Tottenham Hotspur walilazimika kufanya kazi ya ziada kupata ushindi dhidi ya Sheriff Tiraspol.
Wakicheza kwa kujituma tangu mwanzo, Spurs wanaofundishwa na kocha Mreno Andre Villas-Boas walitulizwa na vijana wa Sheriff.
Ilikuwa nusura Spurs wafungwe mabao kama matatu, lakini hatimaye katika kipindi cha pili alikuwa Eric Lamela aliyepata bao lake la kwanza tangu kusajiliwa.
Jermain Defoe naye aliweka rekodi kwa kufunga bao la 23 katika mashindano ya Ulaya, rekodi ambayo ni ya juu zaidi katika klabu yake hiyo ya London Kaskazini.
Kwa ushindi huo, Spurs wamefuzu kusonga hatua inayofuata na hivyo watakuwa na msongamano wa mechi kama ilivyokuwa msimu uliopita. Inaweza kuwa vyema kwa wachezaji wasiopata nafasi ili nao waoneshe uwezo kwa kuzungusha kikosi.
Katika matokeo mengine, Swansea walishindwa kulinda uongozi wao kwa kwenda sare ya bao 1-1 na Kuban Krasnodar wakati Rubin Kazan waliwafunga Wigan bao 1-0.
FC St Gallen walifungwa nyumbani kwa mabao 2-3 walipocheza na Valencia ambao wamefuzu kwa hatua ijayo huku Lazio wakiwafunga Apollo Limassol mabao 2-1.
Tromso nao waliokuwa nyumbani walichinjwa na Anzhi Makhachkala bao 1-0, AZ Alkamaar wakawafunga bao 1-0 Shakhter Karagandy, Maccabi Haifa wakaenda suluhu ya bao 1-1 na PAOK Salonika.
Mechi nyingine zilishuhudia Ludogorets Razgrad wakitoka sare ya 1-1 na Chornomorets Odesa, miamba PSV wakawaangusha Dinamo Zagreb kwa 2-0 wakati Esbjerg fB wakiwapiga bao 1-0 Elfsborg.