in , ,

SportPesa waingia Tanzania


*Wamwaga Tsh milioni 50 Serengeti Boys

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kushirikiana
kikamilifu na kampuni inayoongoza kwenye michezo ya kubahatisha ya
SportPesa, iliyozindua shughuli zake rasmi jijini Dar es Salaam.

Katika hafla iliyofana Hyatt Plaza, shughuli hiyo ilirushwa mubashara
kuanzia saa 05:55 kwa saa za Afrika Mashariki, huku kampuni hiyo
ikitangaza mara moja udhamini wa Tsh milioni 50 (zaidi ya USD 22,000)
kwa Timu ya Taifa ya Soka ya Vijana – Serengeti Boys watakaoshiriki
kwenye mashindano ya Afrika nchini Gabon.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo,
Dk. Harrison Mwakyembe aliikaribisha kampuni hiyo, akisema ni mshirika
mwenye thamani kubwa kwenye sekta ya michezo.

“Nawashukuru kwa kuona fursa na uwezo mkubwa uliopo Tanzania, si tu
katika kukuza michezo lakini pia kutoa nafasi za ajira. Nawahakikishia
kwamba wizara yangu itawaunga mkono, karibuni kwenye nchi ya michezo.
Hii ni fursa ya kipekee na muhimu kuendeleza michezo na hatutaiacha
iende,” Mwakyembe aliiambia hadhira iliyokuwapo.

Waziri alihudhuria hafla hiyo, akiwa amesafiri umbali wa kilometa 600
kutoka Dodoma hadi Dar usiku, baada ya kuwasilisha mapendekezo ya
bajeti ya wizara yake bungeni. Anasema huu ni wakati bora zaidi ambao
SportPesa wamechagua kuwekeza nchini Tanzania.

“Bunge limepitisha mapendekezo ya bajeti ya wizara yangu baada ya
mjadala mkali na mrefu ulioanza Ijumaa. Wawakilishi wa wananchi
hawafurahii kasi iliyopo kwenye maendeleo ya michezo.

“Nawashukuru wabunge kwa kuwa wakali kwangu. SportPesa ndiyo nguzo ya
matumaini yangu katika kuendeleza michezo Tanzania na labda mwaka
kesho hawatanipa (wabunge) wakati mgumu kama wa mwaka huu,”
akasisitiza Mwakyembe.

Mapema, Mkurugenzi wa Utawala wa SportPesa (Tazania), Abbas Tarimba
alikuwa na haya ya kusema:-

“Tunalenga kubadilisha uso wa maendeleo ya soka ncini kama sehemu ya
dhima yetu. Nawaasa Watanzania kuwa wavumilivu hadi Jumamosi ndipo
tutatangaza rasmi timu tutakazokuwa washirika nazo kwenye soka.

“Tanzania ina vipaji vingi, akiba Mbwana Samatta wengi na watapata
fursa zao kupitia mafunzo kwenye kambi, kwa sababu tunayosema
tutayatekeleza. Katika miezi michache ijayo tutatangaza mipango
mikubwa ya soka,” akaahidi Tarimba.

Mkurugenzi Mkuu wa Mpito katika Uwekaji Dau Tanzania, James Mbawe
alitamka rasmi kwamba SportPesa wamepewa leseni ya kufanya kazi ncini
baada ya kukidhi viwango na kanuni zote katika michezo ya kubahatisha.

“Haya ni mafanikio makubwa kwa Tanzania kwa sababu itaongeza kuonekana
kwetu, tunaona fahari kwa kuja kwao,” akasema.

Alieleza kwamba uwekaji dau kwenye michezo ni moja ya sekta zinazokua
zaidi nchini Tanzania, ambapo michezo hiyo imeipatia Serikali Tsh
bilioni 21.9 kwa mwaka wa fedha, wakiwapita casino walioingiza Tsh
bilioni 21.2.

“Utazamaji soka lilikuwa suala la kijamii hadi miaka minne iliyopita,
lakini kucheza kutabiri matokea kumeanzisha sekta mya na kujenga ajira
na miradi ya kijamii.

“Serikali imetambua mafanikio yake. Tutahakikisha tunawalinda
washindi, familia na Tanzania dhidi ya athari hasi za uwekaji dau
kwenye michezo,” akasisitiza Mbawe.

Pande zote zitafaidika na uwapo wa ushirika wa SportPesa na klabu
kubwa za Ligi Kuu ya England kama Arsenal, Southampton na Hull City,
klabu za kwanza kwenye daraja la juu nchini humo kudhaminiwa jezi na
chapa kutoka Afrika, na matarajio ni kuwapo washirika wengi wa ndani.

SportPesa ilianzishwa Kenya 2014 na ina ofisi zake Liverpool, Nairobi
na sasa Dar es Salaam.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

HATIMAYE ARSENE WENGER AVUNJA MWIKO

Tanzania Sports

HILI LA UWANJA, TFF INAZIDI KUCHANA NGUO ZAKE ILI TUONE NYETI ZAKE