*Hull, Stoke sare, kadi nyekundu kama kawaida.
Tottenham Hotspur wamewachakaza Queen Park Rangers (QPR) mabao 4-0 huku Hull waliowakaribisha Stoke wakiwabana na kwenda nao sare ya 1-1.
Spurs wameanza ligi vyema chini ya kocha wao mpya, Mauricio Pochettino kwani walishinda pia mechi yao ya kwanza, huku upande wa pili ikiwa ni kilio kwa kocha mkongwe, Harry Redknapp aliyepoteza pia mechi ya kwanza.
Baada ya mechi hiyo, timu mbili hizo zilitenganishwa na nyingine 18, kwa Spurs kuwa kileleni wakati QPR wakiwa mkiani. Ni kumbukumbu mbaya kwa Redknapp ambaye alifukuzwa klabuni hapo misimu miwili iliyopita pasipo kosa lolote.
Winga Nacer Chadli alifunga mabao mawili, huku mlinzi Eric Dier na mshambuliaji Emmanuel Adebayor wakifunga bao moja moja kwa Spurs. Redknapp alijiunga QPR 2012 wakielekea kushuka daraja, akashuka nao kisha kuwapandisha.
Ni mapema mno kuwahukumu, lakini lazima wakaze buti kwa sababu wanao wachezaji mahiri kama walinzi wa kati Rio Ferdinand aliyetoka Manchester United na Steven Caulker aliyehamia London akitoka Cardiff.
Kocha Redknapp anayesaidiwa na aliyepata kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya England, Glenn Hoddle aliwaanzisha kwa mara ya kwanza wachezaji wake wapya, Leroy Fer na Mauricio Isla ambao pengine watakuwa wazuri baada ya kuzoea.
HULL PUNGUFU SARE NA STOKE
Katika mechi nyingine ya alasiri kwa saa az England ilishuhudia Stoke waliokuwa wamewazidi Hull kwa mtu mmoja wakikaribia kuzama hadi bao la dakika za mwisho la kusawazisha.
Beki wa kati wa Hull, James Chester alipewa kadi nyekundu dakika ya 14 tu ya mchezo kutokana na kumchezea vibaya Glenn Whelan, lakini walikuwa wenyeji hao waliotangulia kupata bao kabla tu ya nusu ya kwanza kumalizika, likifungwa na Nikica Jelavic.
Hata hivyo, bao la dakika ya 84 la Ryan Shawcross lililotokana na mkwaju wa karibu uliokwenda chini chini katika kona ya kushoto ya goli liliokoa pointi moja kwa wageni. Hilo lilipatikana baada ya Phil Bardsley kugonga mlingoti wa goli.