*Hispania matumaini mapya
Wakati Ufaransa wametangaza kutorejea tena kwa mechi za Ligi Kuu – Ligue A kwa msimu huu na kuwapa Paris Saint-Germain (PSG) ubingwa, kuna matumaini kwamba Hispania watarejea uwanjani hivi karibuni.
Waziri Mkuu wa Ufaransa, Edouard Philippe ametangaza kwamba hapatakuwapo na mechi za soka ya ushindani nchini kote hadi Septemba, ikitegemeana na hali itakuwaje wakati huo.
Kwa msingi huo, ikamaanisha kwamba Ligue A na Ligue B, kwa maana ya ligi kuu na ligio daraja la kwanza vinamalizika mara moja kwa msimu huu wa 2019/2020. Mechi nchini humo zilisitishwa tangu mwnazoni mwa Machi mwaka huu kutokana na virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Baadhi ya wachezaji wamekubali kuondokana na asilimia 50 ya mishahara yao, kwa kusogezwa mbele muda wa malipo kwa ajili ya kusaidia klabu zao wakati huu wa janga la Covid-19 kwa vile wenye dhamana ya utangazaji wa mechi na haki za televisheni wameshikilia kima fulani cha fedha.
Akihutubia Bunge la Taifa, Philippe alisema kwamba Ufaransa hawataki kuwatia watu hatarini na kusababisha kusambaa tena kwa kasi kwa virusi hivyo hatari.
“Mashindano makubwa ya michezo hayawezi kuanza tena nchini hadi Septemba. Msimu wa klabu za wachezaji wa kulipwa wa 2019/2020 hauwezi kurejea tena,” akasema na kuongeza kwamba ni marufuku kuwapo shughuli itakayowakutanisha washiriki zaidi ya 5,000.
Kutokana na hatua hiyo, waratibu wa ligi hiyo – Ligue de Football Professionnel (LFP) wamewapa PSG ubingwa. Klabu hiyo walikuwa na alama 12 ziadi ya waliokuwa wanawafuatia kileleni mwa jedwali la msimamo wa ligi.
Tayari klabu wamesema kwamba wanatoa taji hilo kwa heshima ya wafanyakazi wa sekta ya afya na mashujaa walio mstari wa mbele katika kupambana na janga la Covid-19.
Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji wa PSG, Nasser Al-Khelaifi anasema kwamba wafanyakazi wa sekta muhimu nchini Ufaransa wanaoendelea kuchapa kazi wamejitoa sadaka na wanahitaji pongezi na shukurani nyingi, na PSG inatoa kwao hizo.
Wiki iliyopita, watangazaji wa mechi hizo kubwa – BeIN Sports na Canal+ walikubaliana kwamba watawalipa LFP kiasi cha fedha za haki ya matngazo, baada ya kuwa wameshikilia kadiri ya €130m pale mechi zilipositishwa kwa muda usiojulikana. Kiasi kilichobaki kilitarajiwa kulipwa mwishoni mwa Juni, na klabu zimejulishwa kwamba zitalipwa kwa ukamilifu kwa mujibu wa mkataba licha ya msimu kutorejea.
“Tunaheshimu mwenendo, mchakato na uamuzi wa Serikali ya Ufaransa,” akasema Al-Khelaifi, akiongeza kwamba timu yake inadhamiria kuendelea kucheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) ambayo kwa msimu huu haijakamilika. Kwamba wapo tayari kusafiri kwenda nchi nyingine kwa ajili ya kucheza kukamilisha mashindano hayo makubwa zaidi kwa klabu katika Ulaya.
Kutoka Hispania, Ligi Kuu – La Liga inatarajiwa kurejea kwa ajili ya kukamilisha msimu wa 2019/2020. Waziri Mkuu Pedro Sanchez amesema kwamba wachezaji wa kulipwa wataruhusiwa kurejea kwenye kazi zao kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo – Mei 4.
Sanchez akasema kwamba watu wa michezo, wakiwamo wanasoka, wameruhusiwa kuendelea na misimu yao tofauti ya soka, ikiwa ni sehemu ya hatua nne za kupunguza ‘lockdown’ ya kitaifa kutokana na athari kubwa za virusi vya corona kwa watu wake.