Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) kimezitaka klabu kupunguza vitendo vya wachezaji kupiga mipira ya vichwa kwenye mazoezi na kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji.
Tamko hilo linakuja baada ya kuwapo hofu kwamba kupiga mipira vichwa sana huweza kuja kusababisha shida ya akili (dementia) baadaye miongoni mwa wanasoka husika, japokuwa bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja juu ya hilo.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonesha kwamba wapo wachezaji kadhaa waliokuwa wakipiga sana vichwa waliopata ugonjwa huo. PFA inataka uwapo wa mkakati wa uratibu mpana kwenye mchezo huo juu ya changamoto husika kwa ajili ya kupima, kufuatilia, kusimamia na kurekebisha mfumo wa mazoezi na kulinda, ili kuwakinga wachezaji katika muda mrefu.
Utafiti uliofanyika mwaka jana ambao uligharimiwa na PFA ulimaizi kwamba wanasoka wana mara 3.5 ya vifo kuliko watu wengine, tatizo likihusishwa na matatizo yanayosababishwa kwenye mfumo wa neva.
Nobby Stiles na Jack Charlton walipoteza maisha baada ya kupambana na matatizo kama hayo wakati mkongwe wa zamani wa soka, Sir Bobby Charlton majuzi amegunduliwa kuwa na ugonjwa huo.
“Sayansi imekuwa ikiendelezwa haraka kwenye eneo hili na tunahitaji kuchukua hatua haraka ili kupunguza madhara kwa kuzingatia ushahidi uliopo sasa,” anasema Mwenyekiti wa PFA, Ben Purkiss.
Mtendaji Mkuu wa PFA, Gordon Taylor anasema kwamba PFA pamoja na Wakfu ya PFA wataendelea na kujitolea kwao, kwa kushirikiana na Chama cha Soka (FA) kwa ajili ya kugharamia utafiti kwenye eneo hilo. Hata hivyo, anasema kwamba kwa muda huu soka haiwezi kuacha mambo yaendelee yalivyo.
Inaelezwa kwamba Bodi ya Kimataifa ya Soka inatarajiwa kujadili suala linalohusiana na hilo Jumatatu, pamoja na kuweka ulazima wa wachezaji wanaoumia vichwa kutolewa uwanjani. Uamuzi wa mwisho utafanywa na mkutano mkuu unaofanyika mwezi ujao.