazi waliyobakisha ni ndogo. Kazi iliyobakia si ndogo hata kidogo na kama wachezaji wetu hawatajituma kwa nguvu zote na kufuata kwa umakini maelekezo ya mwalimu Mkwasa na benchi lake la ufundi matokeo yanaweza kugeuzwa jijini Blantyre hapo kesho.
Timu yetu inahitaji kuwaheshimu wapinzani na kuwa na tahadhari ya kutosha kwenye mchezo huo. Kuna mambo kadhaa yanayotoa onyo kwa Taifa Stars kuelekea mchezo wa kesho. Kwanza mwalimu Ernest Mtawali amekosolewa kupita kiasi na wachambuzi na wadau wa soka nchini Malawi kufuatia kipigo cha 2-0. Hivyo kwa vyovyote vile amejizatiti kukiongoza kikosi chake kuweza kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa kesho.
Ikumbukwe pia mshambuliaji Chiukepo Msowoya aliyekuwa majeruhi amerejea kwenye kikosi cha Malawi na kuna uwezekano mkubwa mwalimu Mtawali atamuanzisha hapo kesho. Mshambuliaji huyu wa zamani wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini ana uwezo mkubwa wa kupachika mabao hivyo walinzi wetu wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kumdhibiti.
Zaidi ya hapo Malawi ni timu bora zaidi ukilinganisha na Taifa Stars. Hiyo ni kulingana na viwango vya ubora vya FIFA vilivyotolewa tarehe 1 mwezi huu ambapo Malawi ipo kwenye nafasi ya 101 wakati Tanzania tupo kwenye nafasi ya 136. Kwa vovyote vile viwango hivi vya FIFA vya hivi karibuni vinatuelekeza kuwaheshimu wapinzani wetu kuelekea mchezo wa kesho.
Hata ukitazama ushiriki wa michuano mikubwa kwenye miaka ya karibuni utagundua kuwa Malawi ni timu bora zaidi. Wakati Tanzania tukiwa hatujashiriki Kombe la Mataifa ya Afrika tangu mwaka 1980 Malawi walishiriki michuano hiyo mwaka 2010.
Jambo lingine ni kwamba kikosi cha Malawi kimepata muda wa kutosha wa kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa kesho ukilinganisha na kikosi cha Stars. Mara baada ya kurudi nchini kwao juzi Alhamisi walianza mazoezi mara moja jana asubuhi wakati Stars iliyoingia Malawi hapo jana haitakuwa na muda wa kutosha kwa ajili ya kujiandaa ukilinganisha na muda waliopata Malawi.
Mbaya zaidi kusafiri kwa basi hapo jana kutoka Lilongwe mbaka jijini Blantyre ambapo kuna umbali wa zaidi ya kilomita 250 kumewaongezea uchofu wachezaji wa Taifa Stars. Wachezaji wetu wanatakiwa kukumbuka kuwa mchezo bado uko wazi. Wanatakiwa kupigana kwa nguvu zote hapo kesho ili kusonga mbele.