Ilikuwa kazi ngumu Arsenal kumsajili Mesut Ozil kutoka Real Madrid, iliyotiwa mikono na wapinzani wakubwa kuivuruga.
Wakati Arsene Wenger na viongozi wenzake Arsenal walihangaika tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa kusajili nyota, wenzao walikuwa wakiwaombea mabaya.
Imeripotiwa sasa kwamba Mwenyekiti wa Tottenham Hotspur, Daniel Levy anayejulikana sana kwa ung’amuzi na kupata madili makubwa ya wachezaji, aliingiza mkono wake.
Levy aliyechelewesha kumuuza Gareth Bale hadi siku ya mwisho ya usajili, alirudi tena nyuma na kuwataka Real Madrid wasiwauzie mahasimu wao (Arsenal) Ozil.
Hata hatua ya kuchelewesha mauzo ya Bale inachukuliwa kama roho ya kwa nini, kwa vile Bale alishaamua kuhama, akakataa kufanya mazoezi na alishakubaliana malipo yake na Real Madrid.
Hata hivyo, Levy na kocha wake, Andre Villas-Boas walijidai kana kwamba walikuwa wakisubiri wasajili mchezaji mwingine kabla ya kumwachia Bale.
Spurs walipata kitita cha pauni milioni 85.3 katika dili la mchezaji huyo, lakini baada ya kuzipata, Levy alimpigia simu Rais wa Real Madrid, Florentino Perez kumsihi asiwauzia Arsenal Ozil kwa sababu ni wapinzani wao wakubwa.
Eti Levy aliona kwamba kumuuza huko kutaharibu ile imani iliyokwishawekwa juu ya urafiki baina ya Spurs na Real Madrid, na huo ungeonekana kama usaliti.
Arsenal ndio mahasimu wakubwa wa Spurs kwa eneo la London Kaskazini na Spurs wamekuwa wakijaribu kuwafukuzia kwa kila namna, lakini hawajawahi kumaliza ligi juu yao kimsimamo.
Levy anaelezwa kusema kwamba wana uhusiano maalumu na Real Madrid, ndiyo maana wamewapa Bale baada ya kuwapa tena kiungo mwingine, Luka Modric.
Spurs walipata kuwauliza Real Madrid Julai mwaka huu iwapo Ozil alikuwa anauzwa, wakaambiwa hapana, ambapo walitaka awe katika dili ya kumtoa Bale na kumpata Ozil pamoja na kiasi cha fedha.
Hata hivyo, baada ya Bale kutua Madrid pamoja na kocha mpya, Carlo Ancelotti, ilimaanisha kwamba walihitaji viungo washambuliaji wachache kwa mfumo anaoupenda.
Alichofanya Rais Perez wa Real Madrid ni kumkatalia kwa upole Levy wa Spurs na kumruhusu Ozil kujiunga na Arsenal kwa ada ya pauni milioni 42.5 na kukata kilimilimi cha Spurs.
DAVID MOYES AJARIBU KUMTIBUA WENGER
Naye Kocha wa Manchester United, David Moyes, hata baada ya kujua Arsenal wanamchukua Ozil, alijaribu kutumia kila nguvu kumzuia ili amchukue yeye.
Simu zilikuwa hazikatiki kutoka Old Trafford Jumatatu – siku ya mwisho ya usajili wa msimu wa kiangazi, zikitaka kwa namna yoyote ile Ozil asiende Emirates bali Manchester.
Moyes alimtaka Ozil baada ya kushindwa kumsajili Wesley Sneijder wa Galatasaray, maana United wanahitaji mno kiungo nyota kwenye timu yao.
Uamuzi wa Moyes unashangaza, kwa sababu wiki mbili kabla alikuwa ameambiwa na mtu wa tatu kwamba Ozil alikuwa tayari kwa ajili ya kuuzwa, lakini akaonesha hamtaki.
Ilikuwa wakati Arsenal wakijiandaa kumchukua, ndipo Moyes akataka kumvutia kwake kama Chelsea walivyomchukua Willian wa Anzhi Makhachkala aliyekuwa anakaribia kujiunga Spurs.
Wachambuzi wa mambo wanauliza kulikoni Moyes wakati huo alikataa, halafu atake kumharibia mwenzake dakika za mwisho.
Pengine alikuwa amejiamini kwamba angeweza kusajili majina makubwa, lakini alishindwa kwa akina Cesc Fabregas, Thiago Alcantara na wengineo, akaishia kumnasa mchezaji wake wa zamani, Marouane Fellaini.
Moyes ameahidi kuendeleza jitihada zake za kupata wachezaji aliowakosa katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani, wakiwamo pia Leighton Baines wa Everton na Ander Herrera wa Athletic Bilbao.
Moyes ameishia kusajili mchezaji mmoja tu na kutumia pauni milioni 23.5m kwa Fellaini.
Naye Kocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani, Joachim Low ameeleza kushangazwa kwake na uamuzi wa Real Madrid kumuuza Ozil kwa Arsenal.
Amesema anashindwa kuelewa ni kwa vipi waliamua kumuuza mmoja wa viungo washambuliaji bora zaidi duniani.
Ozil anacheza chini ya Low Ujerumani, na kocha huyo alisema Arsenal wamelamba dume, kwa sababu chini ya kocha mzuri kama Wenger na mipango ya klabu, watafanya vizuri, na Ozil atafaidi kwua na Wajerumani wenzake, Lukas Podolski na Per Mertesacker.