Liverpool wawasasambua Newcastle 6-0
Vita ya kuwania nafasi tatu muhimu katika Ligi Kuu ya England (EPL) imeendelea kwa Manchester City kuipigania nafasi ya pili, huku Tottenham Hotspurs wakishindwa kuwashusha Arsenal katika nafasi ya tatu.
City walioachia kombe kwa majirani zao, Manchester United baada ya kufungwa na Spurs 3-1 wikiendi iliyopita, walitokwa jasho kuweza kuwafunga West Ham United 2-1.
Lakini hesabu za soka siku zote huenda ndivyo sivyo, ambapo Jumamosi hii nusura Wigan wawapopote Spurs, kwani walihitaji msaada wa mchezaji wa Wigan, Emmerson Boyce aliyejifunga dakika za mwisho kuepuka kichapo.
Wigan wanaopigania kuepuka kushuka daraja, wakishika nafasi ya 18 kwa pointi 32, walianza kufungwa kwa bao la Gareth Bale, kabla ya Boyce kusawazisha, Callum McManaman kufunga la pili, na kwa bahati mbaya, Boyce kutikisa nyavu za Wigan mpira ukielekea kumalizika.
Spurs walikuwa wakiwania pointi tatu muhimu, ambazo zingewafikisha nafasi ya tatu kwa kuwashusha Arsenal na Chelsea, lakini hesabu za Andre Villas-Boas hazikwenda vyema, na watahitaji kuweka jitihada zaidi mechi zijazo ili wasiangukie tena Ligi ya Europa kama msimu huu, maana wapo nafasi ya tano, nyuma ya United, City, Arsenal na Chelsea.
City walipata mabao yao kupitia Sergio Aguero na Yaya Toure kwa bao la kifundi, lakini Aguero ambaye huwa ni shujaa wa City, alikosa mabao mengine mawili, hakuonekana kuwa fiti sana.
Andy Carroll alifunga bao la kufutia machozi dakika za mwisho, akimfunga Joe Hart kwa tobo, muda mfupi baada ya kipa huyo wa timu ya taifa ya England kuonekana kuumia.
Timu nyingine inayofukuzia nafasi nne za juu, japo kwa mbali, Everton ya David Moyes, ilipata ushindi mwembamba nyumbani Goodison Park kwa bao 1-0 dhidi ya Fulham.
Nyota wa Afrika Kusini, Steven Pienaar alikwamisha mpira kimiani kwa ustadi wa aina yake, kufuatia majalo ya Seamus Coleman, hivyo kuwafanya Fulham wapoteze mechi ya nne mfululizo.
Everton sasa wapo pointi tatu nyuma ya Spurs, na nusura wapate mabao zaidi kupitia kwa wachezaji wao nguli, Marouane Fellaini na Kevin Mirallas. Fulham walipata pigo baada ya tegemeo lao msimu huu, Dimitar Berbatov kuumia, lakini nyota wao mwingine, Urby Emanuelson nusura awasawazishie. Fulham wapo nafasi ya 11 na kwa mwezi mzima wamebakiwa na pointi zile zile 40.
Liverpool walianza maisha bila Luis Suarez aliyefungiwa mechi 10 kwa kumng’ata Branislav Ivanovic wa Chelsea kwa kuwashindilia Newcastle 6-0.
Wakimtumia nyota wa kimataifa wa England, Daniel Sturridge kwenye ushambuliaji, Liverpool walikuwa wanaongoza 2-0 hadi mapumziko.
Liverpool hawakuonekana kuwa na upungufu kutokana na kutokuwapo Suarez, na mchezaji wake mpya wa msimu huu aliyekuwa nje kwa majeraha, Fabio Borini alirejea dimbani.
Mabao ya Liverpool yalifungwa kupitia Daniel Agger, Jordan Henderson mawili; Sturridge mawili na Borini.
Ushindi huo unawaweka Liverpool nafasi ya saba nyuma ya Everton na mbele ya West Browmwich Albion na unawaacha Newcastle wakiwa nafasi ya 16 na sasa wanatishiwa kuvutwa eneo la kushuka daraja.
Kabla ya mechi, kocha wa Newcastle, Alan Padrew alisema ilikuwa muhimu kwao kushinda, lakini waliishia kufungwa, na wakaomboleza, tofauti na kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers aliyekuwa amevalia mavazi meusi.
Kocha Steve Clark alikuwa mtu mwenye furaha Jumamosi hii, baada ya West Bromwich Albion kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Southampton ambao hawakuwa wamefungwa kwa zaidi ya mechi saba.
Mabao ya Baggies yalifungwa na Marc-Antoine Fortune, Romelu Lukaku aliyemchambua kipa Artur Boruc na Shane Long.
Ilikuwa mechi ya aina yake, ambapo wachezaji watatu walipewa kadi nyekundu; Gaston Ramirez na Danny Fox wa Southampton na Fortune wa West Browm.
Stoke City nao wameanza kujiweka kwenye eneo salama katika EPL, baada ya kuwafunga Norwich City bao 1-0, lililowekwa kimiani na Charlie Adam.
Vijana wa kocha Tony Pulis walipokea na kutimiza maelekezo yake, kwani ni wiki iliyopita tu aliwataka kukaza buti kama wanataka kubaki EPL. Bao lao lilipatikana baada ya Adam kupokea pasi ya kubetua ya Peter Crouch na kuwamaliza Norwich.
Kwa matokeo hayo, Stoke wanashika nafasi ya 12 wakiwa na pointi 40 sawa na Fulham, wakati Norwich wametikiswa kidogo, kwa kubaki na pointi zao 38 katika nafasi ya 14, ikiwa ni pointi saba kutoka eneo la hatari.