Menu
in

Soka ya Tanzania na kina Eto’o wao

UJIO wa kikosi cha Cameroon katika anga ya Tanzania kuumana na Tanzania `Taifa Stars’ jioni ya Juni 15 mwaka huu, uliwashitua wengi.

Si kwamba hawakujua Cameroon ingetua kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa michuano ya awali ya Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2010 kule Afrika Kusini, la hasha, bali uimara wa kikosi chao.

Kwa hakika, Cameroon inayoongoza kwa ubora wa soka Afrika, ilisheheni nyota halisi wa soka, wakiongozwa na Samuel Eto’o Fils, Mwanasoka Bora wa Afrika mara tatu aliyewahi pia kushika nafasi ya tatu kwa Ubora duniani.

Ukiachana na nyota huyo anayetikisa katika soka ya Hispania akiwa na klabu ya FC Barcelona, wakali wengine waliokuja nchini ni Rigobert Song Bahanag, nahodha na beki mahiri aliyewahi kung’ara akiwa na L:iverpool ya England. Sasa anaichezea Galatasaray ya Uturuki.

Walikuwapo pia Alexander Song, binamu wa Rigobert ambaye kwa sasa anaichezea Arsenal ya England, kipa Idriss Carlos Kameni wa Espanyol ya Hispania, Geremi Sorele Njitap Fotso wa Newcastle ya England, Stephen William Nsoyuka Mbia (Stephen Mbia) wa Rennes ya Ufaransa na Timothee Atouba wa Hambuger SV ya Ujerumani.

Hawakukosekana akina Modeste Mbami, mkongwe katika kikosi cha Cameroon anayeichezea Marseille ya Ufaransa, Pierre Achille Webo Kouamo wa Mallorca ya Hispania, Andrey Bikey Amugu wa Reading ya England na wengine.

Hawa wote ni mahiri na wana uzoefu mkubwa wa soka ya ushindani wa kimataifa kuanzia ngazi za klabu, na hata timu ya taifa wakiwa wameiwakilisha nchi yao hadi Kombe la Dunia.

Kocha wao, Otto Pfister alikusanya wachezaji hao wanaovuna utajiri mkubwa wa fedha Ulaya kwa ajili ya kuja kuiadabisha Tanzania, nchi dhaifu kisoka inayoshika nafasi ya 23 kwa ubora Afrika.

Lakini haikuwa hivyo, pamoja na kutua kwa maringo na kujiamini mno, walikutana na wakati mgumu siku ya mchezo, kwani hawakupewa kabisa nafasi ya kupumua.

Hakuonekana Eto’o mwenye kashkashi Ulaya, wala Song ambaye alilazimika kucheza ubabe na hata kumtwanga ngumi kavukavu winga machachari anayekuja juu katika soka ya Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa.

Si Ngassa tu, bali Ivo Mapunda, Nsajigwa Shadrack, Amir Maftah, Salum Swedi, Nadir Haroub `Cannavaro’, Godfrey Bonny, Athuman Idd, Shaaban Nditi, Danny Mrwanda, Nizar Khalfan, Kigi Makasi, Abdi Kassim, wote walicheza kitimu na kuwanyima raha kabisa wageni.

Na kama si ubutu wa washambuliaji wa Tanzania, kwa hakika jioni ya Juni 14 ingekuwa ya aibu kwa Cameroon waliobahatika kupiga mashuti matatu tu ya maana katika lango la Stars.

Tafsiri rahisi ni kwamba, wachezaji wa Tanzania, ingawa karibu wote wanacheza soka katika klabu za nyumbani isipokuwa Nizar Khalfan na Danny Mrwanda wanaoichezea klabu ya Al Tadhamon ya Kuwait, walionyesha kwamba, na wao wanaweza.

Si kwamba ninawavimbisha kichwa, bali walionyesha uwezo halisi wa soka, hivyo kushindwa kutofautisha kati ya akina Eto’o na hawa wa Tanzania.

Huu ni thibitisho thabiti kwamba, Tanzania ina vipaji kama zilivyo nchi nyingine zilizopiga hatua kisoka duniani.

