Stars kwenda Misri kwa mafungu
Timu ya taifa ya soka, Taifa Stars
Msafara wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, utaondoka kwa mafungu kuanzia kesho kuelekea Cairo nchini Misri ambako watashiriki michuano ya nchi sita ya Bonde la Mto Nile.
Akizungumza jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni, alisema kuwa kundi la kwanza linalotarajiwa kuondoka kesho litakuwa na watu tisa.
Kayuni aliwataja watakaoondoka kesho kuwa ni pamoja na waamuzi wawili kutoka nchini wanaokwenda kuchezesha michuano hiyo na ambao wana beji za Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA), Oden Mbaga na John Kanyenye.
Alisema waamuzi hao watatua Misri wakiwa pia na kocha wa Stars, Jan Poulsen, atakayekuwa akitokea kwao Denmark.
Alisema kuwa kundi la pili ambalo litakamilisha idadi ya wanaokwenda Cairo kufikia 32, litaondoka Jumapili.
Aliongeza kuwa uondokaji huo wa mafungu umetokana na wenyeji wa mashindano hayo kutuma tiketi kwa awamu mbili.
Wakati huo huo, kocha msaidizi wa Stars, Sylvester Marsh, alisema kuwa wachezaji wake wanaendelea vizuri na mazoezi na jana walitarajiwa kuanza kujifua usiku kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi zitakazochezwa usiku, ikiwemo ya ufunguzi watakayovaana na wenyeji Misri.
Marsh alisema kuwa wameamua kubadili muda wa kufanya mazoezi waizoee hali ya hewa ya usiku na vile vile kuepuka kufanya mazoezi katika hali ya joto wakati hivi sasa, Cairo kuna baridi.
“Tumebadilisha muda wa mazoezi ili kuwaandaa wachezaji kuzoea hali ya hewa na hadi kufikia leo (jana), nimefurahishwa na jinsi wachezaji wanavyojituma mazoezini, kila mmoja anaonyesha kwamba yuko makini na ana dhamira ya kufanya vizuri,” alisema kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar.
Alimtaja kiungo Rashid Gumbo kutoka Simba aliyechukua nafasi ya Henry Joseph kuwa naye tayari amesharipoti mazoezini na wachezaji wote 23 walioitwa wako katika hali nzuri.
Mshambuliaji Athumani Machuppa, aliiambia NIPASHE jana kuwa amepania kujituma katika kuitumikia nchi yake na anaamini kwamba mchanganyiko uliopo sasa utasaidia kuwaongezea ushindani kikosini.
Machuppa anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Vasalunds IF ya Sweden, alisema kuwa hataki kumuangusha kocha Jan Poulsen na hivyo atajituma muda wote ili kuipaisha Stars.
Mara ya mwisho, Machuppa aliitwa Stars mwaka 2008 na mtangulizi wa Poulsen, Mbrazil Marcio Maximo, wakati wakijiandaa kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Malawi. Mechi hiyo haikuchezwa baada ya kuahirishwa.