TANZANIA imepangwa kundi moja na wenyeji kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani, CHAN, zitakazofanyika huko kuanzia Februari 22.
Tanzania ilipata tiketi hiyo baada ya kufanya vizuri mechi zake za ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuzitoa Kenya, Uganda na Sudan.
Iliifunga Kenya kwa jumla ya mabao 2-1, ikaichapa Uganda kwa idadi hiyo baada ya kuifunga bao 1-0 Dar es Salaam na sare ya 1-1 mjini Kampala.
Stars iliifunga Sudan mabao 3-1 mjini Dar es salaam kabla ya kuichapa timu hiyo mabao 2-1 mjini Khartoum, Sudan katika mchezo wa marudiano.
Kwa mujibu wa mipangilio ya makundi ya timu za fainali, Ivory Coast na Ghana zimepewa nafasi ya kuwa ‘mabosi’ wa makundi na kutengenishwa katika makundi tofauti.
Kutokana na droo hiyo iliyofanyika juzi, kwenye mji wa Abidjan, wenyeji Ivory Coast wamepangwa kundi A pamoja na Tanzania, Zambia na Senegal.
Kundi B litakuwa na Ghana, Zimbabwe, DR Congo na Libya.
Ratiba ya ufunguzi wa michuano hiyo, wenyeji Ivory Coast watafungua pazi la michuano hiyo kwa kuipambana na Zambia wakati ufunguzi wa Kundi B ni kati ya Ghana itakayovaana na Zimbabwe.
Zimbabwe iliiondosha Afrika Kusini wakati Tanzania iliitupa nje Sudan kwa jumla ya mabao 5-2. Michuano hiyo imepangwa kumalizika Machi 8.
Fainali za michuano hiyo zitafanyika kwenye mji wa Bouake, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Ivory Coast na ndiyo uliokuwa ukishikiliwa na waasi.