Ndiyo maana haikushangaza kumsikia Eto’o akisema baada ya mchezo kwamba, haamini kama Tanzania haina wachezaji wa kulipwa Ulaya.

Hii ina maana kwamba, kama walivyokubali Watanzania juu ya soka ya maajabu iliyoonyeshwa na mabalozi wao, hata Cameroon, pamoja na kuzoea soka ya kisasa, wameikubali soka ya Tanzania.

Pengine tujiulize, kama ukweli ndio huo, kwa nini tusifike huko waliko akina Eto’o, kama Nonda Shabani aliyekulia Yanga, tena akiwekwa benchi na Mohammed Hussein Daima `Mmachinga’ aliweza kufurukuta na kuwa miongoni mwa nyota halisi wa soka barani Ulaya kuanzia akiwa na FC Zurich ya Uswisi, Rennes ya Ufaransa na baadaye Monaco pia ya Ufaransa alikokwenda kumrithi David Trezeguet wa Juventus ya Italia?

Tatizo kubwa ninaloliona ni kukosekana kwa nafasi ya kuwatangaza wachezaji wetu katika ngazi za kimataifa.

Hata Nonda hakubahatika kwa sababu ya mawakala wetu, bali alijipeleka Afrika Kusini alikochemsha na kurejea kwao Burundi, lakini baada ya kujiuliza akajirudisha Afrika Kusini alikoweka bidii na hatimaye kulamba dume.

Nonda aliyekuwa anaomba nauli ya daladala baada ya mazoezi kutoka Kariakoo kwenda kwao Mwananyamala Koma Koma, si Nonda wa leo. Huyu wa sasa ni milionea wa kutisha aliyeanza kulipwa mshahara mnono tangu mwaka 1998, wakati huo akilipwa sh milioni 20 za Tanzania kwa wiki akiwa na Rennes.

Pamoja na kukosekana kwa mawakala wa uhakika, wanasoka nao wamekuwa watu wa kulewa sifa.

Imeshatokea mara kadhaa kwa wanasoka wetu kupata timu Afrika Kusini, na nchi nyingine za Afrika na hata nje ya hapo, lakini hakuna la maana wanalolifanya.

Wamekuwa watu wa kubweteka na kutokuwa tayari kukubaliana na changamoto za soka ya kisasa ya wenzetu, badala ya kujikita katika kujifunza mambo mengi ili wapate mafanikio ya kweli ya soka, wao huona ni bora kurudi Tanzania wanakoabudiwa na kumwagiwa kila kukicha na vyombo vya habari.

Bila shaka, kwa wakati tulionao, lazima tukubali kwamba, soka ni ajira na biashara kubwa pengine kushinda biashara yoyote halali duniani.

Na kwa bahati nzuri, kwa vipaji vya wanasoka wetu, wana nafasi kubwa ya kuingia katika soko hilo, kama wakiamua na wakati huohuo wakawepo watu wa kuwashika mkono na kuwaelekeza njia za kupita kuelekea soko la kimataifa.

Ndiyo maana naamini, Tanzania ina akina Eto’o wengi, lakini wamekosa ujanja wa kutoka na kuyafikia mafanikio na nyota wengine wanaowika kisoka ndani na nje ya Afrika.

Lakini kama mikakati thabiti itawekwa, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) likaamua kufanya kweli katika kuwasaidia wanasoka wake, urasimu wa klabu kubwa za Simba na Yanga wa kutaka kukumbatia wachezaji wao kila kukicha ukiwekwa kando na wanasoka wenyewe wakijiamini kwamba wanaweza na wakawa tayari kujifunza, sina shaka soka ya Tanzania itapata ufufuko katika miaka ya hivi karibuni, hivyo kwenda sambamba na wenzetu wa nchi za Kusini, Kaskazini na Magharibi kwa Afrika.

Na hili linawezekana kutokana na ukweli kwamba, umri wa wachezaji wa sasa wa Taifa Stars inayonolewa na Mbrazil Marcio Maximo, kwa ujumla unatia moyo kwamba wanafundishika na watakuwa na muda mrefu wa kucheza soka.

Na Tutafakari.

Eric Anthony Mkuti [eric_anthonymkuti@yahoo.co.uk]

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